Pages

Pages

Wednesday, December 31, 2014

Cheka na King Class wapima uzito kwa ajili ya kutwangana Februari 28

Mratibu wa mpambano wa ubingwa wa UBO Africa Anthony Rutta katikati akiwainua mikono juu mabondia Cosmas Cheka kushoto na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa utambulisho wao watakaozipiga Februari 28 katika Ukumbi wa frends corner manzese Dar es Salaam picha zote na Super D.
Mabondia Cosmas Cheka kushoto akitunishiana misuli na Ibrhahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa utambulisho wa mpambano wao wa ubingwa wa U.B.O Africa utakaofanyika feb 28 katika ukumbi wa Frends Corner Manzese Dar es salaam.

Sheikh Shariff Matongo aibuka na mapya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015

Sheikh Shariff Matongo  akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake  jijini Dar es Salaam(hawapo pichani)kuhusu  ndoto yake ambayo ameoteshwa kuelekea mwaka 2015.

NA CHALILA KIBUDA, GLOBU YA JAMII,DAR.

Sheikh Sharif Matongo amesema ameoteshwa ndoto ya mwaka 2015 na kupata ushauri kwa mashekh mbalimbali duniani ambavyo vitatokea nchini na viongozi wasipuuze ndoto hiyo. Sharif aliyasema hayo leo ofisini kwake alipokutana na waandishi wa habari, alisema ameoteshwa mambo saba likiwemo la kupata Rais ajaye ambaye kiongozi ambaye muda mwingi ameishi nje ya nchi kwa kufanya kazi.

Alisema katika ndoto nyingine kifo cha kiongozi mkubwa  ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali na  na mwenye kambi katika Chama cha Mapinduzi (CCM). Sheikh  alisema ndoto nyingine  kutokea kwa mvua nyingi ambapo watu wanaoishi mabondeni ,kutokea kwa vifo vya watoto vingi ,wafanyabiashara kupata mafanikio  makubwa kwa mwaka utaoanza kesho.

Vijana wengi watashinda katika uchaguzi ujao na wazee wataangushwa sana ihivyo wanatakiwa kujitokeza, katiba inayopendekezwa  itapita lakini kutakuwa na vurugu ambazo zitaibuliwa na vijana.

‘’Ndoto yangu  nilioteshwa sikukaanyo peke yangu niliweza kupata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Mufti wa Abuu Dhabi, Mufti wa Nigeria  na wengine wote wakaniambia suala hilo nisikae nalo nishirikishe na watanzania wenzangu,’’alisema Sheikh Shariff Matongo.

Sheikh Shariff alisema katika usafiri wa bahari utakuwa mbaya kutokana na bahari kuchafuka na chombo kimoja kitazama kutokana na kuchafuka huko.

Alisema ndoto hizo ni lazima kuweza kuzingatia kutokana na kupata ushauri wa watu wengi wenye kuaminika katika jamii katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Tuesday, December 30, 2014

Moto mkubwa wazuka Handeni Mjini muda huu baada ya gari la mafuta kugonga nguzo ya umeme



HABARI za kusikitisha ni kwamba moto mkubwa unaendelea kuwaka Handeni Mjini, mkoani Tanga, baada ya gari la mafuta kuanguka kufuatia kugonga nguzo ya umeme na kumwaga mafuta.

Ajali hiyo imesababisha kuwaka kwa moto mkali ambao unatajwa kuweza kuleta athari kubwa, hasa kutokana na eneo lililowaka moto huo.

Taarifa kutoka kwa mashuhuda wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Pedeshee Kunguru zinasema kuwa juhudi za kuuzima moto huo zimechelewa kutokana na jeshi la polisi kuchelewa kufika.

Alipotafutwa Mkuu wa Polisi wilayani Handeni, OCD Tindwa, mwandishi wetu hajaweza kuelewana naye kutokana na simu yake kupokewa huku akiwa kwenye kelele nyingi.

Juhudi za taarifa kamili ya moto huo zinaendelea kusakwa na mwandishi wetu aliyopo ndani ya Handeni, akishuhudia kila kinachojiri katika ajali hiyo.

Kwa taarifa za awali, moto huo umewaka kutoka katika barabara ya Songe, karibu na duka kubwa la mtu aliyetambuliwa kwa jina la John Shayo, huku ukishuka katika maeneo yenye hoteli.

