Pages

Pages

Saturday, July 05, 2014

Michael Wambura apingana na Rais wa Simba,Evans Aveva



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa zamani wa Simba, Michael Wambura amepingana na maamuzi ya Rais wa Simba, Evans Aveva ya kupeleka hoja ya kujadiliwa uanachama wake kwenye Mkutano Mkuu wa timu hiyo, unaotarajia kufanyika Agosti 3 mwaka huu akidai ameshasafishwa na Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
 
Juzi Aveva alitangaza kuwasimamisha uanachama wanachama 69, waliofungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ya kusimamisha uchaguzi wa Simba uliofanyika Jumapili iliyopita, pamoja na kujadili uanachama wa Wambura, ambaye naye aliipeleka Simba mahakamani mwaka 2010.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Wambura aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa madai ya kufanya kampeni kabla ya muda alisema, Kamati hiyo ya TFF ilithibitisha kuwa yeye ni mwanachama halali ingawa alienguliwa kugombea kwa kosa hilo la kampeni, huku akidai kuwasimamisha wanachama hao kutaongeza makundi kwenye timu hiyo.

“Hilo mimi sioni kama kuna sababu ya kulijadili lakini nawataka Kamati hii iliyoingia madarakani kufuta maamuzi yao ya kuwasimamisha wanachama hawa, kwani hawajatenda haki kwa mujibu wa Katiba ya Simba ibara ya 41(d) kwa kuwanyima wanachama fursa ya kujitetea na kusikilizwa kabla ya kuchukua hatua , hivyo ni uvunjifu wa haki za msingi za binadamu. Kama zinavyoainishwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13(6)a pamoja na kanuni za nidhamu za FIFA ibara ya 94(1) na kanuni za adhabu za TFF Ibara ya 35 (1),” alisema.


Wambura pia amedai kuwa, kusimamishwa wanachama hao ni kusababisha mpasuko kwa klabu hiyo na wameenda kinyume cha utaratibu wa katiba ya Serikali, TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hivyo wametumia udikteta.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya Simba Ibara ya 54 (3), uamuzi wowote wa kufukuza wanachama lazima upigiwe kura za siri na wajumbe theluthi mbili waunge mkono na ndipo maamuzi yafikiwe, lakini sio kama walivyofanya wao hivyo hali hii italeta matabaka mawili ya wanaounga mkono uongozi na wanaopingana nao.

Alisema uongozi wa Aveva, hauwezi kupambana na wanachama zaidi ya 500 na hawataweza vita hiyo zaidi watasababisha migogoro, hivyo wakae chini na kuliangalia hilo ambapo atawapelekea nakala yake ya taarifa hiyo aliyoisoma kwenye vyombo vya habari kama ushauri.

Licha ya Wambura kutetea wanachama hao ambao walikuwa wakimuunga mkono, lakini anakinzana na katiba ya Simba ibara ya 11(1)b inayokataza kupeleka masuala ya soka mahakamani, sambamba na ibara ya 55 inayofafanua adhabu ya atakayetenda kosa hilo, ambayo ni kusimamishwa uanachama na baadaye kujadiliwa kwenye mkutano mkuu.

No comments:

Post a Comment