Pages

Pages

Wednesday, September 18, 2013

MGODI UNAOTEMBEA:Tunahitaji wabunge makini na wenye kuuchukia umasikini


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UMUHIMU wa elimu ni pale inapotumika kwa maslahi ya wananchi wote, hata wale wasiobahatika kufikia kiwango hicho. Kama mtu mwenye elimu anafanya mambo yasiyokuwa na faida, jibu lake ni kuwa elimu yake hiyo haina msaada na haina tija.
Watanzania kama hawa wanahitaji maisha bora ili wawe na uhakika wa mlo kamili na sio wengi wao kuzuunguka bila mafanikio. Wabunge na watendaji wengine wa serikali wakiunganisha vikundi kwa watu hawa wanaweza kujikimu kwa kufanya biashara mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Mtu wa aina hiyo ni kama yule anayetembea bila kuvaa nguo, ingawa mguuni mwake ametinga kiatu kizuri, akijidanganya kuwa amejikinga na kukanyaga vinyesi au misumari na miiba.

Kadri ya siku zinavyozidi kwenda mbele, kumekuwa na mihemko kutoka kwa watu wanaoamini kuwa ili mbunge awe na faida kwa wananchi lazima awe ni profesa au dokta.

Hata hivyo haitoshi, watu hao wanafika mbali zaidi wakiamini kuwa watu wa aina hiyo wana uwezo wa kuwawakilisha vyema wananchi wao, jambo ambalo si kweli.

Japo sipingi wabunge wenye elimu au wale wanaotaka kuwania nafasi hiyo wawe na kiwango kikubwa kama kinavyohitajiwa na wengi, ila muhimu ni kuwataka watu hao wahakikishe kuwa elimu zao zinawanufaisha Watanzania na wapiga kura wao wanaoishi maisha ya kubahatisha, huku wao wakiishi kifalme.

Kwa mfano, mbunge wa Korogwe Vijijini, Profesa Stephen Ngonyani, maarufu kama Maji Marefu ameonyesha utofauti mkubwa na wabunge wenzake, wakiwamo wapya na wa zamani.

Maji Marefu amekuwa karibu mno na wapiga kura wake. Ukienda Kororgwe Vijijini utafahamu mazuri anayofanya mbunge huyo aliyeingia madarakani mwaka 2010.

Binafsi naupongeza mchango wa Maji Marefu, huku nikitangaza vita na wabunge wengine wasiokuwa na jipya wala faida kwa wapiga kura wao miaka nenda rudi.

Kwa mfano, kazi ya kwanza ya mbunge ni kuwaunganisha wananchi wake ili ajuwe namna ya kuwaletea maendeleo. Hii si mpaka mbunge asubiri mipango kutoka ofisi nyingine ya serikali.

Mbunge anaweza kuanza kuunganisha vikundi vya wananchi, kama vile wakulima, wafugaji, wafanyabiashara katika masoko mbalimbali kwa nia ya kuwaweka pamoja.

Baada ya kufanya hivyo, kama mfuko wake hauna fedha za kuendesha vikundi hivyo, anaweza kubuni njia nyingine ya kuwasaidia ukiacha utaratibu wa kuomba misaada kutoka kwa wahisani.

Kikundi chochote kilichokuwa na wafanyabiashara hata wa nyanya sokoni, wakajiunganisha watu wasiopungua 50 hadi 100 wanaweza kujiwekea njia ya utajiri mkubwa mno.

Hawa wakiamua kuchangishana hata 10000 kwa mwezi ni sawa na 120,000 kwa mwezi mmoja. Watu hao wakiendelea na utaratibu huo kwa mwaka mmoja watavuna jumla ya Sh Milioni 120.

Fedha hizo sidhani kama zitashindwa kuwasaidia na kuwawekea mfumo mzuri wa kimaendeleo. Watu wa aina hii wapo wengi. Mbunge makini na mwenye mtazamo wa mbali kwanini ashindwe kufanya mpangilio huu kwa ajili ya maendeleo ya wapiga kura wake?

