Pages

Pages

Tuesday, June 03, 2014

Cyprian Musiba amchanachana Yusuf Manji mchana kweupe, ataka wanachama wa Yanga wasimuongezee muda



Na Cyprian Musiba, Mwanachama Yanga
WANACHAMA wa Yanga walifanya mkutano mkuu maalumu wa klabu hiyo kujadili ajenda moja tu kupitisha Kamati ya Maadili kama ilivyoagizwa na FIFA kupitia TFF.
Cyprian Musiba, mwandishi wa makala haya.
Lakini cha ajabu ikaibuka ajenda nyingine kinyemela baada ya Kamati nzima ya Yanga kutishia kutogombea tena katika uchaguzi ujao. Kukawa na ajenda ya uongozi wa Yanga kuomba kuongezewa mwaka zaidi. Uongozi huo chini ya mwenyekiti Yusuf Manji unamaliza muda wake mwezi wa 7 mwaka huu kwa mujibu wa Katiba ya Yanga.
Ninachojua mimi kama Yanga wanataka kuahirisha uchaguzi huo, walipaswa kubadili kwanza Katiba halafu ndio wamwombe Manji aendee kuongoza. Nje ya hapo Manji atakuwa ameichezea Katiba ambayo ndiyo iliyomweka hapo. Vinginevyo anataka kuongoza Yanga kidikteta, kwa maana hiyo Manji hana mamlaka ya kujiongezea muda kwa matakwa yanga. Kwa maagizo ya TFF Yanga ilipaswa kujadili ajenda moja tu.

Manji akafanya usanii kama kawaida yake kuwahadaa baadhi ya wanachama ili wampigie magoti aendelee kuongoza  na kutangaza kumleta Marcio Maximo na mambo mengi ya usanii. Wanachama wa Yanga lazima wajitambue na wajue kwamba Yanga ndio maarufu siyo na nje ya Yanga Manji siyo Maarufu.

Yanga inaweza kujiendesha bila Manji kwa tayari inawadhamini lukuki wa kulipa mishahara na bado yapo makampuni makubwa na matajiri wakubwa wanaitamani Yanga kama Qugis, Reginald Mengi, Mustafa Sabodo na wengine wengi.

Manji asitumie udhaifu wa baadhi ya wanachama wa Yanga kutojitambua kugeuza Yanga kama mali yake. Yanga ni mali ya wananchi siyo mali binafsi ya Manji. Manji anapaswa kujua kwamba siyo wanachama wote hatujitambui, karibu asilimia 97 ya wanachama wa Yanga tunajitambua. Wanachama asilimia 3 waliozaliwa kabla ya kuzaliwa Tanzania ndio hawajitambui na kukubali hata kudanganywa kweupe wakati wa jua kali. Manji anafanya biashara zake na kubwa anaangalia maslahi yake kwanza.

Manji ni mjanja akitambua kuwa ameshamaliza kiakili wajumbe waliohudhuria aliwaletea mwanachama mzungu ili mawazo ya wanachama ambao alikwisha kuwatengeza na kuwaandaa yabaki wasifikiri zaidi ya hapo. Naomba viongozi wa TFF kuisaidia Yanga ili Manji asiifanye mali yake na uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa Julai mwaka huu.

Manji anafanya kazi ya kugombana na Azam ambaye amefanya mapinduzi makubwa ya soka la Tanzania. Manji ameshikilia media za Yanga na mkataba wake wa kushikilia media hizo umeisha, ameshindwa hata kujenga timu bora, Manji ameshindwa kuendeleza jengo la Mafia. Kuna wakati Manji alisema anaidai Yanga mabilioni na kushikilia akaunti ya klabu hiyo.

Sijui kama aliishajilipa fedha hiyo ama hajamaliza kujilipa ndio maana anaomba mwaka zaidi ili amalizie kujilipa deni lake. Nawaomba Yanga wote tunaojitambua kupigania Yanga ili huyu mjanja asijimilikishe. Manji kamwe hana la maana analoweza kufanya Yanga na amekuwa na mawazo ya kuifunga Simba tu mawazo mgando yasiyo na tija.

Mwisho naliona yanayoendelea Simba kwa vurugu zile zinakuja Yanga kwani Kamati ya Uchaguzi ya Yanga inaonekana wazi inafanya kazi zake kwa maelekezo na kwa maana hiyo haki ndani ya Yanga itakuwa historia.

TFF iokoeni na kuisaidia Yanga inakoelekea ni kubaya na vurugu kubwa zinaweza kutokea Yanga.                  

Imeandikwa na Cprian Majura Musiba.

No comments:

Post a Comment