Pages

Pages

Wednesday, June 19, 2013

TATOA walijia juu ongezeko la bei ya BIMA na kusema kuwa hawajashirikishwa kwenye mabadiliko hayo



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UMOJA wa Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) umelalamikia ongezeko la bei za bima, ukisema hazijazingatia uhalisia wa soko, pamoja na kukosa uhalali kwa kuwa hazijashirikisha wadau wa sekta ya usafiri pamoja na jamii kwa ujumla.
 Msemamaji wa Umoja wa wamiliki wa Malori Tanzania, Bwana Elias Lukumay akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko ya kampuni yake kuhusiana na ongezeko la bima. Kulia kwake ni Makamu mwenyekiti wa TATOA, Bi Angellina Ngalula.




Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Malori Tanzania, Bi Angellina Ngalula akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko ya umoja wao ya kupanda kwa bei za bima kwa asilimia 400. Kushoto kwake ni msemaji wa TATOA, Bwana Elias Lukumay.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, msemaji wa TATOA Bwana Elias Lukumay, alisema wanasikitishwa na mamlaka ya uthibiti wa bima Tanzania (TIRA) kuongeza malipo ya bima kwa asilimia 400 bila kutoa sababu za msingi lakini pia bila kushirikisha wadau.

‘Majaribio yetu ya kuzungumza na TIRA yameshindika baada ya TIRA kutojibu barua wala mawasiliano rasmi ya kukutana nao, tofauti na makubalino yetu ya kikao cha mwezi wa pili, kati yetu na wao ambapo tulikubaliana kuwa na kikao kabla ya mazungumzo baina ya wadau na umma juu ya swala hili’ alisema Lukumay.

Akielezea zaidi kuhusu malalamiko hayo, Lukumay alisema vigezo maalumu vya kupandisha bei hizo haviko bayana lakini pia ushindani wa biashara haukuzingatiwa.

‘TATOA inaamini kuna njia nyingi za kufata ili kupandisha bei, lakini kubwa zaidi ni kuacha soko lijiendeshe lenyewe, kwani tuko kwenye soko huria’ alisema Lukumay.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TATOA, Bi Angellina Ngalula, alisema ongezeko hili la bei ni kubwa mno kwa mara moja na litapunguza ushindani wa makampuni ya usafirishaji ya ndani, lakini pia litaongeza bei za usafirishaji kwa kiwango kikubwa sana na hivyo kuumiza uchumi wa nchi na mwananchi wa kawaida ataathirika kwa bei za bidhaa kupanda.

‘Sababu za TIRA kupandisha bei sio za msingi, sababu kama udanganyifu na kuongezeka kwa kesi za bima pamoja na ajali za barabarani, sio sababu tosha za kupandisha bima kwani kufanya hivyo kutaongeza malalamiko zaidi, na pia kuwavunja moyo wateja waaminifu’ alisema Bi Ngalula.

Bi Angellina pia alitoa wito kwa wahusika, yaani TIRA, kuacha tamaa na kutokuendeshwa na genge la makampuni ya bima na kurudi kwenye meza ya majadiliano ili kuweza kupata muafaka kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi kwa maendeleo ya taifa.

‘Bila TIRA kurudi kwenye meza ya majadiliano TATOA itabidi ichukue hatua mbadala kama kwenda mahakamani na kugomea bei hizi mpya, jambo ambalo litasababisha usumbufu kwenye uchumi wetu’ alisitiza Bi Ngalula.

No comments:

Post a Comment