Pages

Pages

Thursday, November 20, 2014

Wananchi wa Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga waipinga Halmashauri ya Mji

Na Mwandishi Wetu, Handeni

MKUTANO wa kwanza wa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation uliyofanyika jana Novemba 19, katika kijiji cha Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kuwakutanisha wananchi wote umeibua kero nyingi za wananchi, ikiwamo ya kijiji chao kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji bila ridhaa yao.

Mmoja wa wakazi na wananchi wa kijiji cha Misima, akilalamikia eneo lao kuingia kwenye Halmashauri ya Mji kinyume cha sheria ya utawala bora, ikiwa ni pamoja na kutoshirikishwa kwa lolote na viongozi wa juu.
Taasisi hiyo ilianzishwa mapema mwaka huu na kuzinduliwa Mei 8 jijini Dar es Salaam, ilifanya mkutano mkubwa wa hadhara Misima, ambapo umati wa wanchi ulihudhuria, huku kero nyingi zikiwasilishwa na kudhihirisha changamoto za utawala bora zinazoathiri maendeleo ya Tanzania.

Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, mwananchi wa Misima aliyejitambulisha kwa jina la Mhina Ally, alisema viongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na madiwani waliamua kuingiza kijiji chao katika Halmashauri ya Mji bila ya kuwashirikisha, ikiwamo kubandika tangazo la pingamizi kwa siku 90 katika maeneo yao kama sheria inavyotaka.

Alisema kutoka Handeni Mjini hadi katika eneo lao ni kilomita 16 zilizozunguukwa na mapori yanayowafanya wananchi wajihusishe na kilimo kwa asilimia 99, hivyo kuingizwa kwenye sheria za mji ni kusababisha ugumu wa maisha.

“Inashangaza mno kusikia Tanzania kuna utawala bora wakati viongozi wachache wanaweza kufanya watakavyo; hali inayoweza kuleta mapigano makubwa, endapo wananchi tutasimama kidete kudai haki zetu zinazokandamizwa na viongozi kila siku,” alisema.

Ally alifika mbali zaidi kwa kusema walisikia tangazo redioni la kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji, huku tangazo la pingamizi likishindwa kuwekwa kijijini kwao kwa hofu ya kupingwa na wananchi wao.

“Viongozi wa serikali ya kijiji waliamua kutoliweka tangazo la pingamizi kijijini kwetu kwasababu wanajua fika tusingekubali, hivyo inashangaza malalamiko yetu kufumbiwa macho na serikali inayoitwa sikivu, licha ya kuzunguuka sehemu nyinyi, kama kwa Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Tanga, alipokaimu DC Halima Dendego, ambaye sasa amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,” aliongeza.

Naye Naye Idd Kisege alisema kuwa ili kuona viongozi wanaogopa kufika Misima, hata namba kwenye nyumba zao hakuna ingawa wanatangaza uchaguzi kwa sheria za mji katika kijiji chao, jambo lisiloweza kuvumiliwa na kila mpenda maendeleo ya Misima.

“Watu wa Misima tunaambiwa sisi ni watata, wakorofi tunapodai haki zetu, ili waendelee kutuburuza, ndio maana kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete waliniburuza Polisi kwasababu ya kuonyesha bango kwa mheshimiwa ili kuona kero zetu,” alisema Kisege.

Naye Mkomwa Athuman alisema kuwa Misima haipo tayari kutumikia sheria za Mji kwakuwa ni mapema mno kwao, hivyo wanaomba serikali, ikiwamo ofisi ya Waziri kulifuatilia suala hilo kwa kina.

“Mzozo huu umeshakuwa mkubwa na kuondoa ushirikiano kabisa kwa viongozi na wananchi wa hapa Misima, hivyo tayari malalamiko yetu yamefikishwa Ofisi ya Waziri Mkuu kulishtakia suala hilo kwasababu sheria ya kuingia kwenye Mamlaka ya Mji Handeni haijafuatwa na imeanzishwa na watu wachache ili kuzima uozo wa ardhi waliyoufanya kwenye kijiji chetu,” alisema.

Katika kila mwananchi aliyezungumza kwenye mkutano huo alionyesha kuguswa na kero hiyo ya mji, huku wakisema kutoka Handeni Mjini hadi Misima ni mbali pamoja na viongozi kushindwa kufuata sheria za utawala bora.

Awali, mkutano huo ulioanza saa tisa alasiri ulifunguliwa na mtoa mada wa kwanza, Kambi Mbwana, ambaye ndiye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, aliyejikita sababu na dhamira kuu ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Mbwana alisema kuwa sababu kubwa ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha utawala bora, ikiwa ni njia moja wapo ya kuwafanya Watanzania wote wajiletee maendeleo kwa kushirikiana baina yao na viongozi wote.

Akizungumzia utawala bora, Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Adam Malinda, alisema kwamba matatizo mengi katika jamii yamekuwa yakichangiwa na viongozi wasiojua nini maana ya utawala bora.

“Utawala bora ni somo muhimu na lazima lipigiwe kelele na watu wote, maana malalamiko mengi ya watu wa Misima yamesababishwa na tatizo hilo, ndio maana unaona kero zimepamba moto,” alisema.

Malinda aliwataka viongozi wa juu, wakiwamo wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuzungumza na wananchi wa Misima ili kutatua mtafaruku huo kwa ajili ya kuwafanya wananchi waendelee na shughuli za kujiletea maendeleo, sambamba na serikali kuwafanyia kazi watendaji wabovu.

Kuhusiana na mzozo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alikaririwa akisema kuwa utaratibu ulifuatwa, ikiwamo kutoka kwa siku 60 za pingamizi, ingawa wananchi hao walishindwa kupita njia hiyto kwa ajili ya kufanikisha malengo yao.



No comments:

Post a Comment