Pages

Pages

Wednesday, February 19, 2014

Tunasubiria matokeo ya mkutano wa wadau wa masumbwi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

HIVI karibuni wadau wa mchezo wa masumbwi walifanya mkutano wa kujadili tasnia hiyo inayokabiriwa na changamoto nyingi, hasa kwa kuona kampuni zinavyouchunia mchezo huo.


Ingawa wamekalia pesa lukuki, lakini wadau hao wameendelea kuziba macho na masikio yao, hata pale tunapoona malalamiko ya wadau wa ngumi na mabondia kuwa wanakosa udhamini.

Bondia Francis Cheka, pichani.
Changamoto hizo ndio sababu inayoufanya mchezo huo ushindwe kupiga hatua kubwa, jambo lililowafanya wadau hao wakutane katika mkutano wao uliofanyika katika Ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.


Waswahili wanasema kupanga ni kuchagua. Kwakuwa wadau hao wameamua kupanga jinsi ya kukabiriana na changamoto hizo, basi ni jambo jema kwao.


Hata hivyo, wadau hao wanakutana kwenye kikao chao wakati wao wenyewe wakati mwingine hawapo makini. Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na kadhia kubwa.


Ni pale promota wa mchezo wa masumbwi, Jay Msangi alivyoutia aibu kwa kuandaa pambano la Kimataifa kati ya Francis Cheka na Mmarekani, Phil Williams.


Ingawa pambano hili la Ubingwa wa Dunia lilimalizika kwa Cheka kushinda na kulitangaza Taifa, ila kasumba ni pale promota alivyoshindwa kujipanga katika suala zima la malipo.

Awali mpambano huo ulitaka kushindwa kufanyika, hivyo serikali kuingilia kati kunusuru zogo hilo, ambalo hadi mwisho ingekuwa aibu kwa Tanzania nzima.


Si nia yangu kukumbushia kilichotokea mwezi Agosti mwaka jana, ila ni namna gani wadau wa ngumi wote wanapaswa kufanyia kazi majibu ya mkutano wao.


Huu ndio ukweli. Wadau hao wakiamua kufanyia kazi yale waliyoamua wenyewe kwa ajili ya kunusuru tasnia hii itakuwa ni jambo la busara kwao na manufaa ya mchezo wa ngumi.


Huu ni wakati wa kufanya jitihada za kuukomboa mchezo wa masumbwi. Kila mtu mwenye malengo na mchezo wa masumbwi anapaswa kuamua kwa dhati kufanya kila analojua kwa ajili ya maendeleo ya ngumi.


Mapromota mfano wa Msangi nao wanapaswa kubadilika na kuamua kufanya juhudi kujijengea heshima ili walau waaminike katika kuandaa mapambano makubwa zaidi.


Kinyume cha hapo kasumba hii itaendelea. Mchezo wa masumbwi utazidi kudidimia. Wadau wakubwa wote watakimbilia katika michezo mingine, hasa mpira wa miguu.


Matokeo yake ni kuona ngumi inapoteza thamani yake, ingawa kuna vijana wengi wanaoweza kucheza masumbwi kwa ajili ya maisha yao na Tanzania kwa ujumla.


Mabondia wote wenye kiu ya kucheza ngumi watapoteza thamani yao, maana hakuna juhudi za dhati za kuleta ushindani, ukizingatia kuwa juhudi zao ni sifuri.


Hili linapaswa kuangaliwa upya, hasa kwa kuona mkutano wa wadau wa ngumi umekuwa na tija kwa mchezo huo Tanzania, ili kuleta picha na juhudi halisi za kuendeleza ngumi na kuona vijana wengi wanaibuka kwa kasi kushiriki kwenye masumbwi.


+255 712053949

No comments:

Post a Comment