Pages

Pages

Saturday, February 15, 2014

Pitia tamko la Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla juu ya mchakato wa Katiba Mpya



TAMKO LANGU KWA UMMA KUHUSU MCHAKATO WA KUANDIKA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Ndugu wanahabari na waTanzania wenzangu,
Nimekuwa nikilazimika kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa wanahabari, ndugu, jamaa na marafiki kuhusiana na namna mchakato wa kuandika katiba mpya ya Taifa letu unavyoenda; wengi wakipenda kujua nini mtazamo wangu kuhusu mambo mengi, haswa hili la serikali mbili ama tatu kwenye muungano wetu. 
      Mbunge wa Nzega, Dkt Hamis Kigwangalla, pichani
Mara nyingi nimekuwa nikikwepa kusema msimamo wangu ni nini kwa sababu niliona ni vema nikajipa muda wa kutafakari kabla ya kuamua kujenga msimamo yangu.
Ila kwa kuwa wakati wa kwenda Bungeni umefika na mimi nimepata bahati ya kuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge hili la kihistoria nimeona leo nitoe mtazamo wangu.

Kwanza, nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu kama tutaweza kufika salama huko tuendako. Si kwa sababu za kitabiri kama mnajimu, la, ni kwa sababu za kisayansi, ambazo nitaziweka wazi hapa kama ifuatavyo:

(i.) Pamoja na kwamba tume imefanya kazi nzuri ya kukusanya maoni na kuyaweka katika nyaraka ambayo tutapaswa kuifanyia kazi, napata shida kama walikuwa makini katika kuendesha zoezi hili.

Kivipi, binafsi napata shida na methodology iliyowawezesha kufikia ‘conclusion’ madhubuti kwamba watanzania asilimia 61 walitaka serikali tatu. 

Kwa sababu za kisayansi naona tume ya Mhe. Jaji Warioba imepotoka na kwamba kusema hivyo ni kutaka kulazimisha uhalali wa hoja hii nyeti kwenye dokumenti ya Rasimu ya Katiba tunayopaswa kuipitisha bila kuwa na msingi wa kitakwimu unaotokana na njia (methodology) za kisayansi za kukusanya ‘data’ na kutafuta ‘validity’ na ‘generalizability’ ya taarifa husika.
(ii.) Kwa jinsi mchakato ulivyo ni ngumu kusema kuwa leo tutaweza kubadili jambo nyeti kama la ‘Muundo wa Muungano’ kuwa uwe ni wa Serikali mbili, ama moja, wakati mapendekezo ya Tume, ambayo ‘yanaelezewa’ na Tume kuwa yanatokana na ‘maoni’ ya wananchi walio wengi, 61% na pili mabaraza ya katiba [cf. 

Muundo katika mchakato huu ni wa pyramid, kwamba unaanza na maoni ya wengi huku chini kwenye kitako, baadaye mabaraza ya katiba hapo katikati na mwisho Bunge la Katiba, kabla ya kura ya maoni]. 

Hivi inawezekana wapi Bunge Maalum la Katiba, kwa hapa tulipofikia, likafanya mabadiliko kwenye mambo yanayohusu ‘muundo’ (structure) wa Katiba? Yaani, kwamba inawezekana vipi wajumbe hawa 640 wabadilishe jambo zito la kimuundo kama hili? Kimantiki haingii akilini. 

Uhalali huo unatoka wapi? Lakini pia hapa hatuwezi kuondoa ukweli kwamba malalamiko na manung’uniko ya baadhi ya watu yana mashiko, kuwa hivi kama hoja ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa ni kuilinda ‘status quo’ ya muungano wa serikali mbili na kama walifanya kazi ya kuwaelimisha wana CCM nchini, na wanaCCM walikuwa wengi zaidi kwenye mabaraza ya katiba ya wilaya [walishinda kwa zaidi ya asilimia 65, inatokeaje asilimia 61 watake muungano wa serikali 3?]

Nini tafsiri ya haya yote? Kwamba ukisema unabadili leo muundo wa Muungano ukaleta wazo tofauti na lile linalotokana na mapendekezo ya tume, kama yanavyosomeka kwenye Rasimu (sura ya 6), mfano ukasema, ziwe serikali mbili tu badala ya tatu zinazopendekezwa, maana yake unaongelea kuanza upya kutengeneza vifungu vipya vya ‘kimuundo’ vya serikali za mitaa, wawakilishi wa wananchi, mambo ya wakuu wa mikoa ama majimbo(provinces) – jambo ambalo litakuwa cumbersome! Vurugu mechi bila uwepo wa rasimu! Swali la kujiuliza hapa ni kwamba – hivi tume hawakuliona hili? 

Pengine wangeweka chaguzi (option) pembeni, maana maoni yote haya wanayo, ila kwa sababu ya muundo wa Muungano ‘waliouchagua’ hawakupenda kuelezea mambo binafsi ya serikali hizi ‘mbili’ za ‘iliyokuwa Tanganyika’ na Zanzibar kwa madai kwamba jukumu lao ni kuandaa rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kinachoonekana hapa ni kwamba walikwishaamua kuwa ziwepo serikali tatu kwa madai kuwa ndiyo maoni ya wananchi na kwa kuzingatia msingi wa hoja kwamba Bunge la Katiba haliwezi kuwa na uhalali wa kubadili mambo ya msingi ya kimuundo wa katiba, kama hili la Muundo wa Muungano, bali ‘kuboresha’ tu yale yaliyomo. 

