Pages

Pages

Saturday, May 24, 2014

Dkt Bilal awaeleza wasomi Japan umuhimu wa vitega uchumi kwa maendeleo ya nchi za Afrika

Na Mwandishi Maalum, Tokyo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema nchi zinazoendelea hususan za Kiafrika bado zinahitaji uwekezaji zaidi vitega uchumi kutoka nje  (FDIs) ili kupata maendeleo ya haraka na  kuondokana na umaskini.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib  Bilal, akitoa muhadhara katika Chuo Kikuu cha Taaluma ya Sera 'GRIPS' wakati alipoalikwa kwenye muhadhara huo uliofanyika chuoni hapo Jijini Tokyo Japan, jana Mei 23, 2014. Picha na OMR.
Dkt. Bilal ameyasema hayo leo (Mei 23, 2014) wakati akitoa muhadhara kuhusu Mtazamo wa Nchi Zinazoendelea  na  Changamoto za Uwekezaji Vitega Uchumi  vya Nje na Hatma yake katika Kuondoa Umasikini kwa  kutumia  mfano wa Tanzania ulioandaliwa na  Taasisi ya Uchanganuzi wa  Sera (GRIPS)  mjini  Tokyo.
Alisema Afrika inahitaji misaada zaidi itakayosadia kukuza teknolojia itakayowawezesha Waafrika kuvuna  maliasili ambazo hazijavunwa. Aliongeza kuwa hii ndiyo njia pekee itakayoliwezesha Bara la Afrika kuongeza mapato na kuchangia maendeleo ya haraka kwa wananchi wake.
Alisisitiza  kuwa uwekezaji unaohitajika zaidi ni katika sekta za  za madini, mafuta na gesi, kilimo na vyanzo vingine vya nishati kama vile nishati ya jua na upepo. Alisema sekta hizo ndizo zinazohitaji teknolojia ya kisasa kutoka mataifa yaliyoendelea ili kurahisisha uvunaji wake.
Wakichangia hoja hiyo, wanafunzi wa chuo hicho walihoji namna Tanzania inavyojiandaa kuhakikisha upatikanaji wa mafuta na gesi hauwezi kuathiri amani na utulivu wa nchi yetu. Makamu wa Rais aliwaeleza kwamba utafutaji, uchimbaji na usambaji unafanyika katika misingi ya uwazi ili Serikali na  kila mwananchi aelewe ni kwa namna gani atakavyonufaika na rasimiali hiyo.

No comments:

Post a Comment