Pages

Pages

Friday, February 21, 2014

Paulo Makonda apinga kudai nyongeza ya posho katika Bunge la Katiba

Paulo Makonda, pichani.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Paulo Makonda, ametoa ukimya kwa kuelezea kuwa hajatoa tamko lolote linalohusu kudai nyongeza ya posho kama inavyodaiwa na baadhi ya Watanzania juu ya sakata hilo.

Na haya ndio mandishi yake.

Huko nyuma niliwahi kutoa maelezo kuwa kazi tuliyopewa ni ya watanzania na inahitaji muafaka wa kitaifa ili tupate Katiba itakayokidhi mahitaji na matarajio ya watanzania,Katiba bora itakayojali haki na usawa kwa ustawi wa Taifa letu kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Kuna baadhi ya watu wameanza kujivika uwakala wa kuwa wasemaji wangu, tena kwa nia ya kutaka kuniondoa katika ajenda hii ya msingi kwa maslahi ya watanzania. 


Nimekuwa nikipigiwa simu na kupokea meseji kuhoji juu ya taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao kuwa ninadai ongezeko la POSHO. 


Naomba ieleweke kwamba sijazungumza na chombo chochote cha habari wala kuandika kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala la posho. Taarifa zilizosambazwa kuhusu mimi sio sahihi. Najitambua na natambua wajibu wangu kwa taifa na kwa watanzania wote katika mchakato huu. Natambua hali ya maisha ya watanzania na natambua matarajio yao kwetu, sijateuliwa kuwa mjumbe ili nipate maslahi binafsi ya kiuchumi bali kushiriki katika kuamua mustakabali wa Tanzania tunayotaka kuijenga. 

Hatuwezi kuwa na azma ya kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho, huku tukiendelea kudai maslahi makubwa zaidi kwa WABUNGE na wawakilishi na kusahau maslahi ya wanyonge walio wengi.
Nawaomba vijana wenzangu na wale wote wanaosambaza taarifa hizo, badala ya kutumia muda mwingi kuandaa majungu na fitina, tumieni muda vizuri kutushauri mambo ambayo sote kwa pamoja tunadhani yatasaidia kuliendeleza Taifa letu kiuchumi, kisiasa na kijamii.

No comments:

Post a Comment