Pages

Pages

Monday, January 06, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Nimeuchoka mgogoro wa Simba usiokwisha

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI mihemko gani isiyokuwa na likizo? Nani yupo nyuma ya wanachama hawa wa Simba? Nini hasa kiini cha mzozo huu? Haya ni baadhi ya maswali ninayojiuliza mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Ni pale ninapoangalia mgogoro unaoendelea kuwapo miaka nenda rudi kwa klabu ya Simba. Ndio, kuna uwezekano mkubwa mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage hayupo sahihi.
Na inawezekana pia anavunja Katiba hasa kwa kuangalia kuwa Makamu Mwenyekiti wake Godfrey Kaburu alijiuzulu na nafasi yake haijajazwa hadi wakati huu.
Katiba ya Simba inasema Makamu Mwenyekiti anapojiuzulu nafasi yake inatakiwa izibwe ndani ya siku 90. Tangu Kaburu ang’oke, ni zaidi ya siku 200 zimepita.
Haya ni mapungufu makubwa sanjari na ubabe aliokuwa nao Rage katika madaraka yake ndani ya Simba. Pamoja na hayo, Simba inatakiwa kufanya uchaguzi Mkuu Mei mwaka huu.
Hivyo inaonyesha kuwa Rage ana nafasi ndogo ya kuwapo katika nafasi hiyo, hasa kama kweli wanachama hao wamemchoka mwenyekiti wao huyo.
Kama hivyo ndivyo, sioni kwanini wanachama hao wasijipange ili wasubiri Uchaguzi Mkuu wao. Hii siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu chokochoko hizi hazina tija.
Hata kama Rage akiamua kutangaza kujiuzul leo, nani anaweza kushika nafasi yake kwa nyakati hizi za kuelekea uchaguzi? Binafsi naona huu ni mgogoro wa maslahi.
Kuna mtu au watu wapo nyuma ya wanachama hawa ambao kila mwaka wamekuwa wakijiweka mbele. Baadhi yao ndio walioshiriki kumsumbua Hassan Dalali wakati yupo madarakani.
Muda wake ukaisha na wanachama hawa hawa wakamchagua Rage awe mwenyekiti wao. Ndani ya mwaka mmoja, wakageuka na kumuona Rage si chochote.
Mgogoro huu ulikuwapo tangu mwaka 2011. Kila siku ni maneno na mvutano usiokuwa na maana yoyote. Ndio, naweza kuwa miongoni mwa wadau wa soka wanaotaka Rage ang’oke au akubali kuongoza kwa kufuata katiba yake, ila kwakuwa wakati wake umeshakwisha, sidhani kama kuna haja ya kupambana naye.
Waswahili wamesema kuku wako, manati ya nini? Hata afanye vipi, bado atatakiwa aitishe Mkutano Mkuu wa Simba utakaombatana na Uchaguzi Mkuu ndani ya mwaka huu.
Nafikiri Watanzania wote hususan mashabiki na wanachama wa Simba wangetulia ili mipango ya kiutendaji ifanywe kama ipo na baadaye watakutana katika uchaguzi wao.
Hapo watafanya uamuzi wowote watakaopenda. Kinyume cha hapo tutaendelea kubabaisha kwa kuingiza chokochoko zisizokuwa na maana na kuharibu soka letu.
Hakika siwezi kuvumilia, hivyo kuna haja sasa ya wanachama wote wa Simba kumuacha Rage na badala yake wajiandaye katika Uchaguzi wao utakaotishwa kwa mujibu wa Katiba yao.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949

No comments:

Post a Comment