Pages

Pages

Thursday, November 21, 2013

Jeshi la Polisi latoa onyo kali kwa wanaotumia vibaya silaha wanazomiliki kihalali

Advera-SensoAdvera Senso – SSP
JESHI la Polisi kwa kupitia Msemaji wao Advera Senso, limesema katika siku za hivi karibuni, imebainika kuwa, baadhi ya watu waliomilikishwa silaha kihalali wamekuwa wakitumia silaha hizo kinyume na malengo mazuri ya umilikishwaji. Baadhi yao wamekuwa wakitoa vitisho kwa wananchi kwa kutumia silaha hizo bila sababu za msingi wawapo katika maeneo mbalimbali, kama vile kwenye mabaa, kumbi za starehe na hata kulipizana visasi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na malengo ya umilikishwaji.


Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali kwa wote wenye tabia hiyo kuacha mara moja na badala yake wanatakiwa kuzingatia sheria na masharti waliyopewa wakati wa umilikishwaji.
Aidha, Jeshi la Polisi linaanza operesheni kali ya kuwabaini wote wanaofanya vitendo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya silaha hizo wale watakaobainika kwenda kinyume cha sheria na matumizi ya silaha zao.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wazalendo na wenye mapenzi mema na nchi yetu, kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini  watu hao wanaojihusisha na vitendo hivyo ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kupitia namba ya simu 0754785557, namba za simu za makamanda wa mikoa au kwenye kituo chochote cha Polisi.

No comments:

Post a Comment