 

Msimu wa tatu wa The Mboni Show kuanza Januari 2

Mkurugenzi wa Mboni Show, Mboni Masimba (wa pili ktoka kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana katika  ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kuanza kwa msimu wa tatu wa kipindi chake 'The Mboni Show' kinachotarajia kuanza Jan 2, 2015. Kushoto ni kiti Simpompa na kuanzia kulia ni Afisa Masoko wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (PSPF) Magira Werema na Kaimu Mkurugenzi wa Masoko TBC,Bw.Fadhili Chilumba.
Kutoka Kulia Afisa Masoko wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (PSPF) Magira Werema akizungumza wakati wa uzinduzi kipindi cha Mboni Show uliofanyika katika Ukumbi wa Idara Habari Maelezo jijini Dar es Salaam. Pembeni ni Kaimu Mkurugenzi wa Masoko TBC,Bw.Fadhili Chilumba pamoja na Mkurugenzi wa Mboni Show, Mboni Masimba.
Na Mwandishi Wetu.
Mkurugenzi wa Mboni Show, Mboni Masimba ameamua kuhamishia kipindi cha Mboni show katika kituo cha utangazaji cha Taifa (TBC) kutoka EATV ili kuvutia watazamaji wengi na wapya kwa wazee pamoja na vijana.
Kipindi cha Mboni Show kitaanza kurushwa TBC kuanzia January 2 mwaka 2015 siku ya
Ijumaa saa 3 Usiku-4 Usiku na marudio Jumanne saa 9:00 mchana-10:00mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar ndani ya ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mboni Masimba ametoa shukrani kwa EATV kwa ushirikiano wao kwa kipindi chote alichokuwa nao,na kusema kuwa amehamishia kipindi cha Mboni Show katika kituo cha TBC ili kuvutia watazamaji wengi hakuna atakaye tumia jina la Mboni Show na hakuna kitakachomkwamisha kwa vile ana hati miliki.

Bayport yamjaza mapesa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza MUCE kutoka kwenye fao la Bima ya Elimu

Mratibu wa Bima ya Elimu ya Bayport Tanzania, Ruth Bura kulia, akizungumza jambo katika makabidhiano ya hundi kwa bwana  Kennedy Kaupenda kushoto kwake, Makao Makuu ya Bayport, mapema wiki hii. Picha zote na Mpigapicha Wetu.

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM 
TAASISI ya kifedha ya inayojihusisha na mambo ya mikopo ya Bayport Tanzania, imempatia Sh Milioni tatu mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE), Kennedy Kaupenda, kufuatia huduma mpya ya Bima ya Elimu inayoendeshwa na taasisi hiyo nchini.

Huduma hiyo mpya ya Bima ya Elimu ya Bayport Tanzania ilianza mapema mwaka huu kwa ajili ya kuwapatia fursa wanafunzi kuendelea na masomo baada ya mzazi aliyejiunga na huduma hiyo kufariki Dunia.

Mwanafunzi wa MUCE, Kennedy Kaupenda kushoto, akizungumza baada ya kukabidhiwa hundi yake ya Sh Milioni 3 kutoka kwenye Bima ya Elimu inayoendeshwa na Bayport. Kulia kwake ni Mratibu wa Bima hiyo, Ruth Bura.   

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Bima ya Elimu inayotolewa na Bayport Tanzania, Ruth Bura, alisema Kaupenda alitajwa kama mnufaika kwa mzazi wake aliyefariki Dunia, hivyo waliamua kumtafuta kwa ajili ya kumpatia mafao yake kwa ajili ya kuendelea kupata elimu bila vipingamizi vyovyote.

Alisema huduma hiyo ina vipengele vine ambavyo ni Bronze, Gold, Silver na Exucutive, huku akisema kuwa makato ya kila mwezi ya Bronze ni Sh 2,500, ambapo fao lake ni Sh Milioni 3, wakati makato ya Gold ni Sh 6,250, huku fao lake likiwa ni Sh 7,500,000.
Ruth Bura, Mratibu wa Bima ya Elimu Bayport Tanzania kulia akimkabidhi hundi bwana Kennedy Kaupenda kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu baada ya kufariki mzazi wake.

Monday, December 22, 2014

Kizazi kipya waliteka tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014



Na Mwandishi Wetu, Handeni
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, msimu wa pili wa tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014 lililofanyika katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Desemba 20, ulimalizika huku wasanii wa muziki wa kizazi wilayani hapa, wakiliteka tamasha hilo lenye mguso wa aina yake.

Wasanii hao wanaofanya vizuri wilayani Handeni na mkoa mzima wa Tanga, wakiongozwa na RSK Kibajaji, Diki Mani na kundi la WC, walionyesha uwezo wa juu kiasi cha kuvipoteza vikundi vya ngoma za asili vilivyokuwapo katika tamasha hilo.

Awali, wasanii hao walipangwa kama sehemu ya kunogesha tu na pia kuwapa nafasi ya kujitangaza ili wafikie malengo yao, lakini uwezo wa kuimba, ubunifu na ujuzi wa kulishambulia jukwaa kuliwafanya wasanii hao washangiliwe muda wote uwanjani hapo.

Akizungumza katika tamasha hilo, Mratibu Mkuu, Kambi Mbwana, alisema kwamba waliamua kuwaalika wasanii wa kizazi kipya ili kuwatangaza, jambo ambalo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa hasa pale vijana hao walipoweka ubunifu wa hali ya juu katika kazi zao.

