Pages

Pages

Saturday, July 27, 2013

MAMBO FULANI MUHIMU:Ndio tatizo la kujirahisi, jichunge mwanakwetu



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI siku nyingine tena tunapokutana katika safu hii inayokujia kila Jumamosi, huku nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja tukielezea mambo ya uhusiano na maisha.
Wawili wapendanao wakitafakari love yao.

Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama nitashindwa kukushuru wewe unayeguswa na safu hii kiasi cha kutufanya tuwe wote kila wiki tukichambua mambo haya ya uhusiano.

Hakika ndio furaha yangu, maana bila wewe safu hii haiwezi kuwa na mashiko kwa namna yoyote ile. Baada ya kusema hayo, nirudi kwenye mada yangu ya wiki hii.

Siku za nyuma nilielezea kujirahisi na namna inavyoleta mkanganyiko kwenye jamii. Kutokana na ugumu wa msichana kumwambia mwanaume kuwa anampenda, baadhi yao hujikuta wakiingia kwenye wasiwasi mkubwa.

Kwa mfano, mwanamke anayemwambia mwanaume kuwa anampenda, siku zote anabaki kwenye presha. Hawezi kujidai katika uhusiano huo.

Pia wapo wanaume wanaotumia udhaifu huo kuwanyanyasa wasichana wa watu kisa wamelazimishwa mapenzi. Ndio hao ambao wanamuachia msichana kila kitu.

Hata msichana akitamani kutoka out na mpenzi wake huyo, dume zima linaweza kujibu sipo tayari, au sina pesa leo. Anajibu hivyo akiamini kuwa mwanamke atatoa yeye.

Haya ndio madhaifu, maana mwanaume huyo anafanya hivyo kwasababu ameyafutwa yeye. Ila kama yeye mwenyewe ndio amesumbuka kumpata mwanamke huyo, hakika angekuwa na nidhamu kwa mpenzi wake.

Linapotokea suala hilo, wasichana wengi wanajikuta wakiishi kwenye wasiwasi wa aina yake. Hawajidai hata kidogo katika uhusiano huo.

Ndio maana kuna kila sababu ya sisi jamii kuwa makini katika suala zima la uhusiano kwa ajili ya faida yetu. Na inapotokea mmoja wetu anaona hapewi ushirikiano kwa mtu anayempenda, basi akubali matokeo.

Kinyume cha hapo atakuwa mtu wa presha siku zote na hata hayo mapenzi hawezi kuyafurahia hata kidogo. Ndio kwanza mtu anaweza kukonda.

Hawezi kuona raha ya mapenzi kama yanavyosemwa na baadhi yao, maana utamu huu una pande mbili. Huu ndio ukweli wa mambo, hivyo tuangalie mara mbilimbili.

Kwa mfano, kuna baadhi ya wasichana ambao siku zote kazi yao ni kuhudumia wanaume. Hii ni kwasababu waliweka mbele sana matamanio yao kwa watu hao.

Ama wao ndio waliojilengesha ili wapendwe au ndio waliojitoa kuwarubuni wanaume hao. Haya ni matatizo makubwa katika suala zima la uhusiano.

Ingawa kila mmoja ana nafasi ya kusema kwa mwenzake anapoona ameshikika kihisia, ila hatuwezi kujilainisha hata kwa wale wasiokuwa tayari.

Kuna haja gani kujitoa kwa mtu asiyekuwa na walau robo ya upendo wa dhati kwa mwenzake? Nini maana ya raha ya upendo, kama faida yetu ni kutumika zaidi hasa kwa suala zima la pesa na matunzo kwa wapenzi wetu?

Hadi leo wapo wanaume wanaotegemea mifuko ya wasichana, wakijilainisha kwasababu wao ndio walioombwa kuingia kwenye uhusiano mahali fulani.

Hii sio kweli na kuna kila sababu ya kujiangalia upya kama tuna lengo la kuishi kwa furaha, maana si kila mahali kunastahili kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.

Kwa kulijua hili, nadhani jamii hasa wasichana watatambua namna gani wapo na wanaume kwenye uhusiano wakati wenzao hawana thamani ya upendo.

Huu ndio ukweli wa mambo na kuna kila sababu ya kujiangalia upya kwa faida yetu, maana kama hatujajipanga katika uhusiano, basi hata maisha yetu yanakuwa ya mashaka.

Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949



No comments:

Post a Comment