Mtu makini atahoji kuwa ni kwa nini wamekwepa kuzungumzia ukweli kwamba ‘Tanganyika’ hayupo? Na nini itakuwa hatma ya Katiba yake? Na ni lini wabia hawa wa Muungano walikaa wakakubaliana washirikiane kwenye mambo yapi kwenye huo muungano wa Shirikisho?

Sasa wabunge wa Bunge maalum la katiba tukiukataa huu muundo wa serikali tatu nini kitatokea? Maana yake sehemu kubwa ya rasimu hii italazimika kubadilishwa.

(iii.) Jambo lingine ambalo litatusumbua ni kuwa, vipi kama wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba tukiamua tujenge msimamo kwenye hoja ya Serikali Moja itakuwaje? Maswali mengi yataibuka bila kupata majibu hapa, kuwa ni nani atakuwa ‘Mpatanishi’ kwa niaba ya Tanganyika (ama Tanzania bara)? Maana Zanzibar yupo na ana uhai wake kamili, Tanganyika yuko wapi hapa?

Mhe. Jaji Joseph Warioba na wenzake wanapaswa wajibu maswali haya:

1. Ni njia (methodology) ipi ya kisayansi na kitakwimu walitumia kufikia ‘conclusion’ hiyo madhubuti kabisa kuwa 61% ya watanzania walitaka Muundo wa Serikali Tatu? Watueleze watanzania sample size, sampling technique, sampling frame na namna walivyowafikia na kuwahoji watu hao.

2. Watueleze ni nani aliyewatuma kwenda kubadilisha Muundo wa Muungano?

3. Ni nani sasa atakuwa na mamlaka ya kuandika Katiba ya Serikali ya Tanganyika (ama Tanzania Bara – ambaye aliishakufa?), kama tukiamua kwenye Bunge la Katiba kupitisha Rasimu hii yenye Muundo wa Muungano wa Serikali tatu? Tunaanzia wapi kumfufua Tanganyika?

Maoni yangu: Mtu yeyote mpenda demokrasia ataona wazi kwamba kuna utata uliogubikwa na ukungu wa presha za kisiasa za kuona zoezi hili linakamilika. 

Utata wa uhalali wa Bunge la Katiba kubadili hoja za msingi kwenye rasimu ni jambo zito, na mashaka kwamba pengine Jaji Joseph Warioba na wenzake walikuwa na ajenda yao ya siku nyingi ya kuleta serikali tatu kinyume na matakwa ya Chama Tawala, CCM, ni jambo zito zaidi. 

Hivyo, kuondoa mamlaka na madaraka ya wananchi (kama kweli yapo kama inavyosema tume) kwenye jambo zito la kimsingi kama Muundo wa Muungano ni jambo linalotishia usalama wa mchakato na ni jambo lisilokubalika kwa kuwa linaondoa haki, wajibu, mamlaka na madaraka ya wananchi kufanya maamuzi kuhusu katiba yao (an act of popular sovereignity). 

Mkanganyiko huu unatia mashaka zaidi ya kuleta mwangaza wa mabadiliko ya kutokea kwa maridhiano. Jaji Warioba na wenzake walilijua hili na wameleta ‘chaos na frustration’ kwa maksudi kwa kujificha chini ya kivuli cha ‘uhalali’ wa Bunge la katiba (yaani ‘legitimacy of rule or of law is based on the consent of the governed’) na nadharia pana ya demokrasia yenye msingi kwenye kanuni za ‘popular sovereignity’ wakijua kabisa wabunge tutashindana, tutatofautiana!

Mimi nina maoni kwamba, ili mchakato uishe salama, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete aingilie kati, atumie mamlaka yake kusitisha mchakato huu mpaka itakapoundwa tume nyingine ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la Muundo wa Muungano na kisha ipigwe kura maalum ya maoni kuhusiana na jambo hili ili watanzania washiriki kikamilifu na waamue na siyo kufanya maamuzi ya kubadilisha Muundo wa Muungano bila kutupa fursa ya kujadiliana na kushiriki kufanya uamuzi kuhusu jambo hili.
Ni jambo lisilo na busara hata kidogo kwenda kujadili Rasimu ya Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu Muundo wa Muungano wetu.

Kama kuna presha ya muda wetu wa miaka mitano kuisha kuna dirisha la kutokea; tusogeze mbele muda wa uhai wa Uongozi wa awamu hii ama turudi nyuma tufanye mabadiliko ya sehemu za katiba zinazohusiana na Tume ya Uchaguzi tu.

Hatuna namna ya kukwepa moja kati ya mambo haya kwa sababu hata tukifanikiwa kufunika kombe mwanaharamu apite, tukapitisha Katiba hii, bado tutahitaji kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria mbalimbali nay a kitaasisi kutokana na Katiba mpya itakayokuwa imepatikana, zoezi ambalo kwa kila namna litahitaji muda wa kutosha na sioni kama upo! Demokrasia ni gharama na haikwepeki!

Maswali ni mengi zaidi ya Majibu. Wasiwasi ni mwingi kuliko uhakika. Tutafika salama kwenye kupata Katiba hii kweli? Ni bora tukawie kuliko kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila kutazama tuendako, tutambae lakini macho njiani na mbele tunakoelekea.

Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega.

HK (Nimesaini)
Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB.

No comments:

Post a Comment