“Hawa wasanii waliweza kuchanganya lugha katika mashairi yao, kuimba nyimbo zinazoelezea mazingira ya Handeni na mkoa wa Tanga, bila kusahau kuhamasisha mambo ya kimaendeleo sambamba na kuelimisha wahudhuriaji namna ya kusomesha watoto wao.

"Hii iliwafanya mashabiki, wadau na wahudhuriaji washindwe kukaa kwenye viti vyao kutokana na kazi nzuri ya wasanii hao ambao kwa kiasi kikubwa wanaonyesha vipaji na uwezo mkubwa wa kushambulia jukwaa,” alisema.

Naye mgeni rasmi katika tamasha hilo, ambaye ni Katibu Tawala wa wilaya ya Handeni, John Ticky, aliyemuwakilisha Mkuu wa wilaya Muhingo Rweyemamu, alilimwagia sifa tamasha hilo kwa hatua ya kuitangaza Handeni, sanjari na mafanikio yake kwa ujumla.

“Hili ni tamasha zuri mno maana limechanganya burudani ukizingatia kuwa sera zao zinachangia maendeleo kwa kiasi kikubwa mno, hivyo kama sehemu ya serikali naomba juhudi hizi ziendelee kwa maendeleo ya Taifa letu,”  alisema.

Nao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF ambao ndio wadhamini wakuu wakiwakilishwa na Meneja Mkoa Tanga, Frank Maduga, alisema tamasha la Handeni Kwetu limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mkoa mzima wa Tanga, jambo linalowafanya waliunge mkono na kuwataka pia Watanzania wote wajiunge na mfumo wa hifadhi wa NSSF Tanzania, hususan wakazi wa Handeni na mkoa wa Tanga.

NSSF tunajivunia kwa kiasi kikubwa kuwa wadhamini wa tamasha hili ambalo kwa mwaka huu tumeshuhudia wananchi wakielimishwa umuhimu wa kuwa wanachama ambapo wengine walivutiwa na kujiunga moja kwa moja kwenye mfuko wetu wakati tamasha linaendelea uwanjani hapo,” alisema Maduga.

Naye Candy Masunzu, Meneja wa Taasisi inayojihusisha na mikopo, Bayport Tanzania ambao pia walikuwa wawezeshaji wa tamasha hilo, alisema Handeni Kwetu ni moja ya matukio makubwa yenye kuburudisha na kuelimisha sanjari na kukuza uchumi wa Taifa, huku akiwataka Watanzania kuchangamkia fursa ya mikopo kwenye taasisi yao ili wakuze uchumi wao.

Wadhamini wengine wa tamasha hilo lililoshirikisha vikundi mbalimbali vya ngoma za utamaduni wilayani Handeni, ukiacha NSSF na Bayport Tanzania ni pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.


Sunday, December 07, 2014

Tamasha la NSSF Handeni Kwetu sasa Desemba 20



Na Mwandishi Wetu, Handeni
TAMASHA la Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu, sasa litafanyika Desemba 20, badala ya Desemba 13, kama ilivyotangazwa hapo awali, huku sababu kubwa ikiwa ni kuwaachia Watanzania washiriki katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika Jumapili ya Desemba 14 nchini kote.
Mratibu Mkuu wa Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, pichani akizungumza jambo katika tamasha la mwaka jana lililofanyika kwa mafanikio makubwa wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Akizungumzia hilo leo mjini Handeni, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kwamba hatua ya kusogeza mbele kwa wiki moja, ni kutokana na mguso wa tukio lenyewe na nia ya kuwashirikisha Watanzania wote ili kuliweka tamasha lao katika kiwango cha juu.

Alisema kuwa Desemba 13 ni siku ya mwisho kwa kampeni za ugombea uenyekiti wa serikali za mitaa, vitongoji na mitaa, hivyo kwa kushauriana na jeshi la Polisi wilayani Handeni, wamekubaliana kulifanya Desemba 20.

“Tumeangalia mambo mengi sana hadi kukubaliana lifanyike Desemba 20, ikiwa ni kukosekana kwa wengi, wakiwamo Wakurugenzi ambao kimsingi wao ndio wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mengi.

“Tunaamini kwa kufanyika Desemba 20, tamasha litakuwa kwenye mvuto pamoja na kukwepa malalamiko kwa baadhi ya wanasiasa ambao huenda wangelalamika endapo lolote lingetokea huku wao kushindwa uchaguzi wao,” alisema Mbwana.

Mbwana alitumia muda huo kuwaomba radhi wadau wote, wakiwamo wasanii, wadhamini na wale waliokuwa wamepanga kutembelea Handeni Desemba 13, huku akiwataka safari yao ifanyike kwa ajili ya Desemba 20, ukizingatia kuwa wote wanaweza kushiriki chaguzi zao na kupata muda mkubwa wa kutembelea wilayani Handeni na mkoa mzima wa Tanga kumaliza mwaka wao vizuri.

 Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.