Pages

Pages

Sunday, February 16, 2014

Yuko wapi mwimbaji wa 'Niite Basi', Joslin? Unakumbukwa na mashabiki wako popote ulipojificha

Joslin pichani.
WAPENZI wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, hawatashindwa kuufahamu wimbo wa 'Niite Basi'. Wimbo huu uliimbwa kwa ustadi mkubwa na msanii Joslin aliyekuwa ndani ya kundi la Wakali Kwanza.
Mr Blue pichani.
Kwa wadau haswa, jina hili ni tishio kwao maana linawagusa moja kwa moja juu ya kibao hiki. Ilikuwa balaa. Baada ya kutoka na wimbo huo, msanii huyu alitingisha katika vituo vya redio na televisheni.

Kila shoo alikuwa hakosi. Wengi wanapenda jinsi alivyoimba kwa hisia na mipangilio ya aina yake. Kwa mfano, katika mashairi yake kuna mahali anagusa zaidi anaposema; Unaponiita mpenzi Joslin napata wazimu, isitoshe baby pale unaponichumu, mwili unasisimka then napoteza fahamu babyyyyy, nitafanya nini? Haya ni baadhi ya mashairi makali sana.

Katika historia ya mapenzi kila mtu anajua namna gani anajisikia faraja kuwa na anayempenda kwa dhati. Fikiria mtu anakuita mpenzi au anakuchumu kabisa. Duhhh ni shidaaa.

Pamoja na mazuri haya, lakini msanii huyu alianguka kabisa. Hata pale alipotoa wimbo wake uliokwenda kwa jina la Itika haujaweza kumrudisha kileleni tena. Ule msuguano wake na nyota Mr Blue ukatoweka maana alishindwa tena kukaa kileleni hivyo kutajwa tajwa.

Kwa wasiofahamu, Joslin alijikuta akiimba wimbo mmoja na hasimu wake wa wakati huo, Mr Blue, wimbo wa Dully Sykes, uliojulikana kama 'Dhahabu'. Vijana hawa walifunikana balaa. Inadaiwa kuwa hakuna aliyejua kuwa anaimba wimbo mmoja na mwenzake.

Kila mmoja aliingiza sauti kwa wakati wake. Baadaye ukawa wimbo matata sana katika anga ya muziki wa BONGO FLEVA. Je, nani anajua msanii huyu anafanya nini kwa sasa?

Amepotea kabisa. Blog yako ya Handeni imemkumbuka kijana na inajaribu kuelezea namna alivyoweza kuimba kwa ustadi wa aina yake. Hapana shaka baada ya kuandika haya kijana huyu ataibuka na kuelezea wapi yupo, anafanya nini na kwanini ameanguka?

Alikuwa msanii mkali sana. Ana kipaji cha aina yake.
Huyu ndio msanii anayekumbukwa kwa leo.
Wiki ijayo tutaendelea na kumkumbuka nyota mwingine wa sanaa na kuelezea kazi zake ambapo hata hivyo alionekana kutoweka.

Unamkumbuka msanii gani, wakati huo wewe unafanya nini?

Tutajie au muelezee kisha tutumie kwa email yetu kambimbwana@yahoo.com au +255712053949


No comments:

Post a Comment