Pages

Pages

Wednesday, February 05, 2014

FIFA walikalia sakata la Okwi wa Yanga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), limeshindwa kutoa majibu sahihi ya suala la Mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga, Emmanuel Okwi, aliyezuiwa kukipiga katika klabu hiyo, licha ya usajili wake kufanyika kwa kufuata sheria zote za soka.

Mara baada ya kuingia kwenye mkanganyiko, Shirikisho la Soka nchini TFF, lililazimika kumsimamisha Okwi kuchezea Yanga hadi hapo suala lake litakapotolewa ufafanuzi na FIFA.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa bado hawajapata majibu ya mzozo dhidi ya Okwi kuchezea Yanga.

Alisema hali hiyo inawalazimisha kuendelea kulihangaikia jambo hilo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vizuri na kuleta tija kwa soka la Tanzania.

“Tangu tupeleke maombi ya kupatiwa ufafanuzi na wenzetu FIFA juu ya usajili wa Okwi kwa Yanga, akitokea Sports Club Villa ya Uganda, hakuna chochote kilichofanyika, jambo ambalo linachanganya namna suala hilo linavyoumiza kichwa.

“Tunaamini kuwa baada ya wenzetu hao kuliweka sawa jambo hilo, kila kitu kitakuwa sawa kwa ajili kuona linapatiwa ufumbuzi kama tulivyoomba kutoka FIFA,” alisema Wambura.

Utata ulianza pale klabu ya Simba walipolalamika kukosa fedha zao kutoka  Etoile Du Sahel ya nchini Tunisia, ambapo ilimpeleka Okwi kwa SC Villa ya Uganda ambayo nayo ilimuuza Yanga, hivyo suala hilo kuibua mkanganyiko na mvutano wa aina yake.

Kutokana na mkanganyiko, Okwi ameendelea kukalia benchi bila kupangwa hata mechi moja, huku timu yake ya Yanga ikiendelea na michezo ya Ligi ya Tanzania Bara, huku ikijiwinda na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Comorizeni, itakayopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment