Pages

Pages

Monday, June 23, 2014

Mb Dog akamilisha mbili mpya bomba balaa


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa kizazi kipya, Mbwana Mohamed Mb Dog, amekamilisha nyimbo nyingine mbili mpya zinazojulikana kama Ya Moto na Demu Mwingine.


Msanii Mb Dog pichani.
Kukamilika kwa nyimbo hizo ni mwendelezo wa mikakati ya msanii huyo kufanya kazi nzuri ili kumuweka katika kiwango cha juu katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya.

Akizungumza leo mchanaa jijini Dar es Salaam, Mb Dog alisema kwamba nyimbo hizo amezirekodi katika Studio yake ya Macoppa, zilizopo jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa nyimbo hizo zinaungana na ile ‘Mbona Umenuna’ aliyoachia mapema mwezi uliopita na kupokewa kwa shangwe na wadau wa Bongo Fleva Tanzania.

“Hizi ni nyimbo mbili mpya na ambazo naamini zitapokewa kwa shangwe na wadau mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

“Naamini kila kitu kitakwenda vizuri kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa mazuri, ukizingatia kuwa mipango iliyopo mbele yangu ni kufanya kazi ya maana ili nionyeshe ukomavu wangu kisanaa,” alisema Mb Dog.

Mb Dog ni mmoja wa wasanii wanaotambulika kwa umahiri wao katika tasnia ya Bongo Fleva, huku akikumbukwa kwa nyimbo zake, ukiwamo ule wa Latifa na nyinginezo.

No comments:

Post a Comment