Pages

Pages

Sunday, October 27, 2013

Papii Kocha na baba yake wataka Watanzania wawaombee

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI Papii Kocha, anayetumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela, amewataka Watanzania wamuombee ili aweze kutoka na kurudi katika maisha yake ya uraiani.

Papii aliyasema hayo jana alipotembelewa na wadau mbalimbali wa muziki wa dansi, wakiwamo wale wanaounda muungano wa kundi la Bongo Dansi, linalopatikana katika mtandao wa kijamii facebook.
Wanamuziki Papii kocha kushoto na baba yake Nguza Viking wakiwa na nyuso za huzuni katika picha za matukio yao ya kuhukumiwa kifungo cha Maisha Jela. Wanamuziki hao sasa wanamatumaini kidogo baada ya Mahakama ya Rufaa kukubali kupitia vifungu vya sheria iliyowatia hatiani.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, alisema dua ndio zinazoweza kumrudisha uraiani yeye na baba yake Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na makosa ya ubakaji.

Papii aliyasema hayo baada ya kupata maatumaini kutokana na Mahakama ya Rufaa kukubali kufanya marejeo (review) ya jinsi walivyotuhumiwa na kukutwa na makosa hayo kiasi cha kupewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

“Nawapenda sana Watanzania wote na wao ndio wanaoweza kunirejesha mtaani kwasababu ya dua zao, hivyo naomba mfikishe ombi langu kwao ili watuombee mimi na baba yangu.

“Naamini ipo siku naweza kukutana na watu wote huko, hata hivyo hili linaweza kutimia kwa mipango ya Mungu pamoja na dua za Watanzania wote,” alisema Papii Kocha.

Mwanamuziki huyo anakumbukwa kutokana na uwezo wa juu wa kuimba, huku akiitumikia kwa miaka kadhaaa bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.

Papii Kocha pia aliwahi kuimba kibao chake cha Salima, wimbo unaotoa watu machozi kila unapopigwa kutokana na kuandaliwa kwa kiwango cha juu na mwanamuziki huyo.

Aidha, aliwahi kuimba pamoja na baba yake katika kibao cha ‘Seya’, wimbo ulioimbwa kwa ushirikiano, huku wakitumia uzoefu wa hali ya juu kufikisha burudani na elimu kwa hadhira, kabla ya kuhukumiwa mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment