Pages

Pages

Saturday, August 17, 2013

Filimbi ya uhondo wa Fiesta kupulizwa leo mkoani Kigoma



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI wazi hakuna Tamasha kubwa la muziki hapa nchini, isipokuwa hili la Fiesta 2013, linalotarajiwa kuanza kuwaka moto leo mkoani Kigoma, katika Uwanja wa Lake Tanganyika.

Shoo hiyo inayofanyika kila mwaka, uzinduzi wake unaanzia mkoani Kigoma, ambapo shughuli itaendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Ruge Mutahaba
Wadau wa muziki wa Tanzania wamekuwa na shauku ya tamasha hilo kunaatokana na kusheheni wasanii wenye uwezo wa juu wa kuimba na wenye mashabiki lukuki.
Linah, pichani
Wasanii kama vile Barnabas, Mwana FA, AY, Madee, TID, Linah, Recho na wengineo wamepangwa kuwapo katika uzinduzi huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wake.

Katika kila mkoa wa Tanzania Bara, shoo ya Fiesta ndio pekee yenye mguso na inayosisimua kwa kiasi kikubwa, ndio maana mara kadhaa imekuwa ikifanyika uwanjani.

Katika mazungumzo na Handeni Kwetu Blog yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, anasema kuwa tamasha la Fiesta limeshakamilika kwa maandalizi yake.

Mutahaba anasema kuwa mambo mengi yameboreshwa ukiwamo mpango wa wasanii kupanda jukwaani au mikakati ya ufanyaji shoo wenye kuwapa burudani mashabiki wao.

“Shoo ya Fiesta ndio pekee yenye mguso kwa nchi hii, hivyo sisi kama waandaaji tunachofanya ni kuweka mkazo na mguso katika kuandaa ili wadau wetu waburudike.

“Hakuna kinachofanyika kwa sasa zaidi ya kuangalia Fiesta itakuwaje kwa msimu huu mpya, huku mikoa mbalimbali ikitarajiwa kupata shoo hii, hasa mikoa ya Kigoma na Mtwara,” alisema Mutahaba.

Ruge anasema kuwa mikoa ya Kigoma na Mtwara inafanyika shoo hiyo kwa mara ya kwanza, huku wakiamini kuwa italeta burudani na kuwaweka pamoja wadau wote.

Wakati Kigoma shoo hiyo ikipangwa kufanyika kesho, wenzao wa Mtwara watapata burudani ya tamasha hilo Jumamosi ya Agosti 31 na kushuhudia burudani hiyo.

Anasema kwamba baada ya tamasha hilo kuzinduliwa rasmi mkoani Kigoma, watafuata wakazi na wananchi wa Tabora, ambapo Agosti 23 nao wataburudika kwa idadi kubwa ya wasanii waliopangwa kuwapo katika tamasha hilo la aina yake.
Mikoa mingine ambayo itapata shoo hiyo ya Fiesta ni pamoja na Singida, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Tanga, Arusha, Moshi, Musoma na Shinyanga.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Utafiti na Matukio wa Clouds, anasema kuwa Fiesta pia imeongezwa mikakati ya kutafuta namna ya kuwapatia maisha bora Watanzania.

Anasema katika mkoa wa Kigoma, kabla ya shoo hiyo, pia watafanya semina na vijana kama walivyofanya mkoani Dodoma katika uzinduzi wa ‘Twenzetu’.

Mkoa wa Kigoma ambao una mambo mengi mazuri, lakini umekosa mwamko, ndio maana sisi kwa pamoja tukaamua tuingie kwa ajili yaa kufuta tatizo hilo.

“Hii si sahihi, hasa watu wanaposema kuwa mkoa wa Kigoma ni wa mwisho, wakati sisi tunajua kuna mambo mengi yenye mwangaza kwa ajili ya maisha ya wakazi na wananchi wao.

“Hii ni sawa na Mtwara, hivyo tutakuwapo kwa mikoa hii miwili na mengine kwa ajili ya kuhamasisha pia mbiu yetu ya Twenzetu iliyozinduliwa mkoani Dodoma mapema mwaka huu,” alisema Mutahaba.

Anasema juu ya masuala ya amani na utulivu ni jambo la kwanza sehemu zote wanazokuwapo, jambo linalowafanya Watanzania waamini hakuna tamasha lingine lenye mguso na mwanamko kama Fiesta.

Naye Winfirda Josephat maarufu kama (Recho), alijigamba mno juu ya kuonyesha manjonjo yake katika tamasha hilo la Fiesta litakalozinduliwa mkoani Kigoma.

Anasema kuwa amejiandaa vizuri kufanya mambo makubwa katika tukio hilo linalokusanya mashabiki wengi kwa wakati mmoja ili kufurahia muziki kwa ujumla.

Anasema kuwa anaamini alichofanya katika tamasha la mwaka jana kitakuwa kidogo kati ya vitu atakavyoonyesha katika burudani za Fiesta mwaka 2013.

“Sitaki kuongea sana, maana najua sehemu ya kuonyesha mbwembwe ni jukwaani, hivyo naomba wadau wote na mashabiki wangu waje kujionea vitu vya hali ya juu.

“Nipo sawa na nimejiandaa kwa kipindi kirefu mno, huku nikiwa na kila sababu ya kupanda jukwaani na kuwapatia shoo ya aina yake mashabiki wote wa tamasha hili,” alisema.

Recho anatamba na nyimbo kadhaa, ukiwamo wa Kizunguzungu, Upepo, Nashukuru Umerudi na sasa ameachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la Mwali Kigego.

Recho anajulikana sana kwa kufuata nyayo za mkali mwingine wa muziki huo, Rehema Chalamila, maarufu kama Ray C, ambaye mara kwa mara ameshindwa kuficha uhalisia huo.

Mwanadada huyo ametokea katika taasisi ya kukuza na kulea vipaji ya Tanzania House of Talents (THT), kama ilivyokuwa kwa Linah, Barnabas, Mwasiti, Amini, Vida, Mataluma na wengineo waliotokea kwa juhudi za taasisi hiyo ya muziki nchini.

No comments:

Post a Comment