Pages

Pages

Tuesday, February 18, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Nani mkweli, sakata la Okwi?


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

SI lengo langu kuchokoza moto uliozima, baada ya kudaiwa kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), limebariki mshambuliaji kutoka Uganda, Emmanuel Okwi kukipiga katika timu ya Yanga, ikiwa ni uamuzi uliochukuliwa baada ya kuombwa na Shirikisho  la Soka nchini (TFF), kutokana na mkanganyiko uliobuka.
Emmanuel Okwi, mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga.
Hii ni kwasababu ninaamini kuwa ili mchezaji afikie malengo yake lazima avae jezi na kushiriki katika mechi za ndani na nje ya nchi, hasa kama timu yake inashiriki kimataifa.


Kwa mchezaji mwenye malengo, ni lazima atake kucheza Yanga na Azam FC maana kwa mwaka huu ndio zinazoshiriki michuano mikubwa Afrika, ukiacha mechi za ligi ya nyumbani.


Tangu asajiliwe na Yanga katika usajili wa dirisha dogo, Okwi aliingia kwenye mzozo baada ya usajili wake kuzuiwa kwa madai kuwa ulikuwa na utata.


Ni kweli ulikuwa na utata. Na hata sasa utata huo bado ni utata maana unaumiza kwa zamu. Katika kuliangalia jambo hilo, ni wazi Dunia ya leo si ya ubabaishaji.


Klabu za Yanga, Simba na nyinginezo zinapaswa kusajili kwa kufuata taratibu zote. Hali kazalka kwa wasimamizi wa soka, likiwamo Shirikisho la Soka nchini (TFF), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na wadau wengine lazima wasimame imara.

Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia. Ingawa napenda Okwi aiwakilishe Yanga katika ligi ya Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, ila ubabaishaji huu hauna tija.


Kuruhusiwa kucheza kwa Okwi ndani ya Yanga ni jambo zuri mno kwa wadau wa timu hiyo. Lakini pia iwe sababu ya kuhoji nani mkweli kwenye sakata hili. Etoile Du Sahel waliyompata Okwi kwa klabu ya Simba, Yanga iliyomnunua au SC Villa ya Uganda, ambazo zote zinalilia haki ya mchezaji huyo.


Kuna siku kutatolewa uamuzi mgumu utakaosababisha hasara kwa timu na Taifa kwa ujumla. Miongoni mwa hasara hizo ni kupokwa ushindi uliopatikana kwa tabu uwanjani.


Kwa bahati mbaya FIFA wamekuwa makini sana katika kusimamia kanuni na taratibu zao zinazoendesha soka. Inapotokea uzembe na ubabaishaji ni rahisi kuchukua hatua.


Hili likichukuliwa kwa timu za Tanzania, ikiwamo Yanga au Simba, malalamiko yake hayataelezeka. Huu ndio ukweli, hivyo wakati huu mashabiki wa Yanga wanafurahia Okwi kukipiga Yanga, ni wakati wa kujiuliza nani mkweli?


Tukishajua mkweli ni nani, tusimamie vyema sheria ili kesho zikichukuliwa juu yetu isiwe na madhara. Tusilalamike, ukizingatia kuwa sisi ni mabingwa wa kulalama kuhujumiwa.


Kinyume cha hapo matukio mfano wa Okwi yataendelea kutokea na kuibua mzozo usiokuwa na kichwa wala miguu, maana tumeamua kuwa watu wa kubabaisha.

Tukutane tena wiki ijayo.


+255 712053949

No comments:

Post a Comment