Pages

Pages

Wednesday, October 02, 2013

Mbunge wa Kilwa Kaskazini akerwa na magari kufungwa minyororo jijini Dar es Salaam



Kadhia hii hapana
Moja kati ya sifa ya mwanadamu mwenye busara ni kukubali kujifunza kwa makosa aliyotenda na kuomba radhi aliowakosea.Mwalim Julius Nyerere aliwahi kuandika kwenye kitabu chake, Tujisahihishe, kuwa ni: ‘upumbavu mtu kuamini kuwa anajua kila kitu’’.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu.
Naandika kwa kuona kuwa hali mbaya inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam bila hatua stahiki kuchukuliwa. Pia kuwaomba wenzangu wanaokerwa, kuathirika na kuichukia tabia ya ufungaji magari ambayo yanapaki mitaani haswa katikati ya Jiji la Dar es salaam. 

Makundi ya mgambo na kampuni binafsi za ulinzi wamekuwa wanafunga magari kwa minyororo na kudai malipo kutoka kwa wamiliki wa magari husika kwa kusingizia kuwa umepaki ‘mahala pasiporuhusiwa’. Ajabu ni kwamba hakuna alama za katazo.
 
Jambo la kustaajabisha ni kuwa ramani ya mji wa Dar es salaam haijabadilika tangu kuchorwa na kubuniwa kwake na wajerumani miaka ya 1800+ na 1900 mwanzoni. 

Hii inamaanisha kuwa mitaa na barabara zake ilibuniwa kukidhi idadi ya wakazi (200,000) waliokuwa wanaishi kwa wakati ule ama kwa ongezeko dogo kulingana na ukuaji wa mji.
 
Kutokea miaka ya tisini (1990) kumekuwa na ongezeko kubwa la majengo makubwa ,mahoteli, maduka, kumbi za starehe pamoja na shughuli zingine. 
Wizara husika, Halmashauri ya Jiji na sasa Manispaa za Jiji zimekuwa zikitoa vibali vya majenzi kwa wamiliki wa majengo na kutoza tozo mbalimbali kutokana na majengo hayo.
 
 Wizara zote kasoro nne tu (Tamisemi, Maji, Kilimo na Mifugo) ndizo ambazo ziko nje ya mji lakini wizara nyinginezo, mabenki, mahakama kuu, ofisi mbali mbali ziko katikati ya mji; hivyo mahitaji ya huduma ni makubwa sana kwa wananchi.
 
La kustaajabisha zaidi kuwa wakati wanatoa vibali hivi hawakujua tunaalika wakazi wengi zaidi ambao watahitaji huduma za maegesho ya magari ili kuingia ndani ya majengo hayo au kufuata huduma mbalimbali ?
 
Halmashauri ziliamua kuanzisha utaratibu mzuri kwa kutoza gharama za maegesho na kukabidhi kampuni binafsi ambazo zinasimamia. 

Kampuni hizi zinauza vibali (permit) zenye ukomo wa mwaka na kufanya nafasi kuwa finyu zaidi. Imani yangu kuwa kampuni hizi zinakidhi matakwa ya kimkataba kama ilivyokubaliwa, ila yapo maswali yasiyo na majibu: kuwa pesa zinazotokana na tozo hizi zinatumika kufanya nini? 

Hawa wanaolipwa wanawajibikaje na usalama wa magari na vilivyomo ndani ya magari baada ya kulipia na kupewa tikiti?
 
Wananchi wengi wamekuwa wakiharibiwa magari yao kwa kuburuzwa ovyo, lakini pia imekuwa inazusha ugomvi mara kadhaa baina ya wanamgambo na raia. Sidhani kama hii ndilo kusudio la mamlaka hizi.

Nawaomba sana wenzetu mnaohusika katika halmashauri hizi mzingatie utawala wa sheria na kuheshimu haki na misingi ya kiutu. 

Huu si utaratibu mzuri; kimsingi haswa makosa yalianza na halmashauri, hivyo si sahihi kuwajibisha watu kwa makosa ya halmashauri husika. Ni budi halmashauri kuogeza sehemu za kupaki magari kwanza, ili ionekane kama yupo ataekubali kuacha gari yake barabarani ili apate adhabu
Kiungwana ‘ukijikwaa usiangalie ulipoangukia, angalia nini kimekufanya ujikwae’’

Murtaza Mangungu(MB)
Kilwa Kaskazini

No comments:

Post a Comment