Pages

Pages

Sunday, March 09, 2014

TFF yatoa ufafanuzi jezi za Stars



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema jezi mpya zilizotumiwa na Taifa Stars kwenye mechi yake ya kirafiki dhidi ya Namibia, ni msaada wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambao wameingia mkataba na Kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, kusaidia nchi zisizojiweza kiuchumi.

Kwa mara ya kwanza Stars ilivaa jezi hizo katika mechi hiyo iliyochezwa jijini Windhoek, Namibia na kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, ikiwa ni mechi ya kirafiki iliyoko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema si ajabu kwa Stars kuwa na jezi mbili tofauti, huku akidai huo ni utaratibu wa kawaida tu.

Wambura alisema CAF wana utaratibu wa kusaidia vifaa vya michezo kwa nchi wanachama wake, hivyo jezi walizovaa Stars nchini humo ni mfano wa zile zitakazotolewa na CAF.

“CAF wameingia mkataba na Kampuni ya Adidas kusaidia jezi nchi zisizokuwa na uchumi mzuri, hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoingizwa kwenye utaratibu huo.

“Stars ilianza kuzitumia jezi hizo katika mechi dhidi ya Namibia, hivyo wadau wa michezo wafahamu hilo na zitakuwa zikitumika pamoja na zile za zamani,” alisema.

Stars ilirejea juzi saa 1 jioni ikitokea nchini humo, ilikokwenda kucheza mechi hiyo, kama nchi nyingine zilivyoumana katika mechi zao.

No comments:

Post a Comment