Pages

Pages

Thursday, October 24, 2013

Mdau alichambua shidano la Bongo Star Search, ahoji uhalali wake na faida kwa washiriki



Na Jonathan Tito, Dar es Salaam
KWA wadau wa muziki wa Bongo Fleva, watakuwa wameusikia vizuri wimbo mpya wa Elibariki Emanuel ‘Ney wa Mitego’ na kuutafakari kwa kina.
Madame Rita, Mkurugenzi wa Benchmark Production ambao ndio waratibu wa shindano la Bongo Star Search Tanzania.

Katika mashairi ya wimbo huo uitwao ‘Salamu Zao’, msanii huyo amezungumza mengi akitaka salamu zake zifikishwe kwa watu mbalimbali.


Ney alimtaka Diamond afikishe ujumbe wake kwa Zitto Kabwe, amwambie aachane na Bongo Fleva, aendelee na siasa, maana Kigoma Stars amewatelekeza.

Salamu nyingine ni kwa Madam Rita Paulsen, zikihusu ‘kufulia’ kwa washindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS).

Pia Ney alizungumza na Ridhiwani akimtaka amueleze baba yake, Rais Jakaya Kikwete kwamba masela hawamuelewi na Wamakonde wa Mtwara hawataki tena korosho, bali gesi na anaweza kuwaua kwa mkong’oto.

Mwandishi wa makala haya, Jonathan Tito. Ni mtazamo wake binafsi, si msimamo wa Mtandao huu wa Handeni Kwetu Blog.
Ney alikwenda mbali na kumtafuta rafiki wa Edward Lowasa ili amfikishie salamu kuwa anamtaka agombee urais 2015, akiahidi kumpigia kampeni.

Chakushangaza anataka salamu nyingine zifikishwe hadi kwa marehemu Steven Kanumba na Albert Mangwear, kwamba atakayetangulia kufa akawambie wasanii hao kuwa wakati wa misiba yao kuna watu waliiba fedha za rambirambi.

Naamini salamu zote zitakuwa zimefikishwa kwa wahusika, hata zile za Kanumba na Ngwear, huenda ikawa Mack 2B aliyefariki mwezi uliopita, akawa ameshazifikisha.

Jukumu la kumfikishia salamu Mkurugenzi Benchmark Production, Madam Ritha, mwandaaji na mratibu wa shindano la BSS, alipewa mshindi wa mwaka jana wa shindano hilo, Walter Chilambo.

Lakini, hakuna ubaya wengine tukajaribu kuzifikisha kwa Madam, tena kwa maandishi.
BSS, imekuwa ikifanyika kila mwaka washindi wakipewa fedha taslimu kila mwisho wa shindano.

Lakini Ney na wadau wengine wana wasiwasi kama kweli washindi hao wanapewa fedha kutokana na washindi hao kutokuwa na tofauti kimuziki au kimaisha pamoja fedha hizo.
Mshindi wa kwanza wa shindano hilo lililofanyika mwaka 2007, Jumanne Iddi, ninaweza kumuondoa kwenye mlonongo huu wa washindi ‘waliofulia’.

Yeye alikabidhiwa gari, lililodaiwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 10.
Mshindi wa mwaka 2008, Misoji Nkwabi, hakuna anayejua yuko wapi kwa sasa na hatujawahi kusikia hata wimbo wake mmoja ukifanya vizuri kwenye redio, wala hatuna taarifa kuwa aliwahi kualikwa kwenye onyesho lolote.

Paschal Casian, mshindi wa mwaka 2009 aliyepewa Shilingi milioni 30, pamoja na uwezo mkubwa wa kuimba, ameshindwa kutamba kabisa kwenye muziki.

Hilo linalompa hofu Ney na wadau wengine wa muziki. Iweje mwimbaji mzuri, ashinde BSS, apate mamilioni ya fedha, lakini asiwe na maisha mazuri na hata kwenye muziki asifanye vizuri?

Je wanaridhika na fedha wanazopata na kuamua kuachana na muziki au ni kitu gani kinatokea? Fedha wanazopewa zinatosha kujiendeleza kisanii, lakini wengi wao wanashindwa kutamba.

Baada ya Paschal, mwaka 2010 alishinda Mariam Mohamedi ‘Mariamu BSS’ akaondoka na Shilingi milioni 30, lakini hajang’ara kwenye fani na kuishia akihangaika kwenye bendi za taarabu.

