Pages

Pages

Monday, November 10, 2014

SIWEZI KUVUMILIA:Kwanza soka lichezwe, jezi wakati mwingine

Na Kambi Mbwana, Handeni
WAZEE wa zamani walikuwa na makusudi yao kuweka msemo usemao sikio la kufa halisikii dawa. Na wakati mwingine wanasema siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Misemo hii na mingine mingi inaelezea namna gani hutokea matatizo yanayokosa jinsi ya kuyatatua.


Ninaposema hili, najikuta nikikosa hamu ya kusikiliza au kusikia porojo zinazoitwa kuendeleza soka la Tanzania, chini ya Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF),  Jamal Malinzi. Malinzi aliyeingia madarakani hivi karibuni akirithi mikoba ya Leodgar Tenga, amekuwa akikabiliwa na matizo mengi, kiasi cha kuamini kuwa sikio la kufa halisikii dawa.


Hakika siwezi kuvumilia; TFF eti inajaribu kuangalia namna ya kuboresha jezi za timu ya Taifa, Taifa Stars. Sasa jezi zinasaidia nini? Hata tukivaa jezi za aina gani, kama hatuna soka zuri tunanufaika na kitu gani?


Huu ni ubabaishaji uliyoje? Malinzi na jopo lake kubwa analoteua kila uchao anapaswa kuwa makini mno ili asiharibu mwenendo wake mzuri. Kinyume cha hapo ni hasara tupu. Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo iliwahi kutangaza mchakato wa vazi la Taifa. Hadi leo haijulikani mchakato huo umeishia wapi?


Eti mshindi wa jezi ya nyumbani atapewa Sh Milioni moja kama atakavyopewa mshindi atakayebuni jezi za ugenini. Huku ni kupotezeana muda. Hizo Milioni 2 kama zipo TFF si alete mashindano japo ya Kata au wilaya?


Hizo Milioni 2 zinaweza kununulia vifaa vya michezo na kuwapa vijana wanaopenda kucheza soka ili hali hawana vifaa vya michezo? Hakika siwezi kuvumilia. Kwa upande wangu sikuwa na hamu kabisa ya kumlaumu Malinzi. Lakini kadri muda unavyosonga mbele kunafanyika matatizo yanayovunja ukimya.


Au pia wakati mchakato huo unaundwa, pengine kumeshapatikana mshindi na kuna kitu kinataka kufanywa. Malinzi, jezi hazina manufaa kwa sasa. Wala usisimbuke kuzibadilisha au kuziboresha maana zipo.


Watanzania wanataka soka safi. Soka la kuvutia litakalotupandisha chati na kuwaita mawakala wa Kimataifa kwa ajili ya wachezaji wetu. Huu ndio ukweli unaonifanya nishindwe kuvumilia mchana na usiku.


Kinyume cha hapo, utendaji kazi wa TFF ya sasa ni kuboresha jezi na kuhama ofisi kama vile mambo hayo hayakuwapo kabla ya uongozi wao.


Tuonane wiki ijayo.

+255712053949

No comments:

Post a Comment