Pages

Pages

Monday, July 15, 2013

WAASI DARFUR WAILIZA TANZANIA

WAASI wa Jimbo la Darfur nchini Sudan wameliliza Taifa baada ya kuwashambulia kwa kuwapiga risasi askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwajeruhi wengine vibaya. Kutokana na hali hiyo, JWTZ limethibitisha askari saba kuuawa.

Mbali ya vifo hivyo, JWTZ limesema askari wengine 14 wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la kushtukiza lililofanywa na kundi la waasi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe alisema wanajeshi hao walivamiwa wakati wakiwa kwenye msafara wa kuwasindikiza waangalizi wa amani ambao walikuwa wanatoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyara Darfur.

Alisema katika shambulizi hilo, kikundi cha wanajeshi wa Tanzania kilipoteza askari saba na wengine 14 kujeruhiwa, akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na maofisa wengine.

“Hizi ni taarifa za awali ambazo tumezipata, wanajeshi wetu wamepatwa na mkasa wakiwa katika utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Sudan.

“Kama navyofahamu kifungu namba 6 cha majeshi ya kulinda amani, kinakataza matumizi ya nguvu, lakini kutokana na hali hii, JWTZ tutafanya mazungumzo na UN ili kuangalia kama tunaweza kutumia kifungu namba 7 ambacho kinaruhusu matumizi ya nguvu hasa wakati wa kujihami.

Kutokana na hali hiyo, JWTZ limesema linafanya mazungumzo na Umoja wa Mataifa (UN), ili liruhusiwe kutumia silaha kama njia ya kujihami na mashambulizi kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 7 cha sheria za UN.

Alisema kutokana na hali hiyo, JWTZ inafanya mawasiliano na familia za marehemu kuhusu taratibu za mazishi pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu taratibu zote muhimu zinazohusiana na matibabu ya watu waliojeruhiwa katika eneo la tukio.

Mbali na hatua hiyo, alisema kuwa ujumbe maalumu umeteuliwa kwenda Khartom na Darfur ili kuzungumza na mamlaka kuhusiana na tukio hilo.


No comments:

Post a Comment