Pages

Pages

Saturday, October 19, 2013

Edo Kumwembe: Sikuwa na mkataba Coastal Union


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MSEMAJI wa zamani wa Coastal Union, Edo Kumwembe, amesema kwamba hakuwa na mkataba wowote ndani ya timu hiyo yenye maskani yake jijini Tanga, badala yake alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea kama mdau wa mpira wa miguu.

Edo Kumwembe, pichani.
Kumwembe aliyasema hayo siku chache baada ya kudaiwa kuwa amemaliza mkataba wake ndani ya timu hiyo na hakuna juhudi za kuongeza ili aendelee na kibarua chake.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kumwembe ambaye pia ni mchambuzi wa mambo ya soka, alisema kuwa lolote linalotokea ndani ya timu hiyo hawezi kulalamika kwakuwa tangu mwanzo hakuwa na mkataba wowote.


Alisema jambo hilo linamfanya aone kuwa hana anachoharibikiwa katika suala hilo, ambalo habari zinazotolewa katika vyombo vya habari zinasema Kumwembe na kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco mikataba yao imekwisha.


“Kama unazungumzia kocha wa Coastal Union sawa, ila kwa upande wangu sikuwa na mkataba wa kuwa msemaji wa timu hiyo yenye maskani yake jijini Tanga kwa wagosi wa kaya,” alisema.


Aidha, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Coastal Union ya Tanga, Albert Clement Peter , maarufu kama ‘Mkubwa wa Kazi’ alikanusha vikali taarifa zilizosambazwa na baadhi vyombo vya habari kuwa wamemfukuza kocha wao Morocco.


“Hatujamfukuza kocha huyo kama ilivyoripotiwa bali mkataba wake wa kuendelea kuinoa timu hiyo umekwisha hivyo tutaandalia hatima yake, huku kwa sasa akiwa Bukoba kwa ajili ya kukipiga na Kagera Sugar ya mjini humo,” alisema.


Kwa mujibu wa Peter, uongozi unakaa kuangalia namna gani ya kuendelea na kocha huyo au wamuache, ila si kweli kuwa tayari ameshaondolewa kikosini.

No comments:

Post a Comment