Pages

Pages

Thursday, March 27, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Wimbo wa uwanja Simba, Yanga hauna kiitikio

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WIMBO wowote usiokuwa na kiitikio huwa haueleweki. Hata uwe mzuri vipi, maana yake na uhondo wake hutoweka.


Ndivyo ninavyoweza kusema kila ninaposikia wimbo wa ujenzi wa Uwanja kwa timu za Simba na Yanga. Kwa bahati mbaya, wimbo huu ni mzuri lakini namna unavyoimbwa na ukosefu wake wa kiitikio ni tatizo kubwa kwa wadau wote.


Hapa siwezi kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwa kuona wimbo huu unazidi kuimbwa bila kuwa na kiitikio. Kwanini nasema hivi? Klabu ya Yanga imeanzishwa mwaka 1935. Mwaka mmoja baadaye ikaanzishwa Simba, yani mwaka 1936.


Ni miaka mingi sana. Lakini tangu wakati huo, wamekuwa na wimbo wao wa ujenzi wa uwanja. Kila siku wimbo huu unaimbwa na hayaonekani matunda yake.


Hii ni aibu kubwa. Azam iliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni, sasa inamiliki uwanja wa kisasa maeneo ya Chamaz, jijini Dar es Salaam.


Lakini hawa wanaojiita wakongwe bado wanaendelea kupiga porojo zao kila uchwao. Ona, Simba wao wameanzisha kampeni za ujenzi wa uwanja maeneo ya Bunju. Lakini njia wanazopitia hadi kukamilisha unagundua zina ukakasi.


Yanga nao kama walivyokuwa watani wao wa jadi, nao wanataka kuandamana kwasababu hawajajibiwa maombi ya kuongezewa eneo lao Jangwani.


Kwa rasilimali fedha na rasilimali watu za Simba na Yanga wanaweza kuhamisha mtaa eneo lolote la jiji na kufanya wanavyotaka wao.


Ila wanashindwa kwasababu watu wanaowaongoza hawana nia ya dhati ya kuwakomboa. Yanga wakiwa na mwenyekiti wao Yusuph Manji wana uwezo wa kufanya jeuri ya pesa, ila mfanyabiasharaa huyo anaangalia faida yake itakuwaje? Pia anaogopa kwasababu anajua timu hizi zinaendeshwa vibaya.


Simba nayo kila siku wimbo ni uwanja, uwanja. Mwenyekiti wao Ismail Aden Rage, ameufufua tena kwa kuweka mkaka wa siku 100. Hizi ni siku chache katika ujenzi wa Uwanja.


Na sijui kama kuna kinachoweza kuendelea juu ya mpango huo zaidi ya hadithi ya sungura na fisi. Nadhani tumeshindwa kufahamu mapungufu yetu. Watu wote hatujui kuwa wimbo wetu wa uwanja kwa klabu za Simba na Yanga hauna kiitikio.


Na hapa hakika siwezi kuvumilia, hivyo kuna kila sababu ya kujipanga upya.


Tuonane wiki ijayo.


+255712053949

No comments:

Post a Comment