Pages

Pages

Monday, July 01, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Kwa Simba hii haiwezi kumheshimu Juma Kaseja

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mfululizo wa makala zangu, niliwahi kuelezea kasumba wanazokutana nazo wasemaji wa klabu za Tanzania, hasa za Simba na Yanga.
 Juma Kaseja akichupa kuudaka mpira katika moja ya mechi za mpira wa miguu Tanzania.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Msemaji wa Simba alikuwa ni Ezekiel Kamwaga na yule wa Yanga akiwa ni Louis Sendeu, ambao wote wameondoka kwenye timu hizo, tena kwa matatizo makubwa.
Bila kuficha, Sendeu alinipigia simu akinilaumu sana, akisema maneno niliyosema katika makala yangu, japo yalikuwa ni ukweli, ila yataeleweka yametoka kwenye vinywa vyao, hivyo kupigia kelele kitumbua chake kuingizwa mchanga.

Sikumshangaa Sendeu, maana lazima atetee kibarua chake. Wakati Sendeu anailalamikia makala yangu, Kamwaga aliyeacha kazi Simba, kwa madai kuwa mkataba wake umekwisha, yeye aliisoma ile makala na kunipigia simu pia, tukajadili hili na lile, ukizingatia kuwa ilikuwa ni kuwatetea wao.

Ninachokumbuka ni kuwa Simba, ikiwa chini ya Ismail Aden Rage, aliilalamikia ile makala yangu, akimlaumu pia Kamwaga kuwa huenda maaandishi yangu yalitoka kwake.

Maudhui ya makala yangu, yalitokana na namna wasemaji wanavyokuwa vitumishi na wasioheshimiwa. Wanaopewa kazi nyingi bila mapumziko. Hata hivyo haitoshi, mshahara wao ni wa kubabaisha.

Kama Sendeu aliniona mimi mjinga, basi leo akiisoma makala hii atakumbuka kitu, maana aliachwa kama mwana mkiwa.

Nasema hivi baada ya kuona kuwa kinachoendelea ndani ya Simba kwa sasa, hasa kutangaza kuwa kiwango cha Juma Kaseja, kipa wao kimeshuka ni jambo la kawaida mno.

Kwa viongozi wa Simba, chini ya Rage na jopo lake kauli kama hizo ni rahisi kutolewa na kumuacha kwa mizengwe pia. Mtambuka msemaji wa zamani wa Simba, Criford Ndimbo alivyozalilishwa kwa maneno ya kejeli.

Mtambuka wanachama wa Simba kutokea tawi la Mpira Pesa walivyotukanwa. Kwa wale wasiokuwa na kumbukumbu, Rage aliwaambia Mpira Pesa kuwa kikao chao ni cha harusi na maneno mengine ya dharau.

Hii ni kawaida, ndio maana siwezi Kuvumilia. Kumuacha mchezaji katika timu yoyote ni jambo la kawaida mno. Wengi walisajiliwa kwa gharama kubwa na baadaye kutemwa na kuangalia maisha mengine.

Wapo pia ambao baada ya kugundua mwelekeo mbaya, waligeuka na kuangalia maisha mengine, ukizingatia kuwa hawawezi kucheza Simba au Yanga hadi mwisho wa maisha yao.

Wale walioachwa na umri hupumzika kwa ridhaa yao au kulazimishwa kuachwa katika vikosi vyao, ila si kwa dharau. Yoyote anayemuita Kaseja leo kuwa kiwango chake kimeshuka hakika anashangaza umati.

Kaseja bado yupo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, chini ya kocha wake Kim Poulsen na kusimama langoni kila mechi. Mchezaji aliyeshuka kiwango hawezi kung’ang’aniwa kwenye timu ya Taifa.

Kaseja hana kiwango wakati katika msimu mzima wa ligi yeye amesimama langoni kwa mechi nyingi zaidi? Hii inashangaza Dunia. Bila kuacha unazi juu ya kipa huyu, ila ni dhahiri viongozi wa Simba wameamua kumdhalilisha kwa faida zao.

Kuna jambo moja tu Simba wanaweza kufanya na kikawaongezea pia mapato ya kusajili wachezaji wengine, kwa kuandaa hata bonanza la mashabiki wa Simba, wenye mapenzi na Kaseja kwa ajili ya kumuaga na wakavuna shilingi.

Kila mtu atapenda kumuaga Kaseja kama kweli anaachwa na timu yake, maana amecheza Simba kwa mapenzi makubwa na kuisaidia kwa kila aina. Ni mwendawazimu tu anayeweza kumdhalilisha Kaseja Tanzania.

Tanzania nzima sasa imegawanyika juu ya Kaseja. Kila mtu anasema lake, anaelemea zaidi kumtetea maana kinachofanywa na Simba kinachekesha. Pamoja na yote hayo, ukweli unabaki pale pale kuwa Kwa Simba hii haiwezi kumheshimu Kaseja.

Tangu lini asiyekuwa na nidhamu akamheshimu mtu mwingine? Wafanye wanavyotaka, ila ubabaishaji huu haujaanza leo japo ndani ya uongozi wa Rage, Mbunge wa Taboro Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeongezeka mara dufu, hivyo wadau wa soka, wapenzi na wanachama wa Simba wanapaswa kumuangalia mara mbilimbili.

Mungu ibariki Tanzania.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment