Pages

Pages

Monday, August 19, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Filimbi ya malalamiko, mnyukano TFF imepulizwa



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HATIMAE filimbi ya hujuma, pilikapilika, mnyukano ndani ya Ofisi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imepulizwa, baada ya Kamati ya Uchaguzi kutangaza mchakato na siku ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo.
Mdau wa mpira, Michael Wambura
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni, aliwatangazia Watanzania uchaguzi huo sasa utafanyika Oktoba 20 mwaka huu.

Kwa kauli yake hiyo, ni wazi kuwa sasa wadau wa michezo hususan mpira wa miguu wameingia kwenye mihemko ya uchaguzi huo.

Ni wazi wajiandaye kwa lolote kutoka TFF. TFF ambayo imekuwa ikisababisha malalamiko ya aina yake, ndio maana hata Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika kwa wakati.

Nikiwa kama mdau wa michezo hususan mpira wa miguu, ni wazi nina hamu ya kuona uchaguzi huo ukifanyika kwa wakati bila kuleta mzozo wa aina yoyote.

Kamati hiyo isijaribu kuweka hila za aina yoyote, huku ikiwaacha wale wanaopenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kutumia haki zao za msingi.

Uchaguzi huu ambao ulivunjwa baada ya kuibuka kwa mkanganyiko wa aina yake, uliichafua pia soka la Tanzania, hasa pale tulipolazimika kuwaita wageni waje kutuamulia mambo yetu ya ndani.

Hii siwezi kuvumilia hata kidogo. Ni wakati sasa wa kuwa wakali juu ya wale watakaoendelea kuturudisha nyuma kila wakati kwa faida wanazojua wenyewe.

Sura mpya za uongozi za TFF zitaonekana katika siku hiyo ya Uchaguzi, ambapo tutashuhudia pia Rais anayemaliza muda wake, Leodgar Tenga, akielekea mwishoni.

Kwa wale wanaofuatilia soka, watakubaliana na mimi kuwa heshima ya Tenga ya zamani ilitoweka kama barafu juani, hasa kutokana na kushindwa kuwasimamia vyema watendaji wake au Kamati za TFF.

Mara kwa mara tulishuhudia majibizano na kutoelewana kwa kiasi kikubwa, hivyo wadau wa soka kushangaa umuhimu wake ndani ya Shirikisho hilo.

Wahenga wamesema yaliyopita si ndwele. Hebu tugange yajayo kuona kuwa Shirikisho hilo linapata viongozi wake kama inavyotarajiwa na wengi.

Hatuhitaji tena malumbano yasiyokuwa na msingi, maana ndio kitu kitakachotuangamiza katika soka la Kimataifa. Watanzania licha ya kuwa na vipaji vya aina yake, lakini tunashindwa kuwika nje ya mipaka yetu.

Wakati hayo tukiendelea kujipa moyo, tunagundua kuwa nchi za Kenya na Uganda zimetuacha mbali mno. Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inapata kazi kubwa inapokutana na timu za Harambee Stars na Uganda The ‘Cranes’, timu ilizokuwa inajipigia mara kwa mara.

Kama hivyo ndivyo, kwanini tusibaini mapungufu yetu? Kwanini tusiweze kushikwa na usongo kiasi cha kufanya bidii ili soka letu lisonge mbele?

Tunaweza kufanya hivyo na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini kama hakutakuwa na njia za panya wala malumbano juu ya uchaguzi huo wa TFF.

Uchaguzi ndio kila kitu kwa soka la Tanzania. Tunahitaji viongozi wanaopatikana kwa haki na sio wale wanaobebwa au wale wanaokandamizwa kila wakati.

Sheria zifuatwe katika kuelekea kwenye Uchaguzi huo unaovuta hisia za watu wengi. Inapofikia wakati huo, mambo mengi yamekuwa yakiwaka moto, hasa kwa nafasi za Urais na Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo.

Kuchangamkia fursa hiyo kwenye uchaguzi huo wa TFF, ni wazi wamebaini fursa na mafanikio katia nafasi hizo, ila lazima kiu yao hiyo ilete mabadiliko katika mpira wa miguu.

Kama tusipokuwa makini katika hilo, ni wazi hatutakuwa na mafanikio katika sekta ya mpira wa miguu, maana kwenye msingi wa kwanza ambao ni uongozi tulishindwa kuwa makini na kuweka mipango ya kimaendeleo.

Katika hili kamwe siwezi kuvumilia, hasa pale nitakapobaini watu wachache wanaendelea kufanya mambo yanayoweza kuangamiza soka la Tanzania badala ya kuingia watu wa mpira, wenye kujua mbinu za kupiga hatua Kimataifa.

Tukutane wiki ijayo.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment