Pages

Pages

Monday, July 22, 2013

SIWEZI KUVUMILIA:Tupige domo, tukichoka tucheze soka


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa michezo, hususan viongozi wao kwa ujumla wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hali hii inasababisha juhudi zinazofanywa kuwa za zimamoto huku nchi nyingine zikisoganga mbele.
Ivory Coast ni Taifa linalofanya vema katika soka wakati Watanzania tunaendelea na porojo zetu.
Nchi kama vile Uganda, leo imeweza kujiweka katika nafasi nzuri mno katika soka, wakati majirani zao Tanzania hawana jipya. Leo hii Taifa Stars, kuwafunga Uganda ndani au nje ya nchi ni kazi kubwa.

Naweza kulaumu kwa namna moja ama nyingine, ila kwa kiasi Fulani viongozi wetu wa soka, hususan wanaoongoza klabu zetu Tanzania kutokuwa na jipya katika mipango yao.

Leo hii usajili wa klabu ya Simba, unafanywa na Katibu au Mwenyekiti wa Usajili, ambaye hajui chochote kinachohusu mambo ya ufundi. Hata kama akijua, sidhani kama makocha wanashirikishwa.

Hali hii ni mbaya mno. Na hakika siwezi kuvumilia, maana kinachofanywa sasa ni porojo zisizokuwa na mashiko. Ndio maana nasema tupige domo letu kadri tuwezavyo, tukichoka tucheze soka.

Nasema hivi huku nikiumizwa mno kinachofanywa viongozi hawa wa soka, maana hata usajili wao ni porojo tu. Hata kama mchezaji husika akiwa na hana uwezo uwanjani, ila kwa timu za Simba na Yanga atakuzwa.

Atakuzwa kwa magazeti. Ataandikiwa vichwa vya habari vinavyozalisha sifa zisizokuwa na tija. Hii si njia nzuri kwa ajili ya kukuza na kuendeleza soka letu hapa nchini.

Tufanye kazi kwa kuangalia namna gani Tanzania inaweza kusonga mbele na sio kuweka mzaha. Timu kama Simba iliyoanzishwa mwaka 1936, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Yanga kuasisiwa, imekosa jipya.

Leo hii wanaiangalia timu ya Azam kwa mzaha. Wengine wanafika mbali kwa kusema Azam haiwezi kufanana na Simba kwasababu inamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wakati wao ni timu ya wanachama.

Huu ni uongo uliotukuka. Hata kama ni kweli, lakini bado klabu hizi zinaongozwa na binadamu. Simba ipo chini ya Ismail Aden Rage, wakati Yanga ipo chini ya mfanyabiashara Yusuph Manji.

Hawa nao wanaweza kuziletea mafanikio klabu zao. Watimize wajibu wao. Lakini kuendelea kukalia mtaji mkubwa wa wanachama waliozagaa kila mahali ni udhaifu mkubwa mno.

Angalia, leo hii Simba na Yanga wameona uzandiki na uongo ndio mtaji wa kuonekana wao ni zaidi. Hata usajili wao unagubikwa na utata. Anahitaji kigogo mmoja kufanya usajili.

Huyo ana uwezo wa kubadilisha matokeo au kuwataka wachezaji wagomee kama kuna jambo hajafurahia. Hili mara nyingi linasemwa. Utasikia Fulani ametumwa ahujumu.

Hii inaweza kuwa kweli au uongo. Kama amesajiliwa na kigogo mmoja na anamtegemea kuhusu mshahara wake, kukataa jambo lolote analoweza kuambiwa ni ngumu.

Haya yanatokea na yataendelea kutokea siku zote. Lakini kama timu hizi zitaacha porojo na kuamua kufanya kazi kwa kutetea maslahi ya soka letu Tanzania, hakika nchi itapiga hatua.

Huu ndio ukweli wa mambo. Lakini tukisema tuendelee kupiga porojo zisizokuwa na faida yoyote tuendelee kusubiri hasara. Ndio maana nasema tuendelee kupiga domo, tukichoka tucheze soka.

Ndugu zetu Wakenya ambao miaka kadhaa tulikuwa tunawafunza soka, leo hii nao wamezinduka. Soka lao linafanya vema mno. Wanafanya juhudi kubwa kuliendeleza.

Ndio maana hata wachezaji wao wanaonekana katika Mataifa makubwa, akiwamo Victor Wanyama aliyesajiliwa katika klabu ya Southampton ya Uingereza, akitokea Celtic.

Katika vitu vingi tunavyoshiriki na Wakenya wanatuacha mbali. Hata huu mchezo wa riadha ndio kabisa. Hii ni kwasababu sisi tunajua porojo na wenzetu wanajua kucheza pamoja na kuweka mipango.

Hakika siwezi kuvumilia, maana hatuna jipya tunalofanya kila siku zaidi ya hadithi ya sungura na fisi. Nalisema hili bila kuangalia matokeo ya Mkutano Mkuu wa Simba uliotarajiwa kufanyika Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Tusipokuwa makini, kila mwaka tutapiga soga na kulidumaza soka letu na michezo kwa ujumla maana hakuna jipya. Hali hii ni mbaya mno na lazima tujuwe ugonjwa wetu kabla ya kutafuta dawa ya kututibu.
+255 712 053949

No comments:

Post a Comment