Pages

Pages

Sunday, August 11, 2013

Yanga: Mechi yetu na Villa ya Uganda ni muhimu kwetu leo Uwanja wa Taifa


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema mechi yao ya kirafiki ya Kimataifa dhidi ya Sport Club Villa ya nchini Uganda ni muhimu kwa ajili ya kumpa kocha nafasi ya kuangalia mapungufu yao kabla ya kuanza patashika ya Ligi ya Tanzania Bara itakayoanza Agosti 24 mwaka huu.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, pichani.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka hapa nchini, imepangwa kuanza kutimua vumbi saa 10 za jioni katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo wadau wao watajionea burudani ya aina yake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kocha wao Ernest Brandit, atapata fursa ya kuangalia uwezo wa vijana wake kabla ya michuano kuanza.

Alisema kabla ya ligi hiyo kuanza, Yanga pia itaingia uwanjani Agosti 17 kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya timu ya Azam FC,iliyoweka kambi nchini Afrika Kusini.

“Ni mechi kali ya kirafiki dhidi ya Sport Club ya Villa ya Uganda, huku kiingilio cha chini kabisa kwenye mchezo huo kikiwa shilingi 5000 kwa mzunguuko ili kutoa fursa kwa mashabiki kuingia kwa wingi zaidi.

“Tunaamini kocha wetu pamoja na benchi lote la ufundi litapata fursa ya kushuhudia makali na mapungufu ya wachezaji wao ili waone namna ya kuboresha kwa ajili ya kuleta ushindi katika mechi zijazo,” alisema.

Yanga tayari imejigamba kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kutetea taji lao ililotwaa msimu uliopita kutoka kwa mtani wao wa jadi, Simba SC, huku nafasi ya pili ikienda kwa Azam watakayokutana nayo kugombea ngao ya Hisani.

No comments:

Post a Comment