Pages

Pages

Thursday, October 24, 2013

Timu ya Taifa ya wanawake Msumbiji kuwasili Oktoba 25, Uchaguzi Bodi ya Ligi kufanyika kesho

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inawasili nchini kesho (Ijumaa, Oktoba 25 mwaka huu) saa 8.30 mchana tayari kwa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania itakayofanyika Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu).

Msemaji wa TFF, Boniface Wambura.
Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Msumbiji itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya LAM ikiwa na msafara wa watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Sapphire iliyopo maeneo ya Gerezani, Dar es Salaam.


Mara baada ya kuwasili JNIA, kocha na nahodha wa timu hiyo watazungumza na waandishi wa habari juu ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.


Kwa upande wa U20 chini ya Kocha Rogasian Kaijage imejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, na kesho saa 10 jioni itafanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Viingilio kwa mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.


Kamishna wa mechi hiyo Evelyn Awuor kutoka Kenya tayari amewasili nchini wakati waamuzi kutoka Burundi wanatarajia kuwasili leo saa 1 usiku kwa ndege ya Kenya Airways wakiunganishia safari yao Nairobi, Kenya. Maofisa wote wa mechi hiyo wanafikia hoteli ya New Africa.


Katika hatua nyingine, Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) unafanyika kesho (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower kuanzia saa 3 asubuhi.


Mgeni rasmi katika mkutano huo wa Bodi ya TPL ambao unafanyika kwa mara ya kwanza atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga.


Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).


Viongozi wa klabu za FDL wamefikia hoteli ya Royal Valentino iliyoko Barabara ya Uhuru wakati wale wa VPL ambao pia watashiriki Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wamefikia hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo.


Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.



No comments:

Post a Comment