Pages

Pages

Wednesday, July 31, 2013

MGODI UNAOTEMBEA:Nautafuta utukufu wa Samuel Sitta ndani ya CCM

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI jambo lisilowezekana hata kidogo kukaa wiki moja au mbili bila kuona tamko lolote kutoka kinywani mwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta.


 Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, akizungumza jambo. Lowassa ametajwa katika mbio za urais mwaka 2015.

 Mwenyekiti wa CCM, akiwa kwenye kazi za chama chake. Jakaya Kikwete pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha mwaka (2005-2010).

Kiti cha sita baadaye kilikaliwa na Spika Anne Makinda, ambapo bila woga wala soni, Sitta aliwaambia wafuasi wake kuwa nafasi yake imehujumiwa kwasababu ya kuchukia ufisadi.

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akizungumza na Mwana CCM mwenzake, Rostam Aziz kushoto. Rostam aliachia ngazi nafasi zake ukiwamo ubunge kwa madai ya kuchafuliwa.

Waziri Sitta amesema hayo, akiamini kuwa mafisadi wamehujumu cheo chake kwa kisingizio cha jinsia. Yani mwanamke ashike nafasi hiyo ambayo yeye hakutaka iwe hivyo.
Mengi amekuwa akisema, lakini anasahau kuwa hata yeye alipoingia katika nafasi hiyo mwaka 2005, ililazimika kumuondoa Spika Pius Msekwa, akiitwa ‘Agano la Kale’.

Samuel Sitta, pichani
Nani asiyejua utawala wa Sitta bungeni ulivyokuwa na mshike mshike mwingi kiasi cha kumlazimisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ajiuzulu nafasi hiyo mwaka 2008, akisema kuwa tatizo ni Uwaziri Mkuu.

Nimekuwa nikifuatilia kwa kina maneno ya Sitta kila wakati, huku nikiamini kuwa mengi anayotoa, anayatumia kama mtaji wake kisiasa, akiwashughulikia wabaya wake kwa kisingizio cha kuuchukia ufisadi uliotuwama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sitta anapotembea magharibi na mashariki kupinga ufisadi wa viongozi wengine wa serikali inayoongozwa na chama chake, hakika kinachekesha watu walionuna.

Ni kiongozi wa serikali kwa kupitia CCM anayoituhumu usiku na mchana bila kujua athari zinazoweza kukiangusha chama chao.

Ni kutokana na hayo, naendelea kupekua huku na kule kuutafuta utukufu wa Sitta, ndani ya CCM na serikali kwa ujumla.

Inawezekana wapo watu ambao ni wachafu, ila kwa ujasili huo huo anaousema mtaani, basi angeutumia kuwataja watu hao ama kupeleka ushahidi wake mahakamani ili tufanye kazi kivitendo zaidi badala ya porojo zisizokuwa na tija.

Kwanini Sitta amekuwa akiidhalilisha CCM, japo mwenyewe kwa utashi wake anaamini unafurahisha baadhi yao?

Usafi wa Sitta unatoka wapi? Haiwezekani. Hii ni kwasababu Sitta ni miongoni mwa watu wanaotumia fedha nyingi bungeni wakati Watanzania wengi wanaishi kwa kubangaiza.

Sijamuona Sitta akipinga ulaji huo kwa wanasiasa ambao wengi wao wapo bungeni kulala, kupiga makofi, kufanyiana fitina na kusaini posho za vikao, wakati walimu, askari polisi, madaktari wanaofanya kazi ngumu ya kuokoa roho za watu wakiishi kwa mshahara mdogo.

Watu hawa hawajui kesho yao itakuwaje na ndio maana tumeshuhudia walimu wengi wakishindwa kuhudhuria sehemu zao kazi kutokana na changamoto wanazokutana nazo.

Akiwa kama Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ana fursa ya kuingia katika vikao mbalimbali vya Baraza la Mawaziri, ameridhika na kuingizwa kwa hoja ya kulipia simcard kwa Sh 1000 kwa mwezi.

Mpango huu umekuwa mchungu kwa Tanzania kwa sasa, huku vyama vya siasa na viongozi mbalimbali wakipaza sauti zao, akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, John Mnyika, Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wengineo kutoka chama tawala na upinzani.

Sitta anajua kuwa vipo vijiji vingi vinavyostahili umeme lakini tangu nchi ipate uhuru havijawahi kupewa huduma hiyo muhimu na kila siku yamekuwa yakisemwa katika kila vikao vya Bunge?

Je, anajua kuwa watoto wa wapiga kura wake kule Urambo wanasaga na rumba, wakivuja jasho, huku yeye akibaki mjini kutoa matamko ya kuwatusi au kuwadhalilisha viongozi wenzake?.

Huu ni mgogoro gani kama kweli upo kati ya Sitta na viongozi wengine kutoka ndani ya serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, moja ya viongozi wanaofanya kazi nzuri kiasi cha kuwafanya waje kukumbukwa usiku na mchana?

Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alijiuzulu uwaziri mkuu wake huku akitoa lawama kwa baadhi ya watu waliokuwa wakitolea macho nafasi yake hiyo, kabla ya kuhusishwa na kashfa ya Kampuni tata ya kufua Umeme ya Richmond.

Ndio hapo matamko mengi ya Sitta yanapoingizwa kwenye kejeli kwa Lowassa, hasa kwa hoja zake za ufisadi, akiamini zitakuwa mbeleko katika mchakato wake kisiasa.

