Pages

Pages

Tuesday, July 01, 2014

Simba wanahitaji maendeleo, si malumbano tena



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Juzi Juni 29, klabu ya soka ya Simba ilifanya uchaguzi wake mkuu baada ya mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, kumaliza muda wake wa miaka minne wa kuongoza.
Evans Aveva, pichani
Katika uchaguzi huo watu mbalimbali walijitokeza kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye klabu hiyo. Nafasi za juu za uongozi zilikuwa ni rais ambapo Evans Aveva alikuwa akichuana na Andrew Tupa na makamu wa rais ilikuwa ikigombewa na Geofrey Nyange Kaburu, Jamhuli Kihwelo ‘Julio’ na Swed Mkwabi. 

Sitaki kusema nani aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho ila kuwakumbusha wanachama wote na viongozi wapya walioingia madarakani kusimama kwenye ukweli, kuwa Simba haina maendeleo licha ya kuasisiwa miaka 1936.

 Hii ni aibu kubwa kwa klabu kama hii. Nilibahatika kutembelea maeneo mbalimbali kusikiliza kampeni za wagombea, hususan Temeke, Ilala na Kinondoni, ambapo kampeni zilifanyika katika Ukumbi wa Urafiki na kuhudhuriwa na watu wengi sana. 

Kila mmoja alikuwa akijaribu kuonyesha cheche zake juu ya nafasi anayogombea. Wote walionyesha wana kitu cha kufanya. Hata hivyo, mara nyingi mtu anapotaka jambo lake hutumia ufundi mwingi kuomba kura ikiwezekana hata kuongopa. 
Anafanya hivyo kwasababu anataka achaguliwe. Baada ya kuchaguliwa baadhi yao husahau na kufanya mambo yao binafsi. Hii si sahihi. Kwa klabu kama Simba inahitaji mipango na mikakati kabambe kwa ajili ya kuipatia maendeleo. 

Ajenda ya kwanza iwe kuijenga Simba imara na ya ushindi.
Hili likifanikiwa Simba itafanya vizuri kwenye ligi na mashindano mbalimbali ili kurudisha heshima na hadhi ya klabu hii kongwe. Ajenda ya pili iwe kuendeleza soka la vijana. 

Hii inajulikana kuwa Simba ilishaweka misingi ya kuendeleza vijana, ndio maana waliibuka akina Jonas Mkude, Ramadhan Singano na wengineo. 

Hili lifanyike bila kuangalia nani yupo madarakani kwasababu ni sera nzuri zenye manufaa kwa maendeleo ya Simba. Ajenda ya tatu ni kuhakikisha kuwa Simba inakuwa na uwanja wake wa kisasa ili kuondoa gharama za kukodi viwanja vya michezo.

 Imeshakuwa kero na aibu kubwa kwa Simba hii kongwe kukosa uwanja wake. Imezidiwa ujanja na Azam FC iliyozaliwa miaka ya karibuni. 

Ndio, Azam inamilikiwa na mfanyabiashara inajimudu. Lakini katika msingi wa soka la Tanzania mtaji mkubwa kwa klabu hizi ni watu.

Simba ina wanachama wengi bila kusahau mashabiki nchini kote. Ina uwezo wa kufanya lolote kutokana na hadhira ya mashabiki wao.
Hii ni tofauti na Azam wanaosubiri mashabiki kutoka Simba au Yanga. 

Aidha viongozi hao wapya lazima wafahamu kuwa ili waendelee ni pamoja na kuiendesha klabu kibiashara.

 Kuleta umoja, utulivu na mshikamano ili kuwavutia wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuwekeza kwenye klabu hii. Kampuni inayojitambua haiwezi kuingia mkenge kwa klabu isiyokuwa na dira. Klabu inayozalisha mizozo kila baada ya miezi miwili. 

Nasema hili huku nikiamini kuwa utawala wa Rage ulikuwa na kasumba. Mengi yalisemwa na kusikika mchana na usiku. Wapo walioambiwa ni mambumbumbu. Wapo walioambiwa barua zao ni za uchumba si za kikazi.

 Hili liliweza kuwavunja moyo wanachama na kujikuta kuisusa timu yao. Ikafikia hatua mbaya Simba kuingiza mapato madogo uwanjani sambamba na kupata matokeo mabaya uwanjani. 

Kutokana na hilo, najikuta nikiwakumbusha viongozi wapya wa Simba kufanya kazi kama timu moja kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao kongwe. 

Watu wanataka maendeleo si porojo za kikampeni. Wahakikishe kuwa wanakaa chini kubuni sera, miradi kwa maendeleo yao. Waunde timu yenye ushindi, sanjari na kuzalisha mapenzi mema kwa klabu hii ya Tanzania Bara. 

Simba ina wadau wengi. Inao viongozi wa juu wa Serikali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Iwatumie hao kutafuta vyanzo vya mapato vya klabu badala ya kuchangishana kila siku.

 Kwa kufanya hivyo, tunaamini Simba itajiendesha yenyewe na si kutegemea fedha za wafadhili zilizoanza kulalamikiwa na baadhi ya Watanzania, huku ikidaiwa kuwa wafadhili hao wapo kwa ajili ya kuinyonya Simba. 

Mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Friends of Simba, Zacharia Hanspope alitumia muda mwingi kuwaelezea wanahabari uwapo wa kundi hilo na faida yake. 

Mengi aliyosema yana ukweli. Pope alisema ili Simba iweze kujitegemea yenyewe kunahitaji mipango na si porojo tu za kampeni. Pia akasema ghafla haiwezi kujiendesha maana haina vyanzo vingi vya mapato na inahitaji fedha nyingi za usajili, gharama za safari, maandalizi ya ligi na gharama nyingine lukuki. 

Ukisitisha ufadhili hasa fedha za wana Simba, nani mwingine atachangia wakati mapato ya milangoni ni kiduchu? Haya ni maswali muhimu ambayo mwisho wa siku utagundua yana tija. Ili upate 10 ni lazima uanze kwanza na moja. 

Hivyo naamini kwa pamoja klabu hii itapiga hatua kama itawatumia watu wake kusimamia sera na mipango ya klabu. Yale yaliyoahidiwa kwenye kampeni, yale yenye tija basi yasimamiwe kwa vitendo ili kuona klabu inapiga hatua kubwa ndani na nje ya nchi.
kambimbwana@yahoo.com
 +255712053949

No comments:

Post a Comment