Pages

Pages

Tuesday, October 22, 2013

Mkuu wa Mkoa Tanga aagiza Halmashauri zote kujenga maabara tatu kwa kila shule

Na Oscar Assenga, Muheza.
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa ameziagiza Halmashauri zote mkoani hapa kuelekeza msukumo mkubwa kwenye ujenzi wa maabara tatu kila shule ili kuwawezesha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi na kuweza kufanya vizuri.
Gallawa ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea shule ya seminari ya wavulana ya Livingstone iliyopo wilayani hapa pamoja na kuzindua jengo la maabara ya kompyuta iliyojengwa kwa thamani y ash. 149,000,000 ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ndani.
Amesema ujenzi huo wa maabara kwa vyumba vitatu kila shule ni agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,Dokta Jakaya Mrisho Kikwete hivyo kuzitaka halmashauri hizo kutilia mkazo suala hilo kwenye maeneo yao.
Ameongeza kuwa maabara hizo zinapaswa kuwepo kwenye shule za sekondari kuanzia za kata na zile za binafsi kwani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila ya kuwepo wanasayansi.
Aidha amesema katika hilo inabidi itumike nguvu kubwa ikiwemo hata kuhairisha miradi mengine ili kuzielekeza kwenye ujenzi wa maabara kwenye shule hizo.

"Halmashauri zote zinatakiwa kujenga maabara tatu tatu kila shule na sio mbili kwani hilo ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete.
Amezitaka halmashauri kupitia ofisa elimu kupita kwenye shule za binafsi kuwasisitizia suala hilo la ujenzi wa maabara kwani ni muhimu sana hasa kwenye maendeleo ya nchi yetu.
Mkuu huyo wa mkoa ameziagiza pia shule za sekondari na msingi mkoani hapa kupanda zao la mkonge kwenye mipaka yao ili kuwezesha wanafunzi kufundishwa jinsi ya kupanda zao hilo.

No comments:

Post a Comment