Mariamu na Paschal wana maelezo ya kufanana, kila mmoja akidai kununua nyumba. Ni kweli?

Kama kweli Mariamu alinunua nyumba, kwanini aishi kwenye nyumba ya kupanga Mabibo, tena isiyo na hadhi ya mshindi wa BSS?

Huenda nyumba yake kapangisha, lakini kwanini anaonekana kuwa na maisha magumu. Kwa sasa anajipatia riziki kutoka bendi ya Five Star.

Kama kweli walipewa milioni 30, wangeweza kutayarisha albamu zao na fedha zilizobaki wangefanya biashara nyingine na maisha yao yangekuwa mazuri.

Kuna taarifa kuwa Paschal ametayarisha albamu ya muziki wa Injili, lakini hakuna hata wimbo mpya unaofanya vizuri katika redio za dini, huku Mariam hajarekodi wimbo hata mmoja wa taarabu!

Mwaka 2011 mshindi alikuwa Haji Ramadhani, ambaye Ney anasema yuko ‘kitaani’ amechoka.

Ingawa Haji hajachoka mtaani, lakini maisha yake hayatokani na fedha za ushindi kwani wakati wa fainali hiyo alitunzwa fedha nyingi sana.

Ndio maana amenunua gari ya kutembelea na anamudu kupata fedha ya kuweka mafuta kwa kuwa anafanya kazi Twanga Pepeta, ukichanganya na anacholipwa na kutunzwa na mashabiki wa bendi hiyo, maisha yake ni tofauti na washindi wengine wa BSS.

Walter, mshindi wa mwaka jana, hajafikisha hata mwaka, lakini kwa mujibu wa Ney, amepigika na hilo linaweza kuwa kweli kwani kila siku husema kwamba fedha zake ziko benki huku mama yake akiishi nyumba ya kupanga eneo la Forest ya zamani mjini Mbeya!

Walter ameonyesha uhai na nyimbo zake zinafanya vizuri na angekuwa na fedha za kutosha, angekuwa juu zaidi kimuziki kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuimba.

Kila baada ya shindano, washindi wamekuwa na porojo za hapa na pale, kila mmoja akijifanya kuelezea matumizi ya fedha alizopata, lakini baada ya muda unamuona anaendelea na maisha yale yale ya zamani.

Hapo ndipo Ney anauliza, hizo fedha zinakwenda kwa nani? Hii si hoja ya kupuuziwa! Inastahili majibu stahiki.

Isije ikawa kuna watu wanafaidika kwa kupitia shindano hilo na kuwatosa wasanii!
Madam Rita amekuwa akidai kuwaibua wasanii na sasa wamejiunga bendi mbalimbali, bila kujua kuwa walikuwapo huku hata kabla ya kwenda BSS.

Afike mahali aanze kuwasaidia hao washindi kufikia malengo yao kisanii.
Ikiwezekana basi, kabla ya kuwapa fedha wapewe kwenza elimu ya ujasiriamali au kama fedha haziwasaidii, ipo haja ya kubadili zawadi kwa washindi.

La sivyo, wadau wataendela kuwa na hofu kuwa kuna ‘magumashi’.
Wakati wasanii wakisota, hali kimaisha kwa ‘wakubwa’, Madam Rita, Master Jay na Salma Jabir ni tofauti kabisa, wao wanazidi kung’ara tu.

Master Jay, anaendelea kuajiri watu kwenye ofisi yake, huku mwenyewe akiendelea na ‘ofisi kubwa’, BSS.

Tulisikia Salma alienda kusoma Afrika Kusini, lakini msimu wa mwaka juzi wa BSS ulipokaribia, alirejea kuja kuwa jaji huku akizuga na kipindi chake cha runinga cha Mkasi ambacho hakijawahi kumuhoji hata mshindi mmoja wa BSS kuzungumzania mafanikio yake.

Master Jay naye hajamsaidia ‘kutoka’ hata mshiriki mmoja wa BSS kwenye studio yake walau kuonyesha kweli wamelenga kuinua vipaji wao na bosi wao.

Sawa, inawezekana wanaibua vipaji, lakini tujiulize, Diamond, Rich Mavoko, Ommy Dimpoz na wengine, wamepata majina na mafanikio wakitokea BSS?

Hizi ni salamu tu za Ney wa Mitego kwa Madam Rita, nimetumika kama njia rahisi ya mawasiliano na ninatarajia mshindi wa mwaka huu atajengewa misingi bora kimaisha na kimuziki.

No comments:

Post a Comment