Pages

Pages

Wednesday, August 21, 2013

CRDB waja kuwakomboa Watanzania kwa mkopo wa nyumba



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TANZANIA ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake wanaishi maisha ya kubangaiza, huku wakisumbuliwa pia na changamoto za ukosefu wa nyumba za kuishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dk Charles Kimei akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya 'Jijenge' inayohusiana na mambo ya mikopo ya nyumba kwa wateja wao.

Katika jiji la Dar es Salaam, tunashuhudia wakazi wake wengi wakiishi katika nyumba za kupanga, tena zile zisizokuwa na ubora.

Mtu anaishi kwa mashaka wakati wote, hasa pale kinapoingia kipindi cha mvua na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba zao.

Hii ni kwasababu Mtanzania wa kawaida kuweza kumiliki nyumba kunahitaji mihangaiko ya kutosha, huku baadhi yao wakilazimika kudokoa kwenye maeneo yao ya kazi ili wafanikishe ndoto zao.

Wakati hayo yakiendelea kuwa kero kwa Watanzania, benki ya CRDB imekuja kufuta changamoto hizo baada ya kuzindua huduma ya kuwakopesha wateja wao nyumba bora za kuishi.

Mkopo huo unaojulikana kama (Jijenge) utakuwa majibu tosha kwa wanaohangaika na maisha yao, ukizingatia kuwa sasa kila mwenye ajira yake anayelipwa kiasi cha Sh 200,000 ana sifa za kukopeshwa nyumba na benki ya CRDB.

Katika mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Tanzania, Dk Charles Kimei, anasema kuwa wameamua kuanzisha huduma hiyo ili kuwapatia maisha bora Watanzania wote.

Anasema kuwa baada ya kuwaza namna gani ya kuchangia maisha bora kwa Watanzania, ndipo benki yao ilipobuni wazo hilo la aina yake.

“Watu wanaishi maisha magumu na hawana matumaini ya kuweza kuishi kwenye nyumba zao, hivyo kwa kuchukua mkopo wa CRDB basi kila kitu kinawezekana.

“Tumeweka utaratibu rahisi mno kwa wafanyakazi kuanzia kipato cha laki mbili 200,000 kwa mwezi ambapo tunaamini tumejibu vilio vyao,” alisema.
Tanzania ina upungufu wa nyumba milioni tatu, huku kiasi kidogo kilichokuwapo kuleta joto kali kwa wananchi.

Ongezeko la nyumba laki 200,000 kwa mwaka halisaidii kupunguza msoto wa upatikanaji wa nyumbaa bora kwa Watanzania wote.
Hakuna masharti magumu ya kuweza kupewa mkopo huo uliogawanyika katika makundi matatu muhimu.

Kuna wale wanaokuwa tayari kuchukua mkopo wa kujenga nyumba zao, kununua zilizojengwa au wale wanaotaka kuboresha nyumba zao.

“Kila mkopo umewekewa utaratibu wake, huku mkopaji akiishi bila presha maana atapewa miaka 20 hadi kukaamilisha kumaliza deni lake.

“CRDB tunachoweza kufanya ni kumpatia mkopo anaotaka mteja wetu, ila hati yake itabaki katika mikono yetu hadi atakapomaliza kulipa, huku marejesho yake yakiwa madogo kupita kiasi,” alisema.

Anasema kuwa wananchi wengi wameshindwa kumiliki nyumba kwasababu ya kupanda kwa gharama ya kumiliki ardhi, kupanda kwa gharama za ujenzia sanjari na vifaa vyake, ikiwamo saruji, nondo na vinginevyo.

Changamoto hizo zinasababisha pia kuwafanya watu wengi waaishi kwenye nyumba zisizomalizika (mahame) hali inayoharibu mwonekano wa jiji katika macho ya wageni wanaokuja kutembelea Tanzania.

