Pages

Pages

Saturday, July 06, 2013

Mashindano ya Gambo yamalizika wilayani Korogwe, huku timu ya Mtonga ikitwaa ubingwa huo


Siku ya uzinduzi wa Gambo Cup, wilayani Korogwe. Kushoto ni Mkuu wa wilaya Korogwe, Mrisho Gambo akiafutiwa na Ridhiwan Kikwete.

TIMU ya Mtonga FC imetwaa ubingwa wa michuano ya Gambo Cup na kukabidhiwa kombe, ng’ombe, jezi seti moja na mipira miwili, baada ya kuifunga Korogwe United mabao 2-1, katika fainali iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu wilayani hapa.

Mashindano hayo yalianzishwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo na kufadhiliwa na Benki ya NMB, kwa lengo la kukuza na kuibua vipaji vya wachezaji wachanga wilayani hapa na yalishirikisha timu 85 kutoka tarafa nne, ambapo yaligharimu Sh milioni 21.4.

Bao la kwanza la Mtonga lilifungwa na Seleman Msagama katika dakika ya 19, baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Miraji Mtoi na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Korogwe United, Feruzi Ponda na kutinga wavuni.

Baada ya bao hilo kuingia, Korogwe United walisawazisha katika dakika ya 33 kupitia kwa Dullah Shauri, aliyetumia uzembe wa mabeki kupachika wavuni bao hilo.

Bao hilo liliweza kuzidisha hasira kwa timu ya Mtonga FC, ambapo walijipanga na kupata bao la pili katika dakika ya 43 kupitia kwa Chale Dafa, baada ya kuunganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Bunu.

Mshindi wa pili ambaye ni timu ya Korogwe United,  walikabidhiwa mbuzi wawili, jezi seti moja na mpira mmoja, wakati mshindi wa tatu, Bungu Kibaoni walipata mbuzi mmoja, jezi seti moja na mpira mmoja, huku mshindi wa nne hadi wa nane wakipewa jezi seti moja na mpira mmoja na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadhi hizo, Gallawa aliwapongeza benki ya NMB kwa kufadhili mashindano hayo ambayo yalileta mwamko mkubwa kwa vijana kupenda soka wilayani humo na kusema umoja waliouonyesha na wananchi katika michuano waupeleke mpaka kwenye shughuli za maendeleo.

Naye Afisa Mawasiliano wa NMB, Josephine Kulwa, alizipongeza timu shiriki na kuahidi kuendelea kusapoti michezo kwa lengo la kuinua kiwango cha mchezo huo.

No comments:

Post a Comment