Pages

Pages

Friday, February 21, 2014

Salamu za TAWODE katika mafunzo ya Utawala bora jijini Tanga

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Naibu Waziri , Ofisi ya Makamu wa Raisi, Mazingira,  Ummy Ally Mwalimu, Wakuu wa Wilaya, Waheshimiwa Madiwani wanawake  kutoka Halmashauri Mbalimbali, Watendaji wa serikali, Ndugu wawezeshaji, Waandishi wa Habari na Ndugu washiriki,  namshukuru mungu kwa kutuamsha na kukutana pamoja siku ya leo.

Habari za asubuhi na karibuni sana katika Mafunzo ya Uongozi na Utawala Bora (kwa ajili ya Maendeleo ya Wanawake na watoto) kwa waheshimiwa madiwani wanawake kutoka Wilaya nane za Mkoa wa Tanga ambazo ni Mkinga, Muheza, Korogwe,  Lushoto, Handeni, Kilindi, Pangani na Tanga.

Tunawashukuru sana kwa kuitika wito wetu na kuja  kushiriki katika mafunzo haya. Pia tunawashukuru watendaji wa Halmashauri waliofanikisha upatikanaji wa washiriki wetu kwa kutambua umuhimu wa mafunzo haya kwa maendeleo ya Wanawake na Taifa letu la Tanzania. Ni jambo jema kushirikiana pale kunapokua na jambo la kimaendeleo ambalo linahitaji ushiriki wa taaluma, uzoefu na mitizamo mbalimbali. Asanteni sana.  

Kwa namna ya pekee niwashukuru Viongozi wa Serikali na Madiwani  ambao wametoka Wilaya mbalimbali kuja kuhudhuria warsha  huu. Poleni kwa safari na niwatakie safari njema mtakapokua mnarudi.


Kama tunavyojua TAWODE  ni Taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na kikundi cha wanawake wa Mkoa wa Tanga ikiwa lengo ni kuchochea Hamasa ya maendeleo kwa wanawake wa Mkoa wa Tanga mwaka 2011. Na leo tunafurahi kuendelea na  utekelezaji wa shughuli za  Taasisi . 

 Lengo likiwa ni Kuboresha hali za  Kiuchumi na Kijamii za Wanawake na Watoto katika Mkoa wa Tanga na Kuchochea hamasa ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Haki za Watoto na Maendeleo ya Jamii ndani na nje ya Mkoa wa Tanga. Mafunzo haya yanajumuisha Washiriki 93 kutoka Wilaya za Mkinga, Pangani, Korogwe, Muheza, Lushoto,Handeni, Kilindi na Tanga. 

 Madhumuni ya mafunzo haya ya siku tatu ni Kuchochea ongezeko la mchango na ushiriki wa waheshimiwa Madiwani Wanawake katika kusimamia na kutetea maamuzi na Utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo katika Serikali za Mitaa hasa ihusuyo afya ya uzazi, Maji, Utawala Bora, Elimu kwa watoto wa Kike na Upatikanaji wa Mitaji kwa ajili ya shughuli za kuwaongezea wanawake kipato.  Mafunzo mtakayoanza leo ni muendelezo wa kazi zenu za utendaji wa kila siku. 

 Aidha napenda kusema kwamba Mafunzo mtakayopata katika semina hii yataenda sambamba na jitihada za Serikali katika kumwezesha kila mshiriki, sio tu katika maamuzi kwenye ngazi ya familia, bali hata katika ngazi mbalimbali katika jamii na taifa kwa ujumla, katika nyanja mbalimbali za maendeleo kama vile kuanzisha vikundi mbalimbali vya wasichana vya ujasirimali na vya kujadili masuala mbalimbali yanayogusa maendeleo yao ikiwemo kukataa maambuzi ya VVU/UKIMWI, kukataa mimba za mapema, ndoa za mapema na pia kuhimiza kujituma kufanya kazi, kuwahimiza kujitahidi katika masuala ya elimu.  

Hivyo basi tunawaomba washiriki wetu muwe huru  kutoa ushirikiano katika mafunzo haya. Tunaamini mafunzo haya yatawasaidia na kuwaongezea  nguvu ya kuleta mabadiliko katika jamii zetu. Tunatarajia mafunzo haya yatasaidia kuwapa moyo wanawake wengine kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi na kuleta mabadiliko katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Nawashukuru sana Viongozi na waheshimiwa  Madiwani wanawake kutoka Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Tanga. Mhe Mgeni Rasmi, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Raisi, Mazingira Ummy Mwalimu sasa nikuombe rasmi uje utufungulie mafunzo yetu.

No comments:

Post a Comment