Pages

Pages

Saturday, June 01, 2013

Sudan yaitia hofu Tanzania kupeleka timu zake kushiriki michuano ya Kagame



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imesema italiangalia upya suala la vilabu vya soka vya Tanzania vya Simba, Yanga na Falcon kwenda nchini Sudan kushiriki katika michuano ya Kombe la Kagame ambayo inaandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. 
Bernad Membe, Waziri wa Mambo ya Nje

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernand Membe kuulizwa juu ya usalama wa timu hizo zitakapokwenda jijini Darfur ambako michuano hiyo imeandaliwa. 

Membe amesema mpaka sasa hali ya kiusalama katika mji huo bado haijakaa vizuri kwani wageni wote wanaofika huko hupokelewa kwa magari maalumu ya kuzuia risasi pamoja na nguo ngumu za kuzuia risasi. 

Waziri huyo aliendelea kusema kuwa pia hakuna hoteli nzuri na zenye usalama na kuonyesha kushangazwa na watu waliokubali michuano hiyo ifanyike huko wakati wanajua hali ya kiusalama sio shwari. 

Membe amesema kama wizara kwa kushirikiana na vyombo vinavyohusika vitatoa taarifa za awali kabla ya hawajatoa mapendekezo kinyume chake ili kuzuia uwezekano wa kuzitosa timu zetu sehemu ambayo inaweza kuhatarisha usalama wao. 

Michuano ya Kagame safari hii imepangwa kufanyika katika miji ya Darfur ya Kaskazini pamoja na Gordofan ya Kusini Kuanzia Juni 18 mpaka Julai 2 mwaka huu ambapo kutakuwa na makundi matatu huku Kundi A likiwa na timu za Merreikh-Elfasher ya Sudan, APR ya Rwanda, Simba ya Tanzania na Elman ya Somalia. 

Wakati kundi B litakuwa na timu za Al-Hilal-Kaduugle ya Sudan, Tusker ya Kenya, Al Nasir ya Sudan Kusini, Falcon ya Zanzibar na Al Ahly Shandi ya sudan huku kundi C likiwa na timu za Yanga ya Tanzania, Express ya Uganda, Ports ya Djibouti na Vital O ya Burundi

No comments:

Post a Comment