Pages

Pages

Wednesday, September 11, 2013

Sakata la dawa za kulevya, Kaseba awalilia wanamichezo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini, Japhet Kaseba, amesema kuwa maisha yamekuwa magumu kwa wanamichezo, hivyo hatari inaweza kuwa kubwa kutokana na vijana hao kujiingiza kwenye dawa za kulevya.

Kaseba ameyasema hayo siku chache baada ya madai ya kukamatwa kwa wanamichezo Mkwanda Matumla na Joseph Kaniki, aliyewahi kuwa nyota wa kandanda katika klabu ya soka ya Simba.

Akizungumza leo mchana jijini Dar es Salaam, Kaseba alisema kuwa kutokana na kusumbuliwa na ukata, baadhi yao wanajiingiza katika masuala hayo ya dawa za kulevya.

Alisema serikali inapaswa kuwa makini zaidi katika suala hilo, ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema sera ya michezo ni ajira ili kuboresha kipato cha wanamichezo.

“Kijana anaona hana cha kujivunia kutokana na ukata, hivyo wasiwasi wangu wengi wao wanaweza kujiingiza kwenye suala la dawa za kulevya na kuathiri nguvu kazi ya Taifa.

“Kwangu mimi nitaendelea kulia juu ya njaa za wanamichezo na lazima juhudi za ziada zifanyike ili kuokoa vijana wetu ambao wamekuwa na vipaji vya aina yake,” alisema Kaseba.

Sakata la kukamatwa na dawa za kulevya kwa Tanzania limezidi kugonga hisia za wengi, huku kila baada ya wiki moja kutokea tukio jipya la Mtanzania kunaswa na ubebaji wa dawa za kulevya na kulitia aibu Taifa.

No comments:

Post a Comment