Pages

Pages

Thursday, July 24, 2014

Kumekucha tamasha la Saba la Muziki wa Cigogo 2014

Na   Andrew Chale, Dodoma

SHAMRA shamra za tamasha la Muziki wa Cigogo zitatarajia kulipuka hiyo kesho Julai 25, kwenye kijiji cha Chamwino Ikulu, Mkoani hapa kwa kushuhudia vikundi zaidi ya 30, vikiwasha moto wa ngoma na muziki wa kitamaduni  hu ku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi  akitarajiwa kulifungua rasmi.


Katika kukuza na kuendeleza sanaa nchini, tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu ni la msimu wa  Saba (7) likifahamika kama (Wagogo music festival 2014)  lenye kauli mbiu  ‘Utamaduni na Amani’ linatarajia kulindima kwa siku tatu, Julai 25 hadi 27, Kijijini hapo  Chamwino Ikulu.


Akizungumza na waandishi wa habari  katika mkutano uliofanyika mapema leo kwenye ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi mkuu wa tamasha hilo, Dk. Kedmon Mapana,  wa Kituo cha Sanaa Chamwino (Chamwino Arts Center-CAC) alisema jumla ya vikundi  31 vinatarajiwa kushiriki tamasha hilo.


“Tamasha la Wagogo mwaka huu ni la saba, ambapo shamrashamra ya tamasha hilo zinatarajia kuanza majira ya saa nane mchana Mkuu wa Mkoa atakapolifungua rasmi huku tukitaraji pia kuwa na wageni wasiopungua 1000” alisema Dr. Kedmon Mapana.


Na kuongeza kuwa, kituo hicho cha CAC  kimekuwa kikiandaa tamasha hilo kila mwaka huku lengo kuu likiwa ni kudumisha mila na tamaduni za Wagogo.


Aidha, alisema jumla ya wasanii 750 wanaotoka kwenye vikundi hivyo 31,  wanatarajia watawasha moto wa aina yake kwa kuonyesha sanaa ya muziki wa kabila hilo.


“Miaka ya nyuma tulikuwa na vikundi vya kutoka hapahapa Chamwino na baadae kutoka ndani ya Mkoa wetu pekee, lakini kwa sasa tumeamua kualika na makabila jirani.. wapo wanaotoka Dar es Salaam, Pwani, Singida na Visiwani Zanzibar hivyo wote kwa pamoja tutadumisha utamaduni wetu” alisema Dr. Kedmon Mapana.


Dk. Mapana  pia alipongeza wafadhili wakuu wanalioliunga mkono tamasha hilo wakiwemo, Chamwino  Connect  na Schweizerische Eidgenossenschaft  (German).

Tamasha hilo pia uhudhuliwa na wageni mbalimbali kutoka mataifa ya nje, ikiwemo nchi za Ulaya, America, Asia na bara la Afrika, ambapo pia kunakuwa na warsha na makongamano katika vijiji vya Chamwino.

Aidha, alivitaja vikundi vitakavyoshiriki tamasha hilo ni pamoja na kutoka Dodoma kuwa ni New Pendo, Yelusalem, Inueni mioyo, Yeriko, Nyota njema, Ushirikiano, Nyerere na Ebenezer.


Vikundi  vilivyo vijiji vya Wilaya ya Chamwino ni  Upendo (Kijiji cha Dabalo),  Imani, Sinai  (Kijiji cha Membe).  Mchungaji mwema, (Kijiji cha Nzali), Juhudi, Muhubiri (Kijiji cha Kawawa), Nyota njema, Safina, Ndagwa (Kijiji cha Msanga).

Msifuni (Kijiji cha Mlimwa), Nyota, Ufunuo (Kijiji cha Majeleko), Simba (Kijiji cha Mbele zungu) na Inueni mioyo (Kijiji cha Mgunga).


Vikundi kutoka Wilaya ya Kongwa imani ( Kijiji cha Mkutani), Faru (Kijiji cha Songambele) na  Safina (Kijiji cha Chigwingili), Pia  kikundi cha Uvuke na Upendo  (kutoka  Manispaa ya  Dodoma mjini).


Vikundi vingine ni Mandoo/Tasuba kutoka Bagamoyo  Mkoa wa Pwani, Nazareti (Dar es s Salaam), Muungano (Manyoni, Singida) na  Zanzibar.

No comments:

Post a Comment