Serikali inaamini kuwa ili iweze kuwasimamia wananchi wake na hata kuwakopesha lazima wajiunganishe kwa vikundi. Je, nani wa kufanya hayo? Tunahitaji elimu ya Chuo Kikuu kubaini fursa nyingi zinazoishia hewani?

Kwa bahati mbaya, mara kadhaa inapotokea wananchi wenyewe wanahitaji kujiletea maendeleo kwa kuunganisha vikundi, hutokea mgawanyiko unaoshangaza wengi.

Mara kadhaa wabunge na wanasiasa wengine wamekuwa wakihofia nafasi zao, hivyo kutumia hila kuwasambaratisha. Huu sio mpango mzuri. Hatuwezi kuendelea kama hatuna uthubutu.

Watu wanaishi maisha magumu. Kule kwetu wilayani Handeni, mkoani Tanga, kila siku ni malalamiko. Mbunge wa Handeni, Abdallah Omari Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara anakutana na shughuli pevu mno.

Wengi wanaamini katika kipindi cha miaka 20 alichokaa bungeni hakuna cha maana alichofanya, japo kuwa kuna barabara nzuri sasa kutoka wilayani Korogwe kwenda Handeni na ile inayotoka Handeni kwenda Mkata. Hata hivyo, malalamiko hayo kwa viongozi hayawezi kukosekana hata kidogo.

Kama tunavyojua, mema mengi hufichwa na baya moja tu, hivyo hata kama afanye mema mangapi, lakini kama kuna anayelala analala njaa, anayeshindwa kupata huduma muhimu za afya, anayekosa vitu vyenye kuongoza maisha yake, huyo hawezi kukaa na kushangilia, hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wamekuwa na ujasiri wa kuuliza au kuwajibisha viongozi wao.

Kama watu wanakosa mbinu mbadala za kupambana na shida ya maji, njaa kila mwaka, vijiji vingi hata vile vilivyokuwa kwenye (underline) vinakosa huduma muhimu ya umeme, kamwe wananchi wake hawawezi kufurahia mfumo na uongozi wao.

Huu ni wakati sasa wa kukaa na kutafakari mwenendo wa uongozi, hasa wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi. Kwa bahati mbaya, wengi wa wabunge hao wanaolalamikiwa wanatokea katika Chama Tawala, yani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kama hivyo ndivyo, ugumu wa maisha, kulala kwa baadhi ya wabunge wake ni pigo kwa CCM. Mwaka 2015 huenda ukawa mgumu kwa baadhi ya majimbo ambayo wabunge wao wamekosa mbinu mbadala za kuwakomboa wananchi wao.

Kwa mtindo huo, CCM itakuwa inakosea sana kama itaamini kuwa wabunge wao hao wanabebeka. Lazima itafute namna ya kuwadhibiti au kuwasimamia hasa katika miaka miwili hii iliyobakia.

Katika kila jimbo au wilaya, lazima kutakuwa na kero sugu ambayo inaumiza watu wengi. Maeneo mengine ni barabara za uhakika na kwingine ni maji au umeme.

Huduma hizi, yani barabara, maji na umeme ni muhimu. Yanagusa maisha ya mlalahoi kabisa. Tajiri hawezi kulalamika. Kama barabara haipitiki, yeye haimuhusu kwasababu muda mwingi anaishi mjini.

Kama tatizo ni maji, yeye anaweza kuchukua maji mahali popote apendapo kwa ajili ya maisha yake. Kama tatizo ni umeme, anaweza kununua solar power na kutumia kadri apendavyo.

Akiugua hana shida ya kutibiwa katika zahanati ambayo tangu ijengwe haijawahi kuwa na dawa za kutosha. Hata zile za kupunguza makali ya homa ya matumbo wanazipata zikiwa zimeshaharibika kutokana na kutohifadhiwa sehemu nzuri na salama.

