Pages

Pages

Tuesday, June 03, 2014

Amigo, Hega, Diouf wapagawisha Kibaha



Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi nchini, Amigo Lasi, Rogath Hega ‘Caterpillar’, Msafiri Said ‘Diouf’, mwishoni mwa wiki walifanya shoo ya aina yake kwenye ukumbi wa Contena Pub uliopo Kibaha, Pwani, wakati wa shindano la urembo la Redd’s Miss Kibaha.

Wakali hao wa dansi, walitoa shoo ya nguvu wakiwa na bendi yao mpya ya Ruvu Stars inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) chini ya usimamizi wa Luten kanali Charles Mbuge ambapo mashabiki wa muziki na urembo waliokuwapo ukumbini hapo, waliifurahia mno.

Amigo ambaye ndiye kiongozi wa bendi hiyo, ametokea Twanga Pepeta pamoja na Diouf, Victor Mkambi, Jojoo Jumanne na wengineo, wakati Hega na Khadija Mnoga, wamejiunga na bendi hiyo mpya wakitokea Extra Bongo inayoongozwa na Ally Choki ‘Mzee wa Kizigo’.

Katika shoo hiyo, Diouf ndiye aliyekuwa kivutio zaidi kwa mashabiki kutokana na ‘rap’ zake za ukweli, huku Amigo na Hega wakipamba kwa sauti zao za ukweli na tungo ‘zilizokwenda shule’.

Nyimbo zilizokonga nyoyo za wakazi wa Kibaha na maeneo ya jirani siku hiyo, ni pamoja na Ester utunzi wa Seleman Muhumba ambaye ni mpiga solo, Spirit (Hega), Kioo (Amigo),  Network Love (Mhina Panduka), Fadhila kwa Wazazi (Hega) na nyinginezo.


Wasanii wengine waliopo katika bendi hiyo, ni Saleh Tumba, Kuziwa Kalala ambaye ni mpwa wake mkongwe wa dansi Hamza Kalala na wengineo, huku wanenguaji wakiwa ni wasanii ambao ni waajiriwa wa JKT.

Juu ya bendi yao hiyo, Amigo alisema: “Tumejipanga kufanya mambo makubwa katika dansi hapa nchini na tunamshukuru kiongozi wetu Luten Kanali Charles Mbuge pamoja na uongozi mzima wa JKT kwa sapoti wanayotupa.”  

No comments:

Post a Comment