Pages

Pages

Sunday, July 13, 2014

Waziri Mkuu wa zamani Fredrick Sumaye aponda chagizo la ujana kugombea urais



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, amesema kila mtu ana haki ya kugombea urais, ila si muhimu agenda ya ujana ikaendelea kuungwa mkono, maana haina jipya wala faida katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.


Akizungumza katika kituo cha luninga cha Star Tv leo asubuhi, Sumaye pichani, alisema kwamba sera ya ujana haina mashiko, maana mtu anachaguliwa kutokana na sifa na vigezo alivyokuwa navyo.

Alisema hali hiyo inamfanya aone wasiwasi mkubwa kutokana na baadhi ya watu kuanza kupita kwa visingizio kuwa huu ni wakati wa ujana kupewa maajukumu makubwa yaa kiuongozi.

“Naweza kukubaliana na mahitaji ya watu wote wenye sifa ya kugombea uongozi, lakini si sahihi kofia ya ujana ikapewa chapuo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Sumaye alisema wapo baadhi ya watu wanafanya kazi kubwa kuwanunua wa kuwaunga mkono jambo ambalo si sahihi na linapaswa kuangaliwa upya na Watanzania wote.

Alisema mwanasiasa wa aina hiyo akitoa fedha nyingi kununua watu wake, matokeo yake ni magumu kwasababu anaweza kuingiza nchi kwenye hatari kubwa.

“Mtu kama amepewa fedha nyingi ili apate uongozi kutoka kwa watu wake, akiwa rais huyo sidhani kama anaweza kusimamia jukumu zito la ulipaji kodi,” alisema.

Kwa mujibu wa Sumaye, chama kina utaratibu wake wa kuwapata viongozi, hivyo hakuna shaka utasimamiwa vizuri sanjari na kupambana na watoa rushwa, maana nchi itaingia kubaya.

No comments:

Post a Comment