Pages

Pages

Thursday, July 24, 2014

Taasisi ya Handeni Kwetu Foundation kuzinduliwa August 5

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 
SIKU chache baada ya kusajiliwa rasmi chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Taasisi inayojulikana kama Handeni Kwetu Foundation, imepangwa kuzinduliwa August 5 mwaka huu, katika Ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutafuta namna ya kusaidiana na serikali katika mambo mbalimbali, ikiwamo Kujenga uwezo kwa jamii kujikwamua kiuchumi na kuhamasisha utawala.

Akizungumza hilo, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, alisema taasisi hiyo imeanzishwa na itafanya kazi zake bila kuvunja masharti yaliyowekwa na serikali ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanapatikana.

Alisema kuwa taratibu za kuelekea kwenye uzinduzi huo zinaendelea kuwekwa katika hali ya kukutana pamoja kwa wageni walioalikwa kushuhudia uzinduzi huo wa aina yake.

“Kwa miezi kadhaa sasa taasisi ilikuwa kwenye mchakato wa usajili wake, hivyo baada ya kukamilika, kinachofuata sasa ni kuzindua ili ianze kazi zake kama ilivyokusudia.

“Taasisi hii itakuwa na Makao yake Makuu wilayani Handeni, lakini itafanya kazi zake nchi nzima na huko mbele itakuwa na ofisi katika kila eneo itakaloona inafaa,” alisema.

Sababu nyingine za kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuleta ustawi kwa jamii katika njanya mbalimbali, kutoa mafunzo kuhusu kilimo bora na jinsi ya kutafuta masoko, kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha misingi ya utawala bora, kutoa elimu na ushauri kuhusu mbinu bora za kuimarisha  afya na elimu ya msingi kuhusu Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Malengo mengine ni kutoa elimu kuhusu makundi rika katika elimu ya uzazi, kuhamasisha na kushawishi jamii kuzingatia ustawi wa mtoto katika jamii, kufanya utetezi kwa makundi maalum ambayo haki zao zinakiukwa na kufanya tafiti mbalimbali zenye malengo ya kuboresha maisha ya jamii, kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment