Pages
▼
Pages
▼
Friday, October 11, 2013
Ummy Mwalimu: Serikali inatambua na kuthamini ushiriki wa wanawake katika shughuli za kimaendeleo
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya wasichana waelimishaji rika mkoa wa Tanga yaliyohusisha wasichana wapatao 150 kutoka wilaya za Muheza, Lushoto, Pangani, Mkinga na Tanga yenye lengo la kuwajengea uwezo na kuratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la maendeleo ya wanawake (TAWODE).
Na Oscar Assenga, Tanga.
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amesema serikali inatambua na kuthamini ushiriki wa wanawake katika shughulia mbalimbali za maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mwalimu alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya wasichana waelimishaji rika mkoa wa Tanga yaliyohusisha wasichana wapatao 150 kutoka wilaya za Muheza,Lushoto, Pangani,Mkinga na Tanga yenye lengo la kuwajengea uwezo na kuratibiwa na asasi ya kiraia ya (TAWODE) yenye makazi yake jijini Tanga.
Alisema hali hiyo inajidhihirisha katika malengo ya millennia,Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ikiwa ni mkakati wa pili wa kukuza uchumi na kuondoa umaskini (Mkukuta 11) na Sera ya Taifa ya wanawake na Jinsia ya mwaka 2000.
Naibu Waziri huyo alisema wizara yake inajukumu kubwa la kuwajengea uwezo wanawake na wanaume ili waweze kushiriki katika ngazi zote za utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kufaidika sawa kwenye maendeleo yao.
Aidha alisema jambo jengine ni kuhamasisha na kuwezesha jamii kuwapatia watoto haki ya kuishi,kuendelezwa, kulindwa,kutokubaguliwa na kushiriki katika maendeleo ya Taifa na hivyo itatoa miongozo ya kuzuia na kupinga aina zote za ukatili na ubaguzi wa kijinsia kwa
wanawake na watoto.
“Ni ukweli usiopingika kuwa ukimwendeleza mwanamke, umeendeleza Taifa zima na kuwekeza kwa mwanamke ni kuwekeza katika taifa endelevu “Alisema Mwalimu
Alitoa wito kwa wadau wote kuchukua hatua za kumuwezesha mtoto wa kike na kushughulikia mazingira hatarishi yanayomkabili katika kipindi cha ukuaji ili wasipate mimba za utotoni ikiwemo maambukizo ya virusi vya ukimwi na kukosa au kupunguza fursa zake mbalimbali za kujiendeleza.
Awali akuzungumza katika mafunzo hayo,Mkurugenzi Mtendaji wa TAWODE, Fatuma Hamza Mganga alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo wasichana wenye umri kati ya miaka 10 mpaka 24 na kuchochea uwezo na ubora wa kutambua ueledi na umuhimu wao katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla.
Mganga alisema pia semina hiyo ilikuwa na madhumuni ya kuwawezesha katika kujiamini,kujitambua na kuthubuti.
No comments:
Post a Comment