Pages

Pages

Saturday, September 14, 2013

Kivumbi cha Ligi ya Tanzania Bara kuendelea tena leo kwa timu zote 14 kushuka dimbani


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu leo Septemba 14 kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya Mbeya City na Yanga.
Kikosi cha Simba
Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.


Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.


Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.


Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam).

No comments:

Post a Comment