Labda hayo yanapamba moto kutokana na spidi ya Lowassa, mmoja wa watu wenye wingi wa watu wanaomuunga mkono. Kila pembe ya nchi anatajwa usiku na mchana.

Ingawa si mjuzi wa vuta nikuvute ya machaguo ya urais hasa ndani ya CCM, ila ni ngumu mno kumfanya Lowassa ashindwe kwenye mchakato huo kama atahitaji nafasi hiyo mwaka 2015.

Japo hajatangaza wazi juu ya adhma hiyo, lakini Lowassa anatajwa sambamba na wanachama wengine wa CCM, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Sitta asiyelala kwa ajili ya kutangaza mabaya ya wenzake, bila kujua kuwa kauli zake ni kama bomu kwa chama chake.

Ni kwasababu Watanzania wengi siku hizi tumezoea kuishi kwa kukariri. Ama tunaishi kwa mazoea. Kama hivyo sivyo, basi mmoja ajitokeze hadharani kumuuliza Sitta juu ya kukaa kwenye CCM ya mafisadi na wenye majungu?

Kama Rais Kikwete alimuhujumu kwenye uspika, kwanini alikubali uwaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Nafasi ambayo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wenzetu, hasa wale wanaofanya kazi ya kutoka nje ya mipaka yetu katika Bara hili wanaishi kwa kuhabatisha.

Watanzania hao wakiwapo madereva wanaishi kwa manyanyaso ya aina yake, hasa nchi za Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi, pale watu hao wanapotaka kuingia au kutoka.

Ningetaka kuona utendaji kazi wa Sitta juu ya manyanyaso ya Watanzania hao kwa kuimarisha ushirikiano kama cheo chake kinavyosema, badala ya kuikandamiza CCM miaka nenda rudi.

Ndio, Sitta ametangaza kung’atuka katika ubunge ifikapo mwaka 2015, ila sitaki kuamini kuwa hana ndoto za kuona chama chake kinaendelea kuwa lulu ya Watanzania wote.

Ama Sitta anataka CCM ife? Najua Sitta ni miongoni mwa wanasiasa makini, ila si sahihi kuendelea na malumbano yasiyokijenga chama chake, akiamini ndio njia ya kuwasulubu wabaya wake.

Tunahitaji kauli thabiti na utendaji kazi uliotukuka kutoka katika kinywa cha Sitta. Endapo anaona chama kinakwenda ndivyo sivyo, basi awe wa kwanza yeye kusimama hadharani na kukemea na sio kubaki nusu kuzimu na nusu peponi.

Nayasema haya nikiamini Sitta ataona jambo jema la kufanya kwa ajili ya Tanzania. Hatuhitaji tena kupoteza muda.

Tunahitaji vitendo, maana siasa zisizokuwa na tija ndio zilizotufikisha hapa. Kuna mengi ya kufanya kwa ajili ya kufanikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.

Mnyukano unaofanywa na Sitta dhidi ya serikali yake una faida gani? Anajenga au anabomoa? Sitta ana mapenzi na CCM au lengo lake ni chama hicho kutoweka katika historia ya Taifa letu?

Waswahili wanaamini kuwa mwanamke anayetumia muda wake mwingi kuunadi upungufu wa mume wake basi huyo si muungwana. Hana sifa stahili za kuwa mke wa ndoa.

Huyo ana lake jambo. Ama ameingia katika ndoa hiyo kwa ajili ya kuondoa mkosi au pia kuna kitu amefuata hapo, hasa maslahi.

Hili si tusi kwake, maana aliwahi kuitoa dhidi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, akisema kuwa mara nyingi yanayojiri baada ya ndoa huwa hayaonekanai kwenye uchumba.

Haya Sitta anayajua. Mnyukano wao kisiasa waufanye ndani ya vikao halali vya chama, ili apate nafasi ya kuwatumikia Watanzania.

Huo ndio ukweli wa mambo. Japo kuusema kunahitaji moyo, ukizingatia kuwa hali ya siasa ilivyokuwa sasa, imeongeza joto na kuzalisha makundi ya kutisha.

Hao ndio wanaopita huku wakituhumu upande mwingine, huku hoja ya ufisadi ikitumika tofauti kwa kila mtu asiyekubaliana naye.

Hatuwezi kwenda hivyo. Tujaribu kuwa waungwana, maana maneno mengi yanayotolewa katika jamii yamekuwa hayana tija.

Tunatumia vibaya nafasi zetu na kuwapotezea muda wao bure, huku tukijua fika ugumu wa maisha wanaokutana nao mtaani kwao.

Tutumie fursa zetu vizuri kwa ajili ya maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kuwa rasilimali watu, rasilimali fedha na maliasili zote kwa Taifa zinanufaisha watu wote.

Hata iweje, bado siwezi kumtofautisha mbunge yoyote ndani ya CCM au Waziri, hasa wale wanaotumia muda mwingi kutusi wenzao ili waonekane wapo sahihi.

Watu watajiuliza na baadaye kupata majibu sahihi, hasa kwa kukiwajibisha chama tawala CCM.

Ama hajui kuwa maneno yanaumba na wapo watakaofuata ushauri wake, matusi yake dhidi ya viongozi wenzake na chama kwa ujumla, wakati siku zote tunaambiwa samaki mmoja akioza ni wote?

Je, huo utukufu wa Sitta utaendelea kubaki mioyoni mwa Watanzania hata kama muda wake mwingi aliutumia kumtusi Kikwete, Lowassa na wengine anaopingana nao ndani ya CCM?
+255 712 053949

No comments:

Post a Comment