Pages

Pages

Wednesday, October 09, 2013

MGODI UNAOTEMBEA:Tumkosoe Rais Kikwete, ila tusimdharau


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MCHAKATO wa kupatikana kwa Katiba Mpya unaendelea, huku kila mmoja akisema lake. Ni hatua nzuri kwa Tanzania. Kama tunavyojua, Katiba ndio kila kitu. Bila kuwa na Katiba Taifa letu haliwezi kusonga mbele. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, pichani.

Tanzania inaelekea kupatikana kwa Katiba Mpya, huku mtu pekee anayetakiwa apongezwe ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pichani.
Amekuwa mwepesi kusikiliza wananchi wanataka kitu gani kwa maslahi ya Taifa. Kwa mfano, suala la Katiba Mpya limeibuliwa kutokana na baadhi ya watu kuamini kuwa vyama vya upinzani vinashindwa kupiga hatua, ikiwamo kushika dola kwasababu ya kukosa Tume Huru ya Uchaguzi.
Tundu Lissu, pichani.
Kama hivyo ndivyo, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011 kwa ajili ya kuanza hatua ya kwanza hadi ya mwisho ya kupatikana kwa Katiba Mpya.  Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. 

Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo, ikiwa ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya Taasisi, huku mwelekeo wake ukitia moyo kwa kiasi kikubwa mno. 

Hapo kabla, wapinzani waliamini kila kinachofanyika kwa Tanzania, basi si kuneemesha vyama vyao. Hapo kukazuka la Katiba Mpya. Awali wapo waliopinga, wakisisitiza kuwa Katiba inayotumika na kupatikana mwaka 1977 inajitosheleza.

Mvutano ulikuwa mkubwa kiasi cha kuonyesha mpasuko miongoni mwa Watanzania, hasa wanaofuatilia siasa na kwenye vyama vya upinzani, kama vile Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vinginevyo.

Pamoja na yote hayo, rais Kikwete, huku akijua yeye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimaliza mgogoro huo kwa kukubali kuingia kwenye mchakato wa maoni ya Katiba Mpya.
Ndio hapo Tume ikaundwa chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Jaji Joseph Sinde Warioba, ikijumlisha watu mbalimbali wenye lengo jema. Mchakato huo ukaendelea na sasa imefikia kwenye rasimu ambapo inasubiriwa sahihi ya Rais Kikwete.

Pamoja na lengo jema la Kikwete kuhakikisha kuwa anaondoka madarakani akiwaachia Watanzania Katiba Mpya, bado kumekuwa na maneno ya kejeli dhidi yake.

Watu hao hasa wanaojiita wapinzani hata wa mambo mazuri yenye kuleta ushirikiano na maendeleo, wamesahau kuwa ni juhudi za serikali ya Kikwete, imeruhusu mchakato huo na sasa Tume hiyo inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. 

Hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa tunapata Katiba Mpya kama 
inavyohitajika, huku Bunge Maalum likitarajiwa kutoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni na ikionekana ipo sawa basi kiu ya Watanzania kuwa na Katiba Mpya itakuwa imepata ufumbuzi.

Ieleweke kuwa, mchakato huu wa Katiba Mpya umehusisha watu wengi mno, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa. Kumetokea mivutano kadhaa, lakini baadaye ilipatiwa ufumbuzi.

Kama hivyo ndivyo, ni vyema sasa vyama vya siasa vya upinzani vikathamini mchango wa Kikwete katika hili. Mara kwa mara ameshindwa kukubali msimamo hata wa waumini wa chama chake, yani CCM.

Hii ni kwasababu, ni mtu makini anayependa kufanikisha suala zima la Katiba, hivyo Watanzania wote lazima tufahamu jambo hili. Wapinzani wanasisitiza kuwa upande wa Zanzibar haukushirikishwa.

Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishirikishwa kwa kutoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili, likiwamo hili la uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar, pamoja na Bunge Maalum kuongezwa muda wa siku 90 endapo litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa.

Hivyo wanasiasa wanaposema haya lazima waelewe namna gani muundo wa mchakato huu ulishirikisha watu wengi kutokana na wote kuwa na dhamira ya kuwa na Katiba Mpya.

Endapo CCM walitaka kuigomea Katiba hiyo, basi wasingekubali hata huo mchakato wenyewe, maana pamoja na kelele zote zinazoweza kutokea, bado wao ndio wanaoongoza serikali.

Mvutano huo ulifika mbali zaidi pale baadhi yao waliposema kuwa Katiba Mpya ipo kwa maslahi ya CCM na sio Watanzania wote, jambo linalodhihirisha kuwa yote yanayosemwa yana lengo la kuichafua CCM na serikali yake dhidi ya Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Hii napinga. Hata huo muungano unaodaiwa umewekwa kwa vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi chini ya James Mbatia hauna jipya, kwasababu nao pia wanapigania ulaji wao.

Ni Muungano wa vyama vitatu vya upinzani hali ya kuwa kuna vyama vingi vyenye mlengo sawa na wao? Kwanini wao na sio wenzao? Kuna nini ndani ya msuguano huu?

Nani anaweza kunufaika kiongozi wa chama cha siasa cha upinzani au mlalahoi wa Handeni, mkoani Tanga? Yule mwananchi wa kawaida wa Mbeya, Musoma, Arumeru, Shinyanga anaweza kunufaika?

Tanzania ina vyama vingi vya upinzani. Chama sio CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema peke yao. Ndio maana naungalia Muungano huu kwa umakini mno.

Huwezi kutofautisha maslahi ya vyama vya upinzani katika Katiba hii, ndio maana kwa kulijua hilo nao walikuwa ‘busy’ kutembea katika mikoa mbalimbali kuwaelimisha watu wao.

Freeman Mbowe kama Mwenyekiti wa Chadema, anajua fika kuwa mikoa yote aliyotembelea kupiga kelele za Katiba Mpya, alikuwa akilenga maslahi ya chama chake na sio CCM.

Ndio maana nasema, hakuna haja ya kuendelea kupiga kelele, kumdhihaki Rais Kikwete na kusahau mazuri yake kiasi cha kuweka kila kitu wazi juu ya mwelekeo huu wa aina yake.

Kama kuna mapungufu ndani yake, basi yapo kiubinadamu. Yanazungumzika hata itakaposainiwa Rasimu hiyo. Baniani mbaya ila kiatu chake kizuri.

Hakuna haja ya kelele, matusi na kusimangana wakati ipo njia nzuri yenye kujenga jamii bora. Tanzania hii ni yetu wote. Tumezoea kuishi kwa kusikilizana na kusaidiana.

Ndio maana pamoja na nongwa zote, dhihaki isiyokwisha kwa serikali ya CCM, lakini bado ni rahisi kusikilizwa. Kwa mfano, mwana CCM yoyote anaweza kumshangaa Rais Kikwete kukubali kukutana na wapinzani mara kwa mara.

Kwa kuliangalia hili tu, asingetokea mtu anayejiona ni mpinzani kiasi cha kumtusi Rais kwa kumwita dhaifu na mengineyo. Najua si yote mazuri yanayofanywa na Rais Kikwete.

Hii ni kwasababu yeye ni binadamu. Ana mazuri na mabaya yake. Ni vyema tukachukua na kuthamini mazuri yake ikiwamo utaratibu mzuri wa upatikanaji wa Katiba Mpya aliyouanza ndani ya uongozi wake.

Na yale mabaya yake tumuachie au kumkosoa kiungwana ili kujenga jamii bora, kuleta ushirikiano, ukizingatia kuwa huo udhaifu upo pia kwa wapinzani na ndio maana wamekuwa wakiishi kwa kujenga matukio ili waandikwe magazetini.

Nikisema haya, nitaitwa majina lukuki ya kuogofya. Wapo watakaoniita mimi nimeishiwa. Wapo pia watakaosema nimezaliwa familia ya mjumbe wa nyumba 10 na mengineyo lukuki.

Hata hivyo, siku zote ukweli unamuweka mtu huru. Bora niseme ninachokiamini ili kesho nisibaki kusononeka. Bila Rais Kikwete kukubali wazo la Katiba Mpya, ingechelewa kupatikana.

Na lazima wapinzani wasijione wao wapo sahihi kwa kila jambo. Na kuwa mpinzani sio upinge kila jambo. Kwa mfano, Muswada ulivyofikishwa Bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe zogo likaibuka.

Hii ni baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Gosbert Blandes, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati, huku akifuatiwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, ambapo mvutano hao ulifikia wapinzani kutoka nje.

Hapa tu, ni udhaifu wa aina yake. Wapinzani wanapoamua kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge kama kawaida yao, husababisha hoja za upande mmoja kupenya.

Imeshatokea hii mara kadhaa. Hata kwenye Bunge la Bajeti walifanya hivyo, huku baadaye wakitokea mlango mwingine na kuanza kulaumu kupitishwa kwa bajeti hiyo wakisema haina tija na Watanzania.

Sawa, ila kwanini wao walitoka nje? Je, wanasahau umuhimu wao kiasi cha kuchaguliwa na wapiga kura wao? Wapinzani wanaposusa, wanamsusia nani? Au wale waliowachagua?

Katika hotuba yake ya kila mwezi kwa Watanzania, Rais Kikwete anasema, “Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. 

Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao, baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana, ukizingatia kuwa haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo,” alisema Rais Kikwete, ikiwa ni siku chache baada ya muungano wa vyama hivyo vitatu vya upinzani kutangaza maandamano yasiyokuwa rafiki kwa Watanzania wote.

Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria ni sababu ya kuwasumbua Watanzania bila mpango. Ni vyema tukaelewa kuwa nchi hii ikiharibika tutasumbuka wote.

Tuilinde na kuitetea Tanzania na sio vyama vya siasa. Vyama vyetu vinaweza kufa wakati wowote, ila Tanzania itaendelea kubaki, hivyo tusijaribu kukata mti tuliokalia.

Huu ndio ukweli wa mambo. Ndio maana nasema, kama kweli tuna nia ya kujenga, basi tumkosoe Rais Kikwete, lakini tusimdharau maana amefanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya Taifa hili.

Kwangu mimi ni mtu wa kukumbukwa, maana katika kipindi cha uwapo wake madarakani, ameweza kuthubutu na kuwapatia watu kile walichokuwa wanakihitaji, Katiba Mpya.

Lissu asimdhihaki Kikwete. Anaposema hana msimamo na muda mwingi anasema nimeambiwa, nimearifiwa ni kuonyesha hana kauli yake yeye kama Rais wa Tanzania.

Inawezekana, ila angekuwa rais ni Dk Willbroad Slaa, angeweza kujichukulia uamuzi bila kushauriwa? Je, ni Rais gani duniani anayeweza kuyajua yote katika serikali yake?

Iko wapi haja sasa ya kuajiriwa wataalamu wanaoweza kumshauri Rais, ukizingatia kuwa mara kadhaa bado tumesikia wapinzani wakilaumu kuwa rais hana washauri.

Kuna haja sasa ya kuangalia nyendo zetu. Tulipotoka ni mbali mno kuliko tunapoelekea katika mchakato huo wa Katiba Mpya. Katiba ni mali ya Tanzania na sisi ni Watanzania.

Katiba sio mali ya CCM, CUF, Chadema, TLP na vinginevyo hivyo hakuna haja ya kupigia kelele kwa ajili ya maslahi ya vyama hivi, japo wapinzani wanajitoa katika hilo kwa kudai kunaandaliwa utaratibu wa kukibeba chama tawala.

Tuwaangalie kwa jicho makini mno hawa wanasiasa wanaotaka kuandamana leo bila sababu za mpango, wakati wanajua fika wabunge wanayo nafasi ya kupinga, ukizingatia kuwa wao wana nafasi ya kushiriki katika vikao vya Bunge. Bunge ambalo mchakato huo ulianzia hapo na hatua ya wao kutoka nje, kususa, ni ishara kuwa nao wanataka kuweka njia za kuvibeba vyama vyao vya siasa.

Mungu ibariki Tanzania.
kambimbwana@yahoo.com
+255712053949


No comments:

Post a Comment