Pages

Pages

Saturday, March 01, 2014

Mwambao Bonanza hapatoshi Mikocheni Jumapili



Na Henry Paul, Dar es Salaam
Mwambao Soccer Bonanza ambalo hufanyika kila baada ya miezi miwili litafanyika Jumapili katika Uwanja wa Mikocheni A. Shuleni kuanzia saa mbili asubuhi na linategemewa kumalizika saa kumi na mbili jioni.

Akizungumza Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Lusozi Faza, alisema kuwa Bonanza hilo kama ilivyo kawaida litashirikisha timu saba ambazo ni Boko National Veteran, Wazee wa Kazi Veteran, Bagamoyo Veteran, Kunduchi Beach Veteran, Mwenge Benz Veteran, Mbezi Beach Veteran na wenyeji Mikocheni Veteran.

Mwenyekiti Faza alizungumzia Bonanza hilo na kusema kuwa ni mwisho katika mzunguko wa pili baada ya kuanzishwa  katika  mzunguko wa kwanza Mei 13, 2012.

Bonanza hilo ambalo linahusisha timu hizo za Ukanda wa Mwambao limekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa maeneo hayo huku likitoa burudani tosha na kuwakumbusha wapenzi wa soka baadhi ya wachezaji mahiri waliotamba enzi hizo ambao hivi sasa wamesahulika.

Wachezaji hao ni kama vile Said Mrisho ‘Zicco wa Kilosa’, Issack Mwakatika waliochezea klabu ya Yanga na Athanas Michael aliyetamba akiwa na timu za Malindi, Pilsner, RTC Kagera, Tanzania Stars, Lusozi Father aliyechezea Pan African, Toto African ya Mwanza, Athumani Jumapili ‘Chama’ aliyechezea klabu ya Simba na wengine wengi.

Akimalizia Mwenyekiti Lusozi aliwataka wapenzi wote wa soka wa kuanzia Mikocheni, Mwenge, Mbezi Beach, Tegeta, Boko, Bunju na Bagamoyo kuhudhuria kwa wingi na kuja kuona Bonanza hilo ambalo linakutanisha wachezaji mahiri wa zamani waliotamba wakiwa na timu za ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (sasa ligi kuu).

No comments:

Post a Comment