Pages

Pages

Wednesday, June 11, 2014

Usafiri wa treni za abiria wasitishwa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
UONGOZI wa Kampuni ya Reli Tanzania – TRL unawataarifu abiria wote na wananchi kwa jumla kuwa kutokana na kutetereka kwa mojawapo ya madaraja katika bonde la mto Ruvu katika reli ya kati , umeamua kusitisha kwa muda huduma ya usafiri wa abiria hadi ukarabati wa daraja utakapokamilika.

Hapo jana Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu na Wahandisi waandamizi na Mafundi Mchundo Ujenzi walifika katika daraja hilo lililopo km 82/5 na kulifanyia tathmini ili kuona uharibifu uliotokea na mahitaji kuliimarisha ili lirejee katika kiwango cha usalama kuruhusu treni za abiria kupita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji, ukarabati wa kulirejesha katika hali ya kutumika utachukua takriban wiki moja na hivyo kuanzia jana saa 12 jioni eneo la reli kati ya Dar es Salaam na kilomita 82/5 Ruvu limesitishwa kwa huduma za usafiri wa reli.

Kwa taarifa hii wananchi na wateja wa TRL na wananchi kwa jumla ambao walikuwa wasafiri kwenda bara kwa treni ya jana ya Juni 10, 2014 wanatakiwa kufika katika stesheni zilizokaribu nao ili warejeshewe nauli zao ili watafute usafiri mbadala. Wakati taarifa hii inatolewa katika vyombo vya habari zoezi la kuwarejeshea nauli abiria wapatao 1000 lilikuwa zinaendelea katika stesheni mbali mbali za TRL na hasa katika Stesheni kubwa ya Dar es Salaam ambapo safari kwenda bara huanzia.
Aidha Uongozi wa TRL umeomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.

No comments:

Post a Comment