Pages

Pages

Friday, May 02, 2014

Bodi ya Mikopo elimu ya juu na mipango kawakomboa wanafunzi


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

JUHUDI za kukuza kiwango cha elimu kinachagizwa na vitu mbalimbali, bila kusahau taasisi zilizoundwa kwa ajili ya kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maendeleo ya Taifa.

Juhudi hizo zinakwenda sanjari na será zenye tija, ukizingatia kuwa ndio mfumo bora kwa sekta hiyo nyeti. Hapa Tanzania, miongoni mwa será na mikakati kabambe ni pamoja na ile ya uchangiaji wa elimu ya juu. Sera hiyo imekuwa ikitekelezwa nchini kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa (pichani), anasema kuwa será hiyo imezidi kushika kasi, ingawa ilikuwapo tangu wakati wa ukoloni na baada ya uhuru hasa baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974.

Anasema kuwa katika mfumo mpya ulioanza miaka ya 1990, mwanafunzi alitakiwa  kuchangia sehemu ya gharama za elimu tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo alikuwa akipata bure elimu ya juu. Kabla ya kuanza kwa mfumo wa uchangiaji, serikali ilikuwa ikitoa kila kitu kwa wanafunzi waliopata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.

“Hata hivyo, kuanzishwa kwa mfumo huo, kulitokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwezesha kuanzishwa kwa mfumo wa  wananchi kuchangia gharama mbalimbali badala ya serikali kugharimia  kila kitu katika elimu, afya na huduma nyingine.

“Awamu ya kwanza ya kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 1992, wanafunzi walianza kugharamia nauli za kwenda na kurudi kutoka chuoni, ada za maombi ya kujiunga na vyuo, ada za kuandikishwa chuoni na fedha za  tahadhari,” alisema.

Aidha, wanafunzi walilipia ada za serikali za wanafunzi vyuoni. Awamu ya pili ya uchangiaji katika elimu ya juu ilitekelezwa kuanzia Julai, 1994.  Pamoja na gharama zilizohamishiwa kwa wanafunzi na wazazi katika awamu ya kwanza, wanafunzi waligharamia mahitaji ya chakula na malazi.

Hata hivyo, gharama hizo zilionekana kuwa kubwa na serikali kuanzisha utaratibu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi kwa ajili ya gharama za chakula na malazi, huku utaratibu huo ukianzishwa rasmi awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin William Mkapa, mwaka 2005. Ndio hapo ilipoanzishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ambayo ilianza shughuli zake rasmi shughuli zake Julai, 2005.   

Katika awamu hiyo ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji, wanafunzi wanatakiwa kuchangia katika maeneo yote yaliyobaki ya gharama za elimu ya juu, yakiwemo ada za mafunzo, utafiti, mahitaji maalumu ya vitivo na mafunzo kwa vitendo.

Sheria iliyounda bodi ya mikopo, ilianisha majukumu ya bodi ambayo ni kusimamia uendeshaji wa mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuweka utaratibu wa kuwatambua wahitaji wa mikopo; kupokea, kuchambua maombi yote na kutoa mikopo kwa waombaji wahitaji, na Kuweka kumbukumbu za wanafunzi wanaokopeshwa.

Majukumu mengine ni kukusanya marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu  mwaka 1994; kuweka mtandao wa ushirikiano baina ya bodi, taasisi za elimu ya juu, waajiri na wakopaji; na kuishauri serikali kuhusu masuala ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo. Mkurugenzi huyo Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Mwaisobwa anasema tangu mwaka 2005, HESLB  imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Anasema katika miaka minane na nusu tangu kuanzishwa kwake, bodi imeimarisha utendaji kazi na kuweka mifumo na vitendea kazi ili kusimamia ongezeko kubwa la mikopo. “Hivi sasa bodi inatoa mikopo kwa kutumia mifumo ya kielectroniki (mtandao) katika uchambuzi wa mikopo, utoaji mikopo na urejeshwaji wa mikopo. “Vile vile waombaji wa mikopo yanatuma maombi yao kwa njia ya mtandao, tukiamini ni njia nzuri inayoweza kurahisisha utaratibu huo wa kutafuta nafasi ya kupatiwa mahitaji yao,” alisema.

Mwaisobwa anasema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi tangu mwaka 1994/1995 ambapo wakati huo kulikuwa na wanafunzi 6,061 waliojiunga na vyuo mbalimbali vya za elimu ya juu. Anasema kwa sasa wamefikia wanafunzi  233,000, huku wanafunzi 98,371 wakipata mikopo. Mkurugenzi huyo pia alisema mikopo itolewayo na Bodi imekuwa  sababu ya ongezeko la vyuo vya elimu ya juu kutoka 25 vilivyokuwepo mwaka 2004/2005 hadi vyuo 63 mwaka wa sasa wa masomo wa 2013/2014.

“Tangu wakati huo hadi Sedemba, mwaka jana, alisema mikopo yenye thamani ya sh. 1,843,483,926,686.58. Alisema katika mikopo hiyo, sh. 51,103,685,914 zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na sh. 1,792,380,240,772.58 zimetolewa na bodi yenyewe kuanzia Julai, 2005 na wanafunzi walionufaika ni 260,150.

“Pamoja na uchangiaji huo, dhana hii nigeni  katika historia ya Tanzania kwa kuwa mfumo huo ulikuwepo hata kabla ya uhuru. Mwaka 1956, serikali ya kikoloni ilianzisha mfuko uliojulikana kama Tanganyika Education Trust Fund, ambao ulitoa mikopo kwa wanafunzi kutoka familia masikini. Utaratibu huu uliendelea hata baada ya uhuru hadi mwaka 1964 lilipoanzishwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),” Alisema.

Anasema kuwa mwaka 1964 hadi 1974, wanafunzi walitumikia katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa miezi sita na baada ya hapo walihakikishiwa kupata kazi serikalini. Kwa kipindi cha miezi 18 walilipwa asilimia 40 ya mishahara yao na asilimia 60 iliyobaki ililipwa serikali, kama uchangiaji katika elimu ya juu kwa  mwanafunzi husika.

Kupitishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974, kulileta mabadiliko katika taratibu za ugharamiaji wa elimu wa juu. Muda wa kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa uliongezwa kutoka miezi sita hadi mwaka mmoja. Wanafunzi waliokuwa wakijiandaa kujiunga na elimu ya juu walitakiwa kufanya kazi angalau kwa miaka miwili kabla ya kuanza masomo yao.

Anasema kutokana na utaratibu huo, wanafunzi walitia saini mikataba ya miaka mitano na serikali ili kufanya kazi serikalini baada ya kumaliza masomo kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi sehemu zingine. Hiyo ilikuwa njia nyingine ya urejeshaji wa gharama za elimu ya juu. Kwa ujumla, mfumo wa uchangiaji elimu na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, umesaidia vijana wengi wa Kitanzania kupata fursa ya elimu katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kurejesha mikopo hiyo kwa kuwa baada ya kuhitimu, wengi wamekuwa wakishindwa kuheshimu makubaliano au kuwa wagumu katika ulipaji.
+255712053949
kambimbwana@yahoo.com
 

No comments:

Post a Comment