Pages

Pages

Saturday, July 20, 2013

MAMBO FULANI MUHIMU:Wanaoaminiwa, ndio wanaosaliti marafiki zao


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NAKUSHUKURU kwa wewe unayeguswa na safu hii kiasi cha kutufanya tuendelee kuwa pamoja kila siku ya Mungu, jambo linalonipa amani moyoni.
I love you so much baby.
Naamini tutaendelea kuwa pamoja kila siku kama ya leo, kwa ajili ya kupeana hili na lile hususan kwa mambo yanayohusu mambo ya mapenzi.

Ndugu msomaji wangu, baadhi ya watu wameshindwa kuishi kwa amani kwa sababu za kufanya mambo kutokana na kuambiwa na marafiki zao.

Hii naweza kusema kuwa ni akili za kushikiwa, hivyo kwa namna moja ama nyingine, inasababisha mvurugano katika mambo ya uhusiano wao.

Aidha, watu hao pia hujikuta wakifika mbali zaidi kwa kuwabadilikia marafiki zao na kuwatamani wapenzi au wake zao.

Wale wanaoaminiwa na jamaa zao, hutumia muda huo kujiwekea mazingira ya kuwasaliti marafiki zao, baada ya kufanikiwa kuwarubuni wenzao.

Huo ndio ukweli, maana wapo wanaotumia nafasi hiyo kwa kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na wake au wapenzi wa marafiki zao.

Wanatumia muda huo kujichanganya kimwili kwa watu hao, tena katika nyumba au vitanda vya hao maswahiba zao.

Watu ni wengi ila binadamu ni wachache. Kufanya uchafu wa kimapenzi na wapenzi wa wenzao ni rahisi kwao, ukizingatia kuwa hawaoni uchungu ama kinyaa, wakijifanya wajuzi.

Huwateka kabisa kiakili na kifikra. Hubarikiwa utundu wa kujihusisha na mapenzi na wasichana hao ambao, anajua kuwa ni mali za watu.

Sio wanaume tu. Hata wanawake mandumilakuwili ni wengi mtaani kwetu. Yule msanii wa Bongo Fleva, Samu wa Ukweli alisema hata kwetu wapo.

Tena wanawake ndio kabisa, maana baadhi yao huomba ruhusa kabisa kwa marafiki zao wakitaka kutoka ‘out’ na mashemeji zao.

Wengi wao huingia mtegoni na kushindwa kuvumilia, hivyo kujikuta hisia zao zikitamani kulala nao kitanda kimoja kwa ajili ya kuvunja amri ya sita.

Ndio hapo unapotakiwa kusoma alama za nyakati. Hutakiwi kumuamini rafiki yako hata kidogo. Mambo ya mume au mpenzi wako lazima ufanye wewe mwenyewe maana siku hizi waaminifu ni wachache.

Lazima ujuwe kwamba ukimpa nafasi rafiki yako kwa mambo ya mapenzi, huenda ukapinduliwa na nyumba yako akaenda kuishi yeye.

Wapo wengi mtaani kwetu na huko kwenu pia. Baadaye hulia na kusaga meno. Hudanganya kwa mengi likiwamo ‘sijamuita mumeo kaja mwenyewe’.

Hapo jua huna chako muungwana. Hivyo lazima ujuwe mtu wako wa karibu ana uwezo wa kuwa mbaya yako, endapo umemuachia nafasi kubwa kwa mtu wako, hadi kumuingiza mtegoni.

Jua kabisa mtu wako ana uwezo wa kunyakuliwa kulingana na mwenekano wake. Iwe ni uvaaji, usomi wake, ama uwezo wake wa kifedha.

Haya na mengineyo yanaweza kuifanya ndoa ama uhusiano wako ushindwe kuendelea kutokana na wachokonozi hao kuingia kwenye malavidavi yako.

Hakuna njia ya mkato zaidi ya kuhakikisha kwamba rafiki yako, haingii zaidi kwenye ukaribu na mume au mke wako, pamoja na wale wapenzi.

Kuwa mkali, maana siku zote kunguru muoga hukwepesha ubawa wake. Ingawa baadhi yao huwaachia waume zao ama wake zao nafasi ya kujenga mazoea ya ajabu kwa wenzao, ila hulia kilio cha mbwa.

Ni pale wanapong’amua kwamba mtu wake ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na rafiki yake na kuufanya uhusiano wao uyumbe kama sio kuvunjika.

Akija ndani asubiri sebuleni ila sio kuingia hadi chumbani, huku akijua wewe upo mbali. Ikiwezekana asikae ndani kwa madai anakusubiri wewe.

Ndio ukweli huo. Bila kuwa makini utaibiwa na hao hao marafiki zako, maana uadilifu, uaminifu kwenye uhusiano umekuwa adimu kuliko fedha. 

Kuna kila sababu ya kujiangalia upya kama kweli tunahitaji kuishi kwa amani katika uhusiano wetu, maana mapenzi ya dhati yana utamu wake.

Tukutane wiki ijayo.
0712 053949



No comments:

Post a Comment