Dk Kimei anasema mara kadhaa Watanzania wamekuwa wakiishi kwa kujenga kutokana na akiba wanazojiwekea, ukiwa ni mfumo uliopitwa na wakati, ukizingatia kuwa Dunia ya leo inahitaji mipango na ubunifu wa hali ya juu, hasa ukopaji wa nyumba.

Watu hao wanapokopa katika mashirika ya fedha na benki kunafanya waishi kwenye nyumba imara na zenye ubora, ambapo marejesho yake hayaonekani kuwa magumu tofauti na zamani.

Kwa wale wanaoishi kwenye za kupanga huku wakilipa zaidi ya 100,000 kwa mwezi, ni ajabu kama watashindwa kukopa nyumba ili waondokane katika matatizo yao ya kuishi kwa kubahatisha.

Mtu akihamishwa, anaweza kuuza nyumba yake na kuendelea na maisha yake sehemu nyingine ambapo pia fedha hizo anaweza kununua jingo jingine sehemu anakoelekea.

“Haya ni mambo yasiyohitaji gharama kubwa katika mfumo wa maisha ya sasa, hivyo kuna kila sababu ya Watanzania wakiwamo wateja wetu wa CRDB kushawishika katika utaratibu huu,” alisema Kimei katika uzinduzi huo wa huduma hiyo.

Dk Kimei anasema mikopo hiyo ya ‘Jijenge’ ikitumiwa vizuri, watu wataishi kwenye nyumba bora na zenye furaha pamoja na familia zao, huku wakipata huduma zote za jamii kama vile umeme, maji na barabara.

Huduma hiyo ya Jijenge inawahusu watu wote, wakiwamo wafanyakazi walioajiriwa kwenye sekta zote, sambamba na wale waliojiajiri wenyewe.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya makazi, soko la mikopo ya nyumba kwa jiji la Dar es Salaam (Mortgage Business), linakadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 480 kutokana na takwimu za mwaka 2012.

Aidha, Mtanzania wa kawaida ili aweze kumiliki nyumba yake mwenyewe inamchukua miaka 10, huku chanzo cha ukopaji kwa kutumia dhamana ya kitu kisichohamishika, ambacho mara nyingi ni nyumba au kiwanja ikiendelea kuwa mwiba mkali.

Dk Kimei anasema kwamba kiwango cha mwisho cha ukopaji katika benki yao kwa ajili ya kukopeshwa nyumba ni Milioni 500.
Malengo na sifa ya mikopo ni mshahara, michango ya pensheni (sio zaidi ya asilimia 50), mapato ya kodi ya pango, huku matawi yote ya benki ya CRDB yakiweza kumhudumia mteja juu ya huduma hiyo ya Jijenge ya inayohusika na ukopaji wa nyumba.
Mahitaji muhimu kwa mkopaji ambaye ni mjasiriamali ni pamoja na historia pamoja na maelezo ya mteja juu ya biashara yake, taarifa ya fedha iliyokaguliwa na mtaalamu (auditor) kwa kipindi cha miaka mitatu ya karibuni na makadirio ya mtiririko wa fedha.
Mizania na ripoti ya hesabu za faida, hasara za miaka mitatu, pamoja na taarifa ya hesabu za benki kwa miaka 12 kutoka benki ya CRDB na nyinginezo kama zipo, bila kusahau maelezo na viambatanisho vyote juu ya mikopo kutoka benki zote.
Mteja ambaye ni mwajiriwa anatakiwa awe na stakabadhi ya malipo yake ya mshahara kwa kipindi cha miezi sita ya karibuni, taarifa kutoka benki ambayo mshahara wake ulipopitia, barua kutoka kwa mwajiri yenye maelekezo ya kutosha juu ya aina ya mkataba wake, umri wake na taarifa ya mfuko wa fao la uzeeni, mshahara na posho zake kwa ujumla.
Kuanzishwa kwa huduma hiyo, ni wazi Watanzania watakuwa wamejikomboa katika changamoto ya ukosefu ya nyumba bora za kuishi.

No comments:

Post a Comment