Haya yote yanafanyika katika maeneo yenye wabunge waliochaguliwa kwa mtindo wa kura. Tena baadhi yao wanajipitisha kwa wananchi au katika vyombo vya habari wakijitangaza kuwa wao ni machaguo halisi ya wapiga kura wao.

Ni sahihi kujiita hivyo. Lakini mtu huyo anapaswa kupima viatu vyake. Ni vyema pia akafikiria namna wananchi wake wanavyoteseka. Ni vyema akafikira nafasi yake bungeni.

Tangu alipoingia madarakani, ni mara ngapi ameweza kusimama kuuliza maswali yanayowahusu wananchi wake? Je, tangu alipoingia madarakani, ameweza kutekelekeza mambo mangapi?

Kipi kipaumbele chake? Je, ipi mipango yake katika kipindi cha miaka miwili hii iliyosalia? Kimahesabu, bado mwaka mmoja tu. Tena ule ambao utakapoingia utakuwa na mlolongo mrefu.

Ni mwaka wa Uchaguzi wa serikali za mitaa. Uchaguzi ambao kila chama utatumia kujiimarisha na kujiwekea mikakati ya kushinda uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Kama hivyo ndivyo, namna gani wabunge hao wataweza kujipanga kwa ajili ya kuwakomboa wapiga kura wao? Hakuna njia ya mkato. Katika hili kila mtu lazima atomize wajibu wake.

Japo wasema kweli wataonekana ni wachochezi lakini bora waseme ili wajisahihishe. Hii ni kwasababu hata CCM wenyewe wanaamini kuwa wao sio malaika.

Katika utawala wao kuna mabaya na mazuri. Yale mabaya wanaamini watayafanyia kazi kwa ajili ya kuwapatia maisha bora wananchi wao katika kipinddi chote cha utawala wao.

Kuna mengi yanayostahili kufanywa, ila kubwa ni kuhakikisha kuwa wabunge wao wanakuwa wawakilishi wa wananchi wao. Waone ile thamani ya wao kulipwa mshahara mnono na mazuri mengi kutoka bungeni.

Wabunge hawa wauchukie kwa vitendo umasikini. Watumie muda wao kuwa karibu na wananchi wao. Waanzishe miradi ya kimaendeleo, kama vile ufugaji wa nyuki, ufugaji wa kuku wa kisasa na kienyeji, kuvua samaki na mengineyo.

Wasimamie vyema sera ya kilimo kwanza ili kiwe na tija. Wafanikishe kupatikana kwa pembejeo za kilimo na kuwakopesha wananchi wao sanjari na kuwadhibiti katika uuzaji wa mazao yao.

Wabunge hawa watafanya hayo kwa kutumia wataalamu wa serikali waliozagaa kila wilaya kwa ajili ya kusimamia sera hizo na fursa za kimaendeleo.

Wakifanya hivyo, hata elimu zao zinazopigiwa chapuo zitaonekana ni muhimu, maana zinafanikisha maisha bora kwa Watanzania wao, hasa wale waliosimama mstari kuwapigia kura.

Aidha, sera hii itakuwa ni tunu kwa Watanzania wote, ukizingatia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anaamini kuwa katika kipindi cha uongozi wake, lazima wananchi wake wayapate maisha bora.

Hili linaweza kufanikiwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kuwa wabunge wao wanashirikiana vyema na wananchi wao na sio wale wanaotumia muda mwingi  kujenga makundi yao. Wale wanaotumia muda mwingi kufanya biashara zao.

Wale wasiokuwa hata na muda wa kuzungumza na wananchi wao kuona namna gani ya kuwapatia mwangaza wa kimaisha kwa kupitia wao walioomba fursa ya kuwaongoza.

Tusipofanya hivyo, wananchi watakuwa na chuki na viongozi hawa hasa katika kipindi cha Uchaguzi ambapo hakika uwezekano wa kupiga kura za chuki ni mkubwa mno.

+255712053949

Mwisho


No comments